Rosa: Mwanamke shujaa anayepambana na Corona Kigoma
- Ni mmoja wa mafundi wachache wanaoendelea kushona barakoa katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji licha ya mwamko mdogo wa watu kuvaa barakoa.
- Pamoja na kuokoa maisha ya watu, barakoa zimemsaidia kumuinua kimaisha.
- Ni kimbilio la wengi wanaotaka kujikinga na janga hilo katika mji huo.
Kigoma/Ujiji. Kilomita nane nje kidogo ya katikati mwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Rosa Bruno yupo bize akikata kitambaa cha blu juu ya cherehani yake.
Pamoja naye ndani ya chumba cha wastani wa futi saba kwa nane, yupo fundi mwingine anayeendelea na shughuli zake za kushona gauni.
Tofauti na mwenzie anayeshona mavazi, Rosa anaandaa barakoa, moja ya bidhaa muhimu ulimwenguni katika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Uviko-19).
Fundi huyu wa nguo, si mashuhuri tu kwa mavazi, bali ni moja ya mafundi wachache katika manispaa hii ya magharibi mwa Tanzania anayeendelea kutoa huduma ya kushonesha barakoa.
Sehemu kubwa ya mafundi nguo katika mji huu hawatoi kipaumbele katika utengenezaji wa barakoa na baadhi hata ukiwafuata kuwataka wakutengenezee hawapo tayari kukushonea kwa kuwa na maslahi kidogo.
Katika Mtaa wa Kasimbu na maeneo ya jirani ya hadi kata ya Kagera, Rosa amepata umashuhuri kwa kushona vifaa hivyo vinavyosisitizwa na wataalamu wa afya kuvaliwa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa kama sokoni na kwenye vyombo vya usafiri.
“Siwezi kuacha kushona barakoa hata kama watu wachache wanazivaa, nitaendelea kuokoa maisha ya wote,” anasema Rosa huku akimalizia kukata kitambaa kwa ajili ya barakoa.
Rosa anashona barakoa za vitambaa mbalimbali vikiwemo vitenge kulingana na mahitaji ya mteja ikiwa ni moja ya njia ya kujiingizia kipato na kuokoa wakazi wenzie wa Mkoa wa Kigoma na Uviko-19.
Uamuzi wa dada huyo kuanza kushona barakoa ulikuja baada ya kubaini kuwa barakoa za viwandani zilizokuwa zikiuzwa kwenye maduka ya dawa muhimu zilikuwa ni ghali zaidi kiasi cha wakazi wengi wa manispaa hiyo kushindwa kumudu.
“Walianza kuuza barakoa moja ya dukani Sh2,000 wakati Corona imeingia mwaka jana, hii ilikuwa hela nyingi sana. Wakashusha hadi Sh1,500 bado ilikuwa kubwa kwa hali zetu,” anasema.
Kutokana gharama hizo, Rosa (28) anaeleza kuwa aliona fursa ya kutengeneza barakoa ambazo alianza kwa kuziuza Sh1,000 na baadaye kuzishusha bei hadi Sh500 licha ya gharama za uzalishaji kuongezeka ili kusaidia watu wengi wapate barakoa.
Rosa akiwa kwenye eneo lake la kazi la kushonea barakoa ambazo anawauzia wakazi wa Kigoma/Ujiji ili wajikinge na ugonjwa huo. Picha| Gift Mijoe.
Wakati huo, mafundi wengi wa nguo akiwemo yeye, walikuwa wakitengeneza barakoa kwa kitambaa kimoja ambacho hakikuwa imara zaidi kuwakinga watu na maambukizi ya ugonjwa huo.
“Wataalamu walituelimisha kuwa barakoa za kitambaa kimoja siyo madhubuti, ikabidi tuanze kuiga barakoa za viwandani na kuanza kuweka kitambaa laini ndani na kigumu nje zifanane na za dukani,” anasimulia huku akitabasamu kwa aibu.
Katika manispaa hii, ni watu wachache sana wanaonekana wakiwa wamevalia barakoa licha ya Serikali kuendelea kusisitiza watu wajikinge na wimbi la tatu la Uviko-19 ambalo limeshapoteza maisha ya watu zaidi ya milioni 4 ulimwenguni kote kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa Tanzania, hadi Julai 8, kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima kulikuwa na wagonjwa 408 ikiwa ni ongezeko la takriban mara nne ya wagonjwa 100 walioripotiwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 28 mwaka huu. Zaidi ya nusu ya wagonjwa hao au wagonjwa 284 wanatumia tiba ya oksijeni.
Sehemu kubwa ya watu wachache wanaonekana kuvaa barakoa hizo hapa Kigoma mjini ni wale wanaoingia katika ofisi za umma au hospitali kupata huduma.
Tabia za baadhi ya wakazi hawa kutofuata maelekezo ya wataalamu wa afya kujikinga na ugonjwa huo, kulifanya baadhi ya mafundi cherehani wachache waliokuwa wakitoa huduma hiyo mapema mwaka jana kubwaga manyanga.
“Mwaka jana nilikuwa nauza kati ya barakoa 70 hadi 100 kwa siku lakini kwa sasa ni watu wachache wanaonunua,” anasema mama huyo wa watoto wawili.
“Ni mtu mmoja mmoja tu ndiyo anayekuja kununua barakoa.”
Kutokana na kuuza idadi ndogo ya barakoa na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, Rosa ambaye amefanya bidhaa hizo kama sehemu ya biashara, ameongeza bei hadi Sh1,000 kutoka Sh500 ya mwaka jana.
Tofuati na barakoa za viwandani ambazo mtumiaji atahitajika kuzinunua mara kwa mara kujikinga, barakoa za kushonesha zinadumu muda mrefu ili mradi ziwe zinafuliwa mara kwa mara.
Barakoa za vitambaa zinawasaidia watu wengi wasiokuwa na uwezo akiwemo Abdi Mbango mkazi wa Mtaa wa Mashine Kasimbu aliyesema hana fedha za kuwanunulia wanawe na wajukuu barakoa kila siku kutokana na ukata.
Rosa akiandaa vitambaa kwa ajili ya kuunganisha ili kupata barakoo. Mwanamke huyo ni miongoni mwa mafundi cherehani ambaye anaendelea kutengeneza bidhaa hiyo ili kuokoa maisha ya watu. Picha| Gift Mijoe.
Wakati mahitaji ya barakoa yalipokuwa makubwa mwaka jana, Rosa anasema kuwa alikuwa amewaajiri vijana wawili kwa ajili ya kuzisambaza barakoa hizo kwenye maeneo ya masoko na madukani.
Kila kijana alikuwa akijipatia faida Sh100 kwa kila barakoa aliyokuwa akiuza baada ya kuzichukua kwa fundi huyo. Rosa alikuwa akiwapatia wauze barakoa moja kwa Sh900.
Tofauti na nguo ambazo hutumia muda mrefu kuziandaa, Rosa anasema barakoa zimemsaidia kupata mapato mengi zaidi yaliyochangia kuboresha maisha yake kwa kuwa ndani ya dakika 15 anaweza kushona mbili zenye thamani ya Sh2,000.
“Mwaka jana kwa siku ulikuwa unapata kuanzia Sh20,000 au Sh30,000 kwa siku na hapo umefanya kazi kwa saa chache tu,” anasema.
Mapato hayo ambayo ni makubwa kupata kwa siku kulingana na asili ya kazi yake, anasema yalimsiadia kuchangia ujenzi wa nyumba wanayokaa na mumewe na kumudu gharama za kila siku za maisha.
Kwa sasa, Rosa ambaye anavaa barakoa kwenye ofisi yake licha ya kuwa wawili tu, anasema watu hawana muamko wa kujikinga na Corona na anaamini kwa kuwa Serikali imeshaanza kutangaza huenda wakaamka siku zijazo.
“Najisikia furaha sana kuwa naendelea kushona barakoa zinazosaidia kuokoa maisha ya watu,” anasema huku akinipatia barakoa ya bluu aliyokuwa akiishona kwa takriban dakika 10 wakati tukiendelea na sehemu ya mahojiano yetu.
Fundi huyo anawasihi watu wanaopuuza maelekezo ya wataalamu wa afya kuanza kuchukua tahadhari za kunawa mikono na sabuni mara kwa mara kwa maji tirirka, kuachiana mita moja na kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko.
Makala hii imeandaliwa kwa ushirika na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest
