Machifu wa Tanzania wanavyopambana na ugonjwa wa Corona

September 14, 2021 1:44 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Baadhi ya machifu wa Tanzania waliohudhuria Tamasha la Utamaduni ambalo limefanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Msalaba Mwekundu eneo la Bujora wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza. Picha| Mariam John.


  • Wanatumia nyimbo, ngoma, mikusanyiko kuhamasisha watu kuchukua tahadhari.
  • Matambiko, dua na dawa za kienyeji nazo wanazitumia kutoa ahueni.
  • Wahamasisha Watanzani kupata chanjo ya Uviko-19.

Mwanza. Mapambano dhidi ya janga la Corona (Uviko-19) yanaendelea kwa silaha mbalimbali ikiwemo utoaji chanjo na kuwahusisha wadau mbalimbali kwenye jamii ili kuwalinda watu na janga hilo.

Nchini Tanzania, umoja wa machifu unashirikiana kwa karibu na Serikali ya nchi hiyo kuelimisha jamii kujikinga dhidi ugonjwa huo kwa namna mbalimbali ikiwemo nyimbo za asili, dua na ngoma katika shughuli zao za kitamaduni na mila.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu Tanzania, Aron Mikomangwa amesema katika kipindi cha majanga makubwa kama Uviko-19 hutumia fursa ya mikuanyiko ya watu kuwaelimisha kwa nyimbo, ngoma na ngonjera ili wachukue tahadhari ya kujikinga.

“Kuna masuala kama haya ya Corona, huwa zinatungwa nyimbo ambazo zinawafundisha watu ili kujihadhari na gonjwa hili, hata zamani wakati wa magonjwa mengine yaliyokuwa yanawamaliza watu kulikuwa na mambo ya namna hiyo,” amesema Mikomangwa.

Chifu huyo wa kabila la Wasukuma alikuwa akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) katika Tamasha la Utamaduni ambalo limefanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Msalaba Mwekundu eneo la Bujora wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza.

Katika tamasha hilo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi amesimikwa rasmi kuwa mkuu wa machifu Tanzania na kupewa jina la Hangaya (nyota inayong’aa).

“Tunahamasisha watu kwa ajili ya kwenda kupata chanjo na kuwashauri kama Serikali ilivyotangaza,” amesema Chifu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro anayejulikana kwa jina la Jabil. 

Amesema licha kuwashauri watu kufuata miongozo ya Serikali na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono, kuvaa barakoa na kupata chanjo ya Uviko-19 lakini wanatumia njia ya dua ili Mungu aiepushe Tanzania na janga hilo.

“Lakini tunatumia maombi ambayo huwa tunaomba kwa ajili ya Mwenyezi Mungu atuepushe nayo. Tunaomba kwa lugha zetu za kimila, tunapofanya vile kuomba kwa lugha ambazo siyo za kufundishwa, hizo Mwenyezi Mungu anazipokea haraka,” amesema Chifu Jabil.

                           

Ameishauri Serikali kuwaweka katika makundi ambayo watatambulika kirahisi kwenye jamii ili kuondoa dhana ya kuwaona kama ni waganga wa kienyeji wasio na msaada kwenye jamii hasa yanapotokea majanga makubwa kama Uviko-19.

Pia viongozi hao wakimila wamesema wanatumia dawa za asili ili kuwasaidia watu wanaopata magonjwa ya kupumua ikiwemo Uviko-19 kupata ahueni.

“Pia tunatumia miti shamba kutengeneza dawa zinazoweza kusaidia katika kujikinga na kutibu magonjwa ya aina hiyo,” amesema Chifu Route wa Wilaya ya Rorya mkoani  Mara huku akibainisha kuwa matambiko pia hufanyika ya kuombea matatizo ya magonjwa kuondoka kwenye jamii.

Janga la Uviko-19 limeathiri uchumi wa dunia na nchi mbalimbali, hivyo kuunganisha nguvu za wadau inaweza kuwa ni silaha ya kuushindwa ugonjwa huo kwa haraka.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW