Rais Samia apata chanjo ya Corona, awatoa hofu Watanzania

July 28, 2021 9:17 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Amechanjwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
  • Awatoa hofu Watanzania kwa sababu chanjo hiyo ni salama.
  • Awataka kupuuza uzushi kuhusu madhara ya chanjo hiyo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo amechanjwa chanjo ya Corona (Uviko-19) huku akiwatoa hofu Watanzania kuhusu kupata chanjo hiyo kwa sababu ni salama na itasaidia kupunguza madhara ya janga hilo vikiwemo vifo.

Rais Samia amepata chanjo aina ya Johnson & Johnson iliyotengenezwa nchini Marekani leo Julai 28, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam pamoja na viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. 

Rais Samia amesema, kama kiongozi wa nchi ambaye pia anategemewa siyo tu na Watanzania, bali na familia yake pia, hawezi kuyatoa maisha yake kwa kupata chanjo ambayo haina usalama.

“Mimi ni mama wa watoto wanne wanaonitegemea. Ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaonipenda sana nami nawapenda sana. Ni mke pia lakini mbali ya yote ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya nchi hii. 

“Nisingejitoa mwenyewe nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yote haya yananitegemea,” amesema Rais Samia muda mfupi kabla ya kupata chanjo hiyo.

Amewataka Watanzania kuepukana na uzushi ambao unasambaa mtandaoni kuhusiana na madhara ya chanjo dhidi ya Uviko-19.

Amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni hiari na wanaoipuuza watafakari madhara ya ugonjwa huo ikiwemo kwa familia kupoteza wapendwa wao ambao walikuwa ni nguzo muhimu za maisha.

“Nenda leo Moshi, nenda Arusha, nenda Kagera hata Dar es Salaam, uonane na zile koo ambazo wameshaguswa na haya maradhi, wana maneno ya kukuambia na kama wangeweza wote wangekuwa leo hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara waliyoipata,” amesema Rais Samia kuacha kuwavunja moyo watu wenye nia ya kupata chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Serikali za ugonjwa wa Uviko-19 hadi Julai 23, 2021, watu 858 wamegundulika na kupata maambukizi ya ugonjwa huo huku  watu 29 wakipoteza maisha.

“Nenda leo Moshi, nenda Arusha, nenda Kagera hata Dar es Salaam, uonane na zile koo ambazo wameshaguswa na haya maradhi, wana maneno ya kukuambia. Picha| Ikulu Mawasiliano.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema chanjo ya Johnnson & Johnson (Jassen) inayotolewa Tanzania ni chanjo iliyoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutumika katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo bara la Afrika.

“Na hizi taarifa kwamba imesitishwa ni uongo, haya mambo yalikuwa Aprili kule mwanzoni,” amesema Dk Gwajima.

Waziri huyo mwenye dhamana ya afya amewataka Watanzania kutokuwa na hofu ya madhara madogo madogo yanayotokana watakayopata baada ya kupata chanjo hiyo kwa sababu ni za muda mfupi.

Chanjo ya Jassen imepokelewa nchini Tanzania kwa msaada wa Marekani Julai 24, 2021 ambapo kipaumbele kitatolewa kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele kupambana na Uviko-19, wazee na watu wenye magonjwa sugu katika hatua za awali.

Mbali na chanjo ya Jassen, Tanzania inatarajia kupokea aina nyingine za chanjo kadri muda utakavyokuwa unaenda.

Dk Gwajima amesema “chanjo zitakuja aina si moja, ni tano. Kutakuwa na Moderna inakuja, kutakuwa na Pfizer tumeipendekeza kutakuwa na hii Johnson&Johnson inakuja, kutakuwa na Sinopharm na Sinovac  na zingine zote ambazo tutakuwa tunazikubali kupitia kamati yetu.” 

Waziri huyo amesema chanjo hiyo itasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na Uviko-19, kupunguza makali ya ugonjwa kutoka ugonjwa mkali kuja ugonjwa wa kawaida na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazwa na kuwekewa oksijeni.

“Kila mwenye swali, kila mwenye hoja, anayehitaji ufafanuzi, tunampelekea fursa mpaka mlangoni kwake kwa teknolojia au hata ana kwa ana kupitia mtandao wa wataalamu wetu ili aweze kuamua kwa usahihi na kwa haraka bila hofu,” amesema Dk Gwajima.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV