Siyo kweli: Askofu Gwajima hajachanjwa chanjo ya Corona
- Amezushiwa kuwa amepata chanjo hiyo nchini Kenya.
- Yeye ashikilia msimamo wake kuwa hatachanjwa chanjo ya Corona.
Dar es Salaam. Kufuatiwa kuwepo taarifa zinazodai kuwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na Mbunge wa Kawe, Dk Josephat Gwajima amechanjwa chanjo ya Corona, amejitokeza na kusema yeye hajachanjwa chanjo hiyo kama anavyozushiwa.
Taarifa hizo zinazosambaa mtandaoni zikiwa na cheti cha Uviko-19 cha nchini Kenya chenye picha ya Dk Gwajima zinaeleza kuwa tayari Askofu huyo ameshapata chanjo aina ya AstraZeneca Oxford tangu Februari 2020.

Hata hivyo, taarifa hiyo siyo ya kweli kwa sababu ina mashaka mbalimbali ambayo yanaifanya iwe ya kizushi na upotoshaji.
Ukweli uko wapi?
Askofu Gwajima ameendelea kushirikia msimamo wake kuwa yeye hatachanjwa chanjo ya Corona pamoja na waumini wa kanisa lake kwa kile alichodai kuwa zina madhara ya kiafya.
Kupitia katika ukurasa wake wa Instagram, Dk Gwajima amesema uzushi unaosambazwa kuwa amepata chanjo nchini Kenya siyo kweli na kusisitiza kuwa “nilishasema mimi sichanjwi na sitachanjiwa chanjo ya Corona.”
Sehemu ya ujumbe alioandika Dk Gwajima katika ukurasa wake wa Instagram akikanusha madai ya kuchanja chanjo ya Corona.
Hata hivyo, mpaka sasa Wizara ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO) hawajaripoti madhara ya kiafya kwa watu waliopata chanjo ambazo zimethibitishwa ikiwemo ya Johnson & Johnson ambayo imeanza kutumika Tanzania.
Pia timu ya Nukta Fakti imetumia zana za kidijitali ikiwemo “Google Explore” na “QR & Barcode Scanner” kubaini ukweli wa cheti hicho na imegundua cheti hicho siyo cha Dk Gwajima bali kimegushiwa ili kuwapotosha watu.
Cheti hicho ni cha raia wa Kenya anayeitwa Oliver Mathenge aliyepata tayari chanjo hiyo.
Kilichofanyika, cheti hicho kimehaririwa kwa kuongezewa picha ya Gwajima ambapo kwa vyeti vya watu waliopata chanjo ya Corona nchini Kenya havina picha ya muhusika kama ilivyo kwenye cheti halisi cha Mathenge.
Mashaka mengine yanayothibitisha kuwa cheti hicho siyo sahihi ni kwenye tarehe ya kutolewa kwa dozi za chanjo. Cheti cha Gwajima ambacho ni feki kinaonyesha amepata chanjo kati ya Februari na Aprili 2020, jambo ambalo siyo la kweli kwa sababu wakati huo Kenya ilikuwa bado haijaanza kutoa chanjo ya Corona.
Cheti halisi cha Mathenge kinaonyesha kuwa amepata dozi mbili ya chanjo ya AstraZeneca kati ya Machi na Juni mwaka huu, jambo ambalo ni sahihi kwa mujibu wa mifumo ya taarifa za Wizara ya afya ya Kenya.

Licha ya kuwa wananchi wanahimizwa kupata chanjo ya Corona kwa hiari bila kulazimishwa, wametakiwa kupata taarifa muhimu kuhusu chanjo kutoka kwa mamlaka za afya zinazotambulika na Serikali huku viongozi wenye dhamana kwenye jamii kuacha kupotosha wananchi kuhusu chanjo.
Habari hii imeandikwa na Tulinagwe Malopa na Daniel Samson.
Latest