Penzi linavyovunja mnyororo wa maisha
- Inamhusu mwanababa anayelazimika kubadili maisha yake baada ya mrembo kupita machoni kwake.
- Mrembo huyo anavunja siri ya kuwa maisha ya bachela huyo ni gemu la video.
Katika maisha yako, kuna mtu ambaye anafanya ulimwengu wako usimame. Anasababisha uone dunia inazunguka taratibu huku watu wengine wakiwa kwenye ukungu.
Ni mtu ambaye anaingia kwenye ulimwengu wako kukubadilisha na kukufanya uzidi kuwa bora zaidi.
Kama ilivyo Romeo kwa Juliet, Rose kwa Jack na kwa muktadha huu, Millie kwa Guy.
Edd Sheeran amewahi kuimba kuwa watu hudondoka kwenye huba kwa namna mbali mbali ikiwepo mguso tu wa mkono. Ni wimbo wake unaojulikana kama “Thinking out loud”.
Wataalamu wa haya mambo wanaweza fahamu kuwa kinachoongelewa hapa, ni “love at first sight” yaani kuzama katika mapenzi kwa mtu unayemuona kwa mara ya kwanza. Guy alipomuona Millie, dunia yake yote ilisambaratika na kumbakisha yeye na mwanadada huyo tu.
Huenda nimekupeleka haraka kidogo, wacha tuanze kwa kumfahamu Guy ni nani.
Guy kama watu wengine, ni kijana anayeishi maisha ya kawaida. Kila siku ataamka, atajiandaa na ataenda kazini kwake.Guy ni mhasibu katika benki ya humo kwenye filamu hii ya Free Guy.
Guy anapokutana na Millie, dunia yake yote inabadirika. Picha| Et online.
Kuna vitu vingi vinavyomtofautisha Guy na vijana wengine lakini kikubwa ni kijana huyo kuwa na ratiba ile ile kila siku za maisha yake.
Kila siku Guy ataamka na kujiandaa na kazi, lazima kuna mtu atapata ajali na kila anapofika ofisini kwake, lazima majambazi waje kuiba kwenye benki hiyo
Ni maisha ya Guy ya kila siku lakini pale anapokutana na Millie, yote hayo yanabadilika.
Millie na Guy kuvunja mnyororo wa maisha yaliyozoeleka
Huenda ni kitu kimoja tu ambacho kinaweza kuwa kwenye mzunguko ule ule kila siku. Ni gemu la video lililotengenezwa kwa ajili kumpatia tu burudani.
Kila siku sehemu ya kuanzia ni ile ile, majambazi ni wale wale, silaha zinazotumika ni zile zile na hata visa ni vile vile.
“Kuna kitu nataka kukuambia” Millie anamueleza Guy huku sauti yake ikionyesha wazi kuwa kinachofuata ni jambo ambalo Guy hatolifurahia.
“Umeolewa?” guy anauliza. “Hapana” Millie anajibu na Guy anashusha pumzi kwani kwake anaweza kupokea habari yoyote mbaya lakini siyo ya kuwa Millie ana mpenzi mwingine.
Inachekesha jinsi mapenzi yanaweza kukufanya ukawa hamnazo kidogo.
Ukimya wa tafakari unapita na Millie anamweleza Guy ukweli ambao unamwacha taya za mdomo wake zikiwa zimekaribia kugusa shindo.
“Hatupo kwenye maisha ya ukweli. Tupo kwenye gemu la video,” Millie anamwaga mchele kwenye kuku wengi.
Mbaya zaidi ni kuwa mwenye gemu hilo ana mawazo ya kuliteketeza gemu hilo na wahusika wake hivyo wawili hao wana siku mbili tu kubadilisha hilo.
Baada ya kugundua kuwa maisa yake yote amekuwa ni mhusika tu kwenye gemu, Guy anaambua kubadilisha maisha yake. Picha| Polygon.
Guy ambaye alikuwa anaishi maisha yale yale kila siku anabadilika. Gemu linatarajia awe benki, majambazi wakija kuiba wamkute, wamwambie alale chini naye alale na gemu liendelee.
Wewe utafanyaje endapo siku mtu atakuambia maisha yako yoote sio halisi? Ni gemu ambalo kuna mtu huko analicheza na wewe ni mhusika tu kwenye gemu hilo.
Sijui wewe utafanyaje lakini Guy anadhamiria kuokoa wahusika wenzake kwa kupigana kufa na kupona hata kama ikimgharimu maisha yake.
Kutafuta furaha, kuvunja sheria na kuufahamu ukweli usiopingika ni sehemu ya filamu hii yenye nyota kutoka filamu ya “Deadpool,” Ryan Reynolds na mwanadada aliyetikisa kwenye filamu ya Killing eve, Jodie Comer.
Fuatilia filamu hii kuanzia Agosti 13 katika kumbi za kuangalizia filamu au popote unapopata filamu zako.
Usiache kulike podcast yetu, kusubscribe na kumtumia mdau mwingine wa filamu.
Latest