Maagizo ya Rais Samia kwa mabalozi aliowaapisha

August 21, 2021 6:59 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Matarajio yake kwao ni kutanguliza  maslahi ya Tanzania kimataifa.
  • Awataka kutafuta fursa za uwekezaji na kudumisha diplomasia.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza mabalozi walioapishwa kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, kutafuta fursa katika nchi hizo na kusimamia maslahi ya Taifa ili kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Agosti 21, 2021 wakati akiwaapisha mabalozi hao Ikulu jijini Dar es Salaam. 

Walioapiswa ni pamoja na Balozi Luteni Jenerali Yakub Hassan Mohamed ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Uturuki na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo.

Balozi Elsie Sia Kanza anaenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.

“Nakumbuka tarehe 27 Julai mwaka huu niliwaeleza wenzenu kuwa jukumu na matarajio yangu kwenu ni kuendeleza diplomasia ya uchumi kama sera yetu inavyosema,” amekumbushia Rais Samia alichokisema wakati akiapisha mabalozi wengine mwezi uliopita.

Rais Samia pia amesema anatarajia mabalozi hao kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani,  kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania wanaoishi nje na kutafuta fursa za biashara na uwekezaji kwenye taasisi za kimataifa.

Katika maagizo yake, Rais Samia amemuagiza Balozi Kanza kuhakikisha uhusiano kati ya Tanzania na Marekani unaendelea kuimarika na pia aanze kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Mexico.

“Ubalozi wa Marekani pia unaratibu shughuli za Benki ya Dunia na shughuli za Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kwa uzoefu ulioupata kwenye mashirika haya, sina wasiwasi utatuwakilisha vizuri,” amesema Rais Samia kwa Balozi Kanza.

Naye Balozi Kombo, ameagizwa kuendelea kuchochea uwekezaji unaofanywa na raia wa Italia nchini Tanzania ili kuikuza zaidi sekta ya utalii nchini ambayo imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka nchi hiyo ya Ulaya.

Pia amemuagiza Balozi kombo kuongeza fursa za elimu kwa Watanzania katika nchi ya Malta.

Amemuagiza kudumisha uhusiano kati ya Shirika la Chakula Duniani (WFP) na Tanzania kuongeza idadi ya chakula kinachonunuliwa Tanzania ili wakulima wapate soko la kuhakika.

Kwa Balozi Mohamed ametakiwa kuanzisha miradi ya ubia kati ya Tanzania na Uturuki kwa sababu “wametutangulia kiteknolojia.”

Mbali na mabalozi walioapishwa leo, mwingine ni Profesa Elisante Ole Gabriel aliyeapishwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye ameagizwa kusimamia haki na kuchochea maendeleo ya mahakama nchini.

“Una jukumu la kuuendeleza jitihada zilizoanzishwa za kuimarisha matumizi ya Tehama ndani ya mfumo wa mahakama,” amesema Rais Samia akibainisha kuwa hilo litasaidia kuboresha na kurahisisha shughuli za mahakama nchini.

Kabla ya kiapo chake, Profesa Gabriel alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi upande wa mifugo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW