Yaliyomo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa
- Ni moja ya hifadhi zinazopatikana kanda ya ziwa.
- Imesheheni vivituo vingi ikiwemo mito, maziwa na wanyama.
- Ifikika kwa usafiri wa ndege na magari.
Dar es Salaam. Tunaelekea robo ya tatu ya mwaka 2021, umepata muda wa kumpumzika baada ya shughuli nyingi? Kama bado, Kanda ya Ziwa kuna pepo inayokusubiri.
Siyo nyingine bali ni Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa inayopatikana magharibi mwa  Mkoa wa Kagera. Imesheheni uzuri wa kila namna wa wanyama, milima, mabonde, maziwa na mito.Â
Hifadhi hiyo ambayo ni miongoni mwa hifadhi 22 zilizopo Tanzania ina ukubwa wa kilomita za mraba 200 huku hali ya hewa katika hifadhi hiyo ipo katika misimu miwili ya mvua kwa mwaka: kipindi kirefu  cha mvua kuanzia Machi mpaka Mei na kipindi kifupi cha mvua kuanzia Oktoba hadi Novemba.
Hifadhi ya Ibanda-Kyerwa imesheheni kila aina ya vivutio wakiwemo wanyamapori kama swala. Picha| Tanapa.
Kwa nini ukatalii Ibanda-Kyerwa?
Shughuli za utalii unazoweza kufanya ukiwa katika hifadhi hiyo ni pamoja na kuendesha gari mchana na usiku, kuweka kambi katika hifadhi hiyo, chakula cha msituni, kutazama ndege pamoja na kutembea kwa miguu ili kujionea uumbaji wa Mungu katika hifadhi hiyo.
Aidha, hifadhi hiyo imejaaliwa vivutio mbalimbali ikiwemo savana, maziwa , mito na mabwawa yanayokaliwa na wanyamapori wa aina tofauti kama vile nyati wa Afrika, viboko, chui, swala na ndege wa aina tofauti.
Pia utajionea nyasi za wazi za savana, maziwa yaliyotawanyika, milima , mabonde, Mto Kagera na bustani zenye kila namna ya maua.
Ili kufika katika hifadhi hiyo  kwa  njia ya barabara ni  mwendo wa kilomita 220 kutoka Bukoba Mjini kwenda Murongo  au kilomita 372 kutoka Chato mkoani Geita hadi Murongo na pia kutoka nchiniUganda kupitia mji wa Murongo ambao uko karibu na hifadhi kwa kilomita 3.5.
​Pia kwa njia ya angani unaweza kutumia usafiri ndege kokote ulipo hadi katika uwanja wa ndege wa Chato na kisha unachukua usafiri wa barabara mpaka kwenye hifadhi hiyo ambapo ni mwendo wa kilomita 372.
Latest