Ziwa Victoria: Moyo wa Afrika Mashariki

December 11, 2021 5:40 am · Nasibu
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ziwa linalotegemewa na wananchi wa Tanzania, Kenya na Uganda.
  • Limebeba historia muhimu ya Tanzania.
  • Ni kitovu cha utalii ukanda wa maziwa makuu.

Maji ni uhai na shida huwa haziishi penye uhaba au ukosefu wa maji. Tafakari kidogo!

Nimejaribu kuwaza maisha ya Afrika Mashariki bila Ziwa Victoria na kichwa kiligonga na macho yakauma mithili ya mtu anayetahabika kufungua macho yake hadi mwisho ili aweze kuona kwenye giza nene. Kwanini?

Ziwa Victoria ni moja ya maziwa makuu ya Afrika Mashariki. Ni ziwa ambalo limebahatika kuwa kwenye mstari wa ikweta na limezungukwa na nchi tatu za Afrika Mashariki: Tanzania, Kenya na Uganda.

Ziwa Victoria ni chanzo cha Mto Nile wenye urefu wa kilomita 6,650 na urefu huo unaufanya kuwa mto mrefu zaidi duniani ingawa vyanzo vingine vinakinzana na taarifa hiyo.

Mto Nile unakatiza nchi tano barani Afrika zikiwemo Uganda, Sudan, Sudan ya Kusini, Ethiopia na Misri. Kila nchi mto huu ukatizapo unaacha neema kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii, biashara, kilimo na usafirishaji.

Makala hii ni fursa kwako msomaji kujivunia uzuri na upekee wa Ziwa Victoria, ziwa ambalo binafsi nimeona nilitunuku jina la ‘Moyo wa Afrika Mashariki’ na labda mwishoni utakubaliana na mimi.


Historia

Hapo zamani Ziwa Victoria lilijulikana kama Ziwa Nyanza, baada ya John Speke na Richard Burton ambao ni wazungu wa kwanza kuligundua ziwa hilo waliamua kuliita Ziwa Victoria wakimtunuku malkia wa Uingereza Queen Victoria, mwaka 1858. 

Lakini pia inasemekana Waarabu waliwahi kufika ziwani hapo mwaka 1160 na kufanikiwa kutengeneza ramani ya ziwa hilo.

Muonekano wa ziwa Victoria karibu na mji wa Musoma mkoani Mara. Picha| Wikimedia Commons.

Eneo

Ziwa Victoria ndiyo ziwa kubwa zaidi barani Afrika na lina ukubwa wa kilomita za mraba 68,800.

Duniani, ni ziwa la pili kwa ukubwa likitanguliwa na Ziwa Superior lililopo Amerika ya kaskazini, kwa ukubwa huu nchi za Rwanda na Burundi zinaweza kuwa visiwa ndani ya ziwa hili.


Watumiaji

Ziwa hili linahudumia wakazi takribani milioni 40 wa Afrika Mashariki na chakula ambacho ni samaki wa aina ya sato na sangara.

Ziwa Victoria lina kina cha mita 84, ambao ni zaidi kidogo ya robo tatu ya uwanja wa mpira wa miguu.

Ziwa Victoria lina umri wa takribani miaka 400,000. Wewe unataka kuishi mingapi, ndugu?


Chanzo cha Ziwa Victoria 

Asilimia 80 ya maji yote ya Ziwa Victoria yanatokana na mvua, asilimia 20 nyingine huchangiwa na mito inayomwaga maji yake ndani ya ziwa hilo, ukiwepo Mto Kagera.

Masomo ya jiografia yanasema kwamba mara kadhaa Ziwa hili hukauka kabisa na mara ya mwisho kukauka ilikuwa miaka 17,000 iliyopita. 

Na pia kama unakumbuka au kama ulikuwa umezaliwa mnamo Mei 21 mwaka 1996, kulitokea ajali ya meli ya MV Bukoba kuzama ziwani hapa na kupoteza maisha ya watu takribani 1,000. Ajali hii inasemekana kuwa ni moja ya majanga makubwa kuwahi kutokea kwenye usafiri wa majini katika ziwa hilo.


Soma zaidi


Utalii ziwani Victoria

Ziwa Victoria ni kivutio chenye vivutio vingi ndani yake, utalii wa kanda ya ziwa ni mkubwa sana kana kwamba nitahitaji makala mbili kuelezea kiundani ila nitajitahidi kueleweka kwenye hii moja:

Bismarck Rock

Mwamba wa Bismarck au Jiwe la Bismarck, unaweza ukamwelezea mtu jinsi huu mwamba ulivyo na anaweza asiamini mpaka aone mwenyewe, lakini kwa kifupi ni mwamba huu umekaa mawe mengi yamepangwa juu ya mengine na upepo kidogo unaweza kuyaangusha mawe hayo kudumbukia ziwani lakini ndio lipo hivyo miaka yote.


Fukwe za Ziwa Victoria

Kama vile Dar Es Salaam au Zanzibar kulivyo na bahari na fukwe za kupumzika basi hata ziwani pia burudani haitofautiani sana. Mwanza kuna Tunza Resort, Bukoba kuna Bunena Stone Beach na Musoma kuna Palm Beach.

Ziwa Victoria lina visiwa zaidi ya 900 lakini ni visiwa 34 tu ambavyo vina makazi ya binadamu na vyote vinafikika kwa safari za boti kujionea tamaduni za jamii ziishio kwenye visiwa hivyo ikiwemo jamii ya Wakerewe.


Hifadhi za Taifa

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambacho kipo magharibi kusini mwa ziwa hilo na kinajulikana kwa kuwa na sokwe, viboko na swala na uoto wa asili.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ambayo ina miaka saba tangu iwe hifadhi, inasifika kuwa na uoto wa asili na wanyama kama mamba, kobe, chui, swala, nyoka na nyani wa kipekee waitwao debraza wanapatikana katika hifadhi hiyo pekee nchini.

Kufika katika visiwa hivi ni kwa kupitia Mwanza mjini kwa gari au ndege na kuelekea visiwani kwa boti. Je, umesikia mpango wa Serikali wa kulikutanisha Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti?

Moja ya kivutio muhimu katika Ziwa Victoria ni uwepo wa visiwa mbalimbali vinakaliwa na watu pamoja na wanyama. Picha| Tanzania Hotels Agent.

Vihatarishi vya Ziwa Victoria

Ziwa Victoria linakumbwa na matatizo ambayo yanaweza kuteketeza viumbe hai vyote vilivyopo majini humo, matatizo hayo yakiwemo: 

1. Uchafuzi wa Mazingira.Utupaji taka ziwani toka kwenye miji iliyopo kando ya ziwa ikiwemo miji kama Bukoba, Mwanza na Musoma ya Tanzania; Kisumu, Kendu Bay na Homa Bay ya Kenya na Kampala, Entebbe na Jinja ya Uganda

2. Uoto wa magugu maji. Mimea inayokwamisha shughuli zingine kuendelea. 

3. Uvuvi uliyokithiri kutokana ongezeko la uhitaji ya samaki hii pia inatokana na ongezeko la idadi ya watu waishio kwenye ukanda huo.

Utafiti wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Uasilia (IUCN) unaonesha kuwa asilimia 20 ya aina zote za viumbehai katika ziwa hilo waliozingatiwa kwenye utafiti huo wako katika hatari ya kuangamia.

Je, unahisi Ziwa Victoria linastahili jina la ‘Moyo wa Afrika Mashariki?’ 

Kama unakubali, je, unafanya nini kuhakikisha ziwa hili linaendelea kuwa ‘Moyo wa Afrika Mashariki?’ 

Jibu ni rahisi, kwa kuanzia unaweza kusambaza makala hii kwa watu wako wa karibu ili kuhamasisha utumiaji bora wa ziwa hili kwa kutupa taka kwa utaratibu uliyowekwa na mamlaka na kufanya uvuvi kwa kuzingatia vizazi vijavyo.

Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya www.nasibumahinya.com.

Enable Notifications OK No thanks