Afya ya akili yaendelea kuwa gumzo kwa vijana duniani

October 8, 2021 1:45 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inakadiriwa watu bilioni 1 duniani wana changamoto ya afya ya akili.
  • Changamoto hiyo huwafanya baadhi yao kuwa walevi na kujiua.
  • Inashauriwa kujifunza kufunguka na kufanya mazoezi ili kukabiliana na hali hiyo.

Dar es Salaam. Huenda haukumbuki mara ya mwisho kuzungumza na mtu unayemuamini kuhusiana na hisia zako na mambo yanayokutatiza katika maisha yako. 

Yanaweza kuwa ni ugumu wa uchumi, mahusiano, familia au jambo lolote ambalo halipo sawa katika maisha yako.

Ni muhimu kufahamu kuwa, kubaki na jambo moyoni bila kutafuta njia ya kuachia hisia zako inaweza kukusababishia msongo wa mawazo. 

Mfululizo wa matukio yanayokukosesha amani yanaweza kuwa sababu ya kutumbukia katika msongo wa mawazo. kifo, kufukuzwa kazi, magonjwa au unyanyasaji wa kijinsia.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), msongo wa mawazo ni kati ya visababishi vikuu vya ulemavu ikifuatiwa na kujiua ambayo pia ni sababu ya vifo vingi kwa vijana wenye umri wa miaka 15-29.

Jiwazie mema na hakikisha unafunguka pale unapohisi haupo sawa. Picha| Grammarly. 

Ukiangalia kwa makini, zote hizo ni changamoto za afya ya akili.

Takwimu za WHO za mwaka 2020 zimeainisha kuwa takribani watu bilioni 1 duniani wanaishi na matatizo ya afya ya akili ambayo ni chanzo kwa baadhi kujihusisha na ulevi na pia matumizi ya dawa za kulevya. 

Vitendo hivyo (ulevi) ni sababu ya vifo milioni 3 vya watu kila mwaka huku mtu mmoja akifa kila ndani ya sekunde nne kwa kujiua.

Katika nchi zenye uchumi wa kati zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye changamoto za matatizo ya akili hawapati matibabu kabisa.

Gazeti la Hindustan Times la nchini India limeandika kuwa, endapo changamoto za akili ikiwemo msongo wa mawazo hazitotafutiwa ufumbuzi, zinaweza kumsababishia mtu hadi magonjwa ikiwemo magonjwa ya moyo, kupungua kinga ya mwili, saratani, kisukari na upotevu wa kumbukumbu.

Ili kuwa na afya bora ya akili,  WHO inashauri kutafuta mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo ikiwemo kuongea na watu au msaikolojia, kuilisha akili yako maudhui mazuri na chanya kwa kusoma vitabu vinavyoweza kukupatia morali na pia kusaidia wengine pale unapokuwa na uwezo. 

Kwa kujifunza zaidi, Soma hapa

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW