Jinsi ya kusheherekea Maulid kwa wasio Waislamu

October 19, 2021 7:39 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Watafute ndugu ambao hujawasiliana nao muda mrefu.
  • Pia kujenga ukaribu na familia yako.

Dar es Salaam. Kwa waamini wa Kiislamu, Maulid ni siku ambayo ni kumbukumbu ya siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake). 

Muumini wa Kiislamu ambaye ni mdau wa Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesema siku hii huadhimishwa kwa shamrashamra za kumtaja, kumueleza na kusifu mwenendo wa Mtume Mohammad. Ikiwa ni katika njia ya kufurahia kuzaliwa kwake.

Kwenye siku hii, inatarajiwa Waislamu Kumsifu Mtume kwa staha na utulivu na kutoka “sadaqa” kwa watu wanaostahili.

Waumini wa Kiislamu, wanajua nini cha kufanya katika siku hii lakini kwa wasio Waislamu, wengi huitumia kwa njia mbalimbali ikiwemo kutulia nyumbani na familia zao.

Unawezaje kuadhimisha siku hiyo mbali na kukaa nyumbani, haya ni baadhi ya mapendekezo:


Kujumuika na jamaa zako 

Kutokana na majukumu ya kila siku, kwa wenye familia bila shaka wana jamaa ambao hawajaonana kwa muda mrefu. Rafiki zako ambao huenda mmepotezana kwa muda mrefu.

Unaweza kuitumia siku hii kukutana na jamaa zako kadhaa na mkapata kujuliana hali na kubadilishana mawazo.

Kwa mujibu wa Khansa Mohammed, mdau wa Nukta Habari kutoka Zanzibar, anashauri siku hii isiwe siku ya kufanya maovu ikiwemo kulewa na “kutikisa mabuno” badala yake kutoa sadaka kwa wanaostahili.

Kusherehekea na watoto wako

Siku za wiki zimejaa heka heka. Watoto na shule, wewe na kazi kiasi cha kukosa muda hata wa kupiga nao stori mbili tatu za kuboresha mahusiiano yako na wao. Badala ya kuwasaidia kufanya kazi za shule ni kama kawaida yaani “home work”, unaweza kuitumia siku hii kukaa nao na kuongea nao kujua wanachopenda na changamoto wanazopitia.

Maulid ni kati ya siku ambazo pua huumia kwa “minuso” ya biriani, pilau na vyakula vikaangwavyo. Endapo una uwezo mzuri kifedha, siyo haba ukahakikisha watoto wako pia hawaishii kunusa harufu za vyakula vinukiavyo kwa jirani pakee. Mpatie mama uwezo wa kukorofisha jiko.

Jumuika pamoja na familia yako ili muweze kupanga mipango yenu. Picha| Search Engine One. Picha.

Piga ile simu 

Kuna watu ambao wamekutafuta muda mrefu na kutokana na majukumu mengi ya kiofisi ukawaambia utawapigia baadaye na haukufanikiwa.

Kwa kuwa siku hii upo nyumbani, siyo mbaya ukatumia muda huo kuangalia kwenye orodha yako ya simu (call log) kuona ni nani uliahidi kumrudia na haukufanya hivyo.

Pia na jumbe ambazo ulisahau kuzijibu. Na kwa wale wenye ndugu zao wa mkoani, huenda siku ya leo ikawa siyo ya wewe kuwa na kisingizio cha wingi wa majukumu. Wapigie simu uwasalimie pia.

Mimi naenda kwa jirani kutafuta ubwawa, wewe tafuta namna ya kupambana na hali yako. As-salamu alaykum.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW