Msimu wa sikukuu: Utoke au upike nyumbani?
- Wapo wanaopenda kukaa nyumbani ili kujumuika na ndugu na marafiki.
- Wanaopenda kutoka ‘out’ wanataka kutumia muda mwingi na familia kuliko kupika.
- Hata hivyo, sikukuu nzuri ni ile inayowafanya watu kufurahia na kuendeleza upendo kwenye jamii.
Dar es Salaam. Ni siku kadhaa zimesalia kufikia sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya 2021. Kwa wengi siku hizo zilizobaki huenda zikawa zenye hekaheka nyingi za maandalizi ya sherehe hizo yakiwemo ya kununua nguo mpya za watoto, kupanga safari, kufanya manunuzi ya chakula.
Katika siku yenyewe ya sikukuu, baadhi huamua kupika nyumbani huku wengine wakiamua kutoka “out” na familia zao. Kwako ambaye huenda bado haufahamu faida za kila chaguo, huenda maoni haya yaliyokusanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) yakakupatia mwangaza.
Sisi tunatoka!
Sikukuu huwa na pilika nyingi na kwa siku kama Krismasi kwa waumini wa Kikistro, siku huanzia kanisani kwa ajili ya ibada hivyo kutoa muda mchache kwa watu kuandaa vyakula.
Kati ya watu ambao wameamua kutoka na famila zao ni Paul Kadalah, baba aliye na familia ya watu sita. Yeye amesema kwa sikukuu, anaona kuitoa familia yake kupata chakula cha mchana sehemu nyingine ni ahueni kuliko kupika nyumbani.
Kadalah ameiambia Nukta kuwa hadi kufikia chakula kipo mezani, zipo gharama nyingi ambazo zinakuwa zimehusika ukiwemo muda wa kupika, safari za mahemezi, uchovu na kukosa muda wa kufurahia na familia kwa pamoja.
“Ukitoka nje na familia yako, watoto wanapata nafasi nzuri ya kucheza katika maeneo mapya na kumbukumbu wanayobaki nayo juu ya sikukuu hiyo ni kubwa zaidi ya ile watakayotumia nyumbani,” amesema Kadalah ambaye huwa na bajeti isiyovuka Sh500,000 kufanikisha hilo.
Kwa wengine kutoka nje wakati wa sikukuu ni muhimu zaidi kuliko kukaa nyumbani kwa sababu wanapata mazingira tulivu ya kujumuika na familia. Picha|Unsplash.
Kadalah amesema kupika chakula nyumbani kunaweza kuwa jambo jema kama unatarajia ugeni kwa kuwa katika kipindi hiki kunakuwa na uharibifu mwingi wa chakula na kusababisha upotevu wa fedha.
“Ukitoka na famila yako, mtakula chakula huko huko, kula nyumbani hakuna kipya, ni kama Jumapili nyingine tu,” ameongeza Kadalah.
Mara nyingi, katika sikukuu hizi wanaokuwa na jukumu la kuilisha familia ni akina mama na watoto wa kike na baadhi ya watoto wa kiume. Hili huwafanya siku yao kuwa ndefu kwa kuwa wanafanya mambo mengi ili kufanikisha sikukuu hiyo.
Kwa baadhi wenye uwezo ili sikukuu inoge hutoka kabisa nje ya mji wanaoishi na kwenda mahali ambapo familia itafurahia pamoja hususan maeneo tulivu ya kitalii.
Mjasiriamali kutoka Afrika Kusini, Stella Nankya ambaye ni mama wa watoto watano amesema kupika nyumbani huhitaji manunuzi ya vitu vingi kitu ambacho ni ghali zaidi ya kutoka out na famila yake.
Nankya amesema kutoka na familia yake yote humgharimu chini ya Sh2.3 milioni huku maakuli ya nyumbani yakimgharimu zaidi kwa kuwa sikukuu hizo huambatana na gharama za mafuta ya kupikia, maji, umeme, vyakula, matunda, vinywaji na mahitaji mengine lukuki.
“Mimi na familia yangu hupendelea kwenda nje kidogo ya mji tutafikia hotelini na tutakula vyakula vilivyoandaliwa huko, huku tukiwa na muda mwingi pamoja,” ameeleza Nankya.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
Chakula cha nyumbani ni poa zaidi!
Kwa baadhi ya wadau wa sikukuu zijazo, wanaona kupika chakula nyumbani ni bora zaidi kuliko kutoka.
Kati ya wadau hao ni Mariam Shabani ambaye ni mama wa familia yenye watu wanne akiwa yeye, mumewe, mtoto na dada anayewasaidia kazi nyumbani.
Kwa Mariam, kupika nyumbani ni bora zaidi kwani katika sikukuu hupendelea kujumuika na jamaa zake.
“Kupika na kula nyumbani gharama inakuwa nafuu kuliko ukachukua watu wengi na kwenda kula sehemu. Kama ni mimi na mume wangu, yes (ndiyo) tunaweza kwenda kula sehemu,” ameeleza Shabani.
Hata baadhi ya watu ambao hawajaoa au kuolewa nao wanapendelea kupika nyumbani badala ya kwenda kula nje kwenye migahawa na hoteli.
Christian Phillip ambaye bado hajaoa amesema kutoka kunaweza kusiwe kipaumbele hasa siku ya sikukuu kwa kuwa kunakuwa na hatari nyingi zikiwemo wizi, upotevu wa vitu na ajali.
“Ni kweli sipiki lakini teknolojia imerahisisha mambo mengi sana. Nitakaa nyumbani na kualika rafiki wawili watatu, tutaagizia msosi (chakula) kwa njia ya mtandao, tutacheza michezo na kutazama filamu hadi tutakapochoka. Nje huko mara mtu kakukanyaga, amekupaka jasho. Siwezi,” ameeleza Phillip.
Kuna familia nyingine wakati wa sikukuu ndiyo wakati muhimu kwa wanafamilia kukutana na watoto kufurahi pamoja.
Kuna familia nyingine wakati wa sikukuu ndiyo wakati muhimu kwa wanafamilia kukutana na watoto kufurahi pamoja. Picha| Google Unsplash.
Vipi kuhusu hili?
Lawrence Rusere, baba wa familia ya watoto watano, amesema kutoka na familia yako huambatana na baadhi ya changamoto ikiwemo gharama kubwa lakini huwa ni furaha sana hasa kwa watoto kwani huwapatia muda mwingi wa kucheza na kufurahia sikukuu.
Rusere amesema hata kupika nyumbani huwa na changamoto ikiwemo kupika chakula kingi kwa kutarajia wageni wengi ambao baadhi hushindwa kufika.
“Wapo watu huamua kutoka na familia zao na kwenda sehemu za wazi zikiwemo fukwe, hata hivyo gharama huwa kubwa kwani sehemu nyingi hawaruhusu kwenda na chakula chako,” ameeleza Rusere.
Kwa wengine iwe kula nyumbani au hotelini muhimu ni wanafamilia kukutana pamoja kama anavyoeleza Monica Meshack mkazi wa Kakola mkoani Shinyanga.
Monica, mama wa watoto watatu, amesema iwe ‘out’ au iwe nyumbani, muhimu ni familia kuwa pamoja na kutimiza adhma ya sikukuu.
“Kama ni Krismasi, basi watu kweli wafurahie kuzaliwa kwa Mungu (Yesu) na kama ni mwaka mpya, watu wamshukuru Mungu kwa kuuona kwani wapo walioishia njiani (2020),” ameeleza Monica ambaye chaguo lake ni kuwa sehemu atakayofurahia na familia yake yote.
Latest