Kauli, maswali yasiyofaa kumuuliza mtu wako wa karibu

January 3, 2022 4:23 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Unaweza kuuliza kwa lengo zuri lakini isiwe hivyo kwa mtu unayemuuliza.
  • Baadhi ya maswali yanaashiria kuwa unamchunguza mtu.
  • Wengine hupitia changamoto za maisha zinazosababisha wao kuwa kweye hali unayowaona nayo.

Dar es Salaam. Ukitembea tembea barabarani, utaona sura tofauti tofauti. Zipo zinazotabasamu, zilizo na huzuni, usizoweza kutambua hisia zake na hata sura zenye bashasha. 

Hata hivyo, haimaanishi kile kilichopo usoni, ndiyo kipo ndani ya moyo. Wapo wanaovalia sura za tabasamu huku mioyo yao ikiwa na maumivu makali. Yasiyoelezeka kwa kuwatazama.

Hata hivyo, kwa watu ambao huenda haujonana nao kwa muda, unaweza kujikuta kinywa chako kina maswali mengi ya kuwauliza. 

Kati ya maswali na kauli zako, zipo wanazoweza kufurahia na zingine wasipende hata kama hawatokuambia.

Unaweza usiulize au kusema jambo kwa nia mbaya lakini unaweza kujikuta umeumiza hisia za mtu bila kujua kwa kuuliza maswali ambayo unahisi ni kawaida kuuliza lakini kiuhalisia siyo maswali mazuri.

Baadhi ya  maswali yanaweza kumfanya mtu ajihisi duni hatakama alikuwa amejaa furaha. Picha| Ghana Quest.

Ni kauli na maswali gani hayo? Somo hili hapa;

Umenenepa/Umekonda!

Huenda ni kawaida kumshangaa mtu ambaye haujaonana naye kwa muda mrefu. Mabadiliko ya mwili, rangi ya ngozi na muonekano, yanaweza kukufanya uanze kusema mambo yanayoweza kumuumiza mtu.

Maneno kama “ehh, umekonda! Eeh, umenenepa!” yanaweza kuonekana kama kitu cha kawaida lakini wapo wanaoumia na maneno hayo.

Mbunifu wa mavazi na mwandishi wa vitabu, Rahma Bajun kwenye kitabu chake cha “The Wave” ameandika jinsi maswali haya yanavyoumiza moyo.

Bajun amesema siyo maswali mazuri kuuliza kwani haujui sababu ya mtu kuwa na mabadiliko ya mwili. Wapo wanaoumwa na wapo wanaopitia vipindi vigumu vya maisha.

Hata hivyo, kukonda kwao au kunenepa, hakukuhusu.

Haujaoa/ hujaolewa tu!

Linaweza kuwa swali la kutaka kujua hali ya mahusiano ya mtu. Kwa mtu ambaye ameolewa/ ameoa, anaweza kutabasamu na kujibu “tayari” lakini kwa ambaye bado na huenda anataka lakini muoaji au muolewaji hayupo, unaweza kuumiza hisia zake.

Tovuti ya Story Pick, imeandika kuwa, swali hili linaweka msisitizo kuwa mtu kuwa “single”  yaani bila mahusiano ni kosa au dhambi.

Kauli nyingine inayoendana na hii ni “watoto bado?” Hili huelekezwa kwa wanandoa ambao huenda wapo kwenye ndoa kwa muda mrefu lakini  hawajapata au hawajaamua kupata watoto.

Swali hili “linaudhi” na linaingilia faragha ya maisha ya mtu. Story Pick imeandika, swali hilo linaweza kusababisha machozi kwa watu ambao wamehangaika kwa muda mrefu kutafuta watoto.

Unapomuuliza mtu nilini atapata mtoto, haujui mambo anayoyapitia. Picha UT.

Eeh una ujauzito?

Kama haujaambiwa hadi sasa, ujue hayakuhusu. Siyo vyema kuuliza mtu swali hili kama hauna uhakika. Kwenye jukwaa la mijadala ya mtandaoni la Quora, swali hili ni kati ya maswali yaliyotajwa na watu wengi kuwa swali linaloudhi.

Fahamu kuwa siyo kila mwenye tumbo kubwa ni mjamzito. Swali hili kwa mtu ambaye siyo mjamzito linaweza kumfanya ajihisi kasoro kwenye mwili wake hivyo, subiri uambiwe.

Fahamu

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya itifaki na adabu, (etiquette) za biashara na kijamii, Bonnie Tsai wa nchini China, maswali na kauli hizi zinaweza zisipokelewe vizuri na mtu unayemwambia hata kama wewe hauna lengo baya.

Tsai anabainisha kuwa, maswali kuhusu mabadiliko ya mwili yanamaanisha kuwa unamchunguza mtu. 

“Hakuna haja ya wewe kumfanya mtu ajihisi kuwa anatakiwa kuonekana ki namna fulani ambayo inakubalika na wewe au jamii,” ameandika Tsai.

Jifunze kusikiliza watu badala ya kuanza kusema mawazo yako juu ya maisha yao. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW