Huyu ndiye mtu sahihi wa kuanzisha naye mahusiano

November 4, 2021 1:56 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatakiwi kuwa bendera fuata upepo bali mtu mwenye ndoto.
  • Anatakiwa kuwa nyongeza ya pale wewe unapopungukiwa.
  • Ni mtu ambaye anakuweka mbele na siyo kukuficha ficha kama dhambi.

Dar es Salaam. Kuna vitu ambavyo havionekani kwa macho. Inahitaji hisia za moyo na kuzama kwenye ulimwengu wa kufikirika ili kujihisi mnufaika.

Mfano hisia ya kupendwa. Kiuhalisia, haihitaji vitu vya kushikika bali ni kushiba kwa nafsi kutokana na umbali ambao mtu anaweza kwenda kuthibitisha kuwa anakupenda.

Pesa, maua, chakula na “viji outing” vinaweza kuwa nyongeza tu lakini mtu kuahirisha kwenda kazini kwa ajili yako, mtu kuachana na pombe ili awe na wewe na mwingine kujiweka mbele yako unapokuwa hatarini, huo ndiyo upendo. Huo ndiyo mtazamo wangu.

Usinihisi vibaya. Siyo kwamba mimi ni daktari wa mapenzi lakini hakika ninaijua hisia ya kupendwa na kupenda pia. 

Kuanzia moyo kwenda mbiyo pale simu yangu isipojibiwa kwa wakati, kupata makasiriko nisipomuona mpenzi wangu, kuumia pale ninapomkosea na mengineyo, nimepitia. 

Hilo tu, linatosha walau kukupa sababu ya kutilia maanani ninayoyaandika.

Hata hivyo, kwa baadhi huenda ikawa ni njiapanda kubwa kwao juu ya mahusiano waliyonayo na kama mtu aliyenaye ni sahihi kwake.

Mazungumzo yangu na Msaikolojia wa masuala ya elimu kutoka Singida, Yohana Samuel yamenielewesha kuwa, kuna mtu sahihi kwa ajili ya mahusiano lakini pia kwa ajili ya ndoa.

Na pia inawezekana mtu akawa sahihi kwa ajili ya mahusiano tu lakini asiwe sahihi kwa ndoa. Hivyo huenda kuna sababu ya vijana wengi waliopo kwenye mahusiano kupunguza matarajio kwa wenzi wao. Walau si kwa kuwapatia asilimia 100.

Samuel amesema, “kuna mtu unaweza kuwa naye kwenye mahusiano lakini ukitaka kumuoa au kuolewa naye nafsi inasema hapana. Unaona siyo sahihi.” 

Kuhusu ndoa tutayazungumzia wiki ijayo lakini leo tuangalie mtu sahihi kwa ajili ya mahusiano anatakiwa kuwa na sifa zipi.

Akufaaye ni yule anayehuzunika kwenye huzuni zako na anafurahia kwenye furaha zako. Picha| Atlanta Black Star.

Uhuru wa kijamii

Mtu sahihi ni yule ambaye utakuwa huru naye kufanya mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo “videti” vya hapa na pale, matembezi, kusapotiana kwenye kazi zenu na pia kukufariji kwenye siku ambazo mambo yanaenda kombo.

Msaikolojia Jonathan Marshall kupitia chapisho la Business Insider Africa amesema, unaweza kujua mtu ni sahihi kwa jinsi anavyokujali siku unazokuwa unajihisi upo chini na hauna amani. 

Atakujenga na kufurahia mafanikio yako.


Kuendana, mtazamo kwenye mambo mbalimbali

Utajisikiaje pale unapotofautina karibu kila kitu na mtu ambaye upo naye kwenye mahusiano? Bila shaka jibu ni vibaya.

Wakati wewe unaamini hiki, yeye hakiamini na anaamini kile. Ni bora kiwe kitu kimoja lakini vipi kama ni mambo mengi?

Samuel amesema mtu sahihi kwa mahusiano ni yule ambaye walau mna mtazamo sawa kimaisha na mnaendana.

“Ukisema nataka kusoma kitabu na yeye aseme eeh afadhali tuanze pamoja,” amesema Samuel.

Mtu ambaye anaweza kukutoa kwenye reli ya mahusiano ni yule ambaye jibu lake ni hapana kwenye kila kitu unachotaka kufanya naye. Iwe kwenda outing, kufanya mazoezi, kuanzisha kitu na kwa baadhi kupiga picha.

Apite mtihani wa baa

Siyo lazima iwe sehemu ya tungi. Inaweza kuwa sehemu yeyote ya watu wengi. Endapo utakuwa na mtu ambaye kila mara anaangaza angaza pembeni kana kwamba ana hofu ya kufumaniwa, huyo anaweza asiwe mtu wako. Bila shaka mtakuwa wengi  kwenye huo moyo wake.

Marshall amesema, mnapokuwa kwenye sehemu ya watu wengi, mtu sahihi kwa ajili yako ataweka umakini wake wote kwako na macho yake muda wote yatakuwa yakistaajabu bahati yake ya kuwa na wewe licha ya mamilioni kukutolea macho.

Hebu chukua “bae” wako siku moja na mwende sehemu ya wazi uone kama kweli wewe ndiye au na wewe unasindikiza wengine. Yatakayokukuta mimi simo lakini.

Kama kila kitu unachokisema jibu lake ni hapana, hiyo siyo ishara nzuri. Picha| Hakeem Oyato (twitter).

Sikio, bega na hifadhi

Mtu ambaye upo naye kwenye mahusiano anatakiwa kuwa bega lako la kuegemea pale unapohisi dunia inakudondokea pia sikio la kusikiliza matatizo yako.

Mtu ambaye upo naye kwenye mahusiano anatakiwa kuwa na shauku ya kukufahamu zaidi. Kwa sababu ni mtu ambaye anakupenda, anatakiwa siyo tu kujua rangi unazopenda. 

Ajue wapi atapata msaada pale wewe utakapoumwa, awajue nyumbani kwenu walau awe na pa kuanza kujielezea pale unapokuwa kwenye shida.

Siyo rangi, chakula unachopenda na tarehe yako ya kuzaliwa. Mapenzi yanaenda mbali na hayo. Anatakiwa ajue cha kufanya ukikasirika na hata kuwa tayari kufanya jambo kwa ajili yako hata kama hataki. 

Siyo maneno yangu, ni maneno ya Wanasaikolojia Samuel na Marshall.

Hata hivyo, mtu pia anatakiwa kuwa na mipaka na siyo kila kitu ni sawa. Kama umeangalia filamu ya “Coming to America” sehemu ya pili, historia ya mapenzi ya Mwana Mfalme Hakeem ndiyo ninayoiongelea hapa.

Awe mtu mwenye ndoto na anafanya juhudi na mipango  ya kuzifikia. Siyo mkia wako wa wewe ulipo naye awepo.Katika mahusiano, unahitaji mtu wa kukujenga kimaisha na kuongeza pale wewe unapopungua. 

Wiki ijayo, tukutane kwa ajili ya mtu sahihi kwa ajili ya ndoa. Yapo mengi kutoka kwa Samuel ambaye pia ni mwanandoa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW