Ufanye nini kama unahisi rafiki, ndugu wanakupuuza?
- Unashauriwa kujiridhisha kuwa anakupuuzia kwa makusudi au laa.
- Unaweza kutafuta muda na kumwambia hisia zako ili kufahamu mawazo yake.
- Kuwa mwelewa kwani wakati mwingine watu wanapitia kwenye vipindi vigumu.
Dar es Salaam. Hisia za kupuuzwa zinaambatana na mawazo mengi. Unapokuwa kwenye hali hiyo, kati ya vitu unavyoweza kuhisi ni pamoja na kujishuku kuwa huenda kuna kosa umefanya dhidi ya watu fulani.
Inaweza ikawa ni rafiki yako, ndugu na hata mpenzi wako anayekufanya ujihisi hivyo. Hali hii hutokea kwa baadhi pale wanapotuma ujumbe au kupiga simu na wasipate majibu yoyote kutoka kwa mtu wanayewasiliana naye.
Ni katika kipindi hicho ambacho unaanza kuhoji thamani yako kwa mtu huyo na kujiuliza kama na wewe unapaswa kushika 50 zako na kusonga mbele, au kubaki ukivumilia kwani huenda mtu huyo anapitia kwenye kipindi ambacho amepoteza haiba yake.
Kabla ya kuchukua maamuzi magumu ambayo yakasababisha ukampoteza mtu sahihi katika maisha yako, nakushauri uzingatie yafuatayo:
Jihakikishie kuwa ni kweli unapuuzwa au laa!
Wakati mwingine, siyo kwamba unapuuzwa bali ni tabia ya mtu. Moja ya rafiki zangu ambaye nitamuita Kelvin kwa sasa kumtuniza siri yake, aliwahi kunielezea sababu za kwanini hajibu meseji kwa wakati.
Nilimuelewa kwani hata mimi, kuna muda nakua na hali hiyo.
Kelvin aliniambia, anaweza akawa yupo mtandaoni (online) lakini haihitaji mawasiliano na mtu yeyote. Siyo ndugu, siyo mpenzi wala rafiki. Hataki kuwasiliana lakini anataka kuwa mtandaoni kuperuzi mambo mbalimbali.
“Saa zingine mtu anaweza kunitumia ujumbe nikauona, nikaufungua nikausoma na nikasahau kujibu. Watu wengi wananilalamikia lakini ndivyo nilivyo na wengi wamenizoea,” anasema Kelvin.
Hivyo kabla haujatumbukia kwenye bwawa la hasira, jitahidi kufahamu hali ya mtu huyo na kama ni kawaida yake kufanya hivyo au laa.
Wakati mwingine watu huhitaji kuwa peke yao na hivyo kujiweka mbali na mawasiliano. Picha| The conversation.
Mpatie mtu muda
Huwezi kujua ni kwa nini hajajibu simu au ujumbe wako. Huenda kuishiwa salio, kuibiwa simu, kuwa kwenye majukumu yanayomzuia kutumia simu au hata kusahau.
Tovuti ya masuala ya mahusiano, Pivot inaeleza kuwa kabla ya kuchukua uamuuzi wowote ni muhimu kupiga hatua moja nyuma na kumsikilizia mtu huyo kwani huenda anahitaji muda wa kuwa peke yake.
Bila shaka hata wewe kuna muda ambao hautaki kuwasiliana na mtu yeyote. Huenda naye yupo kwenye hali yiyo.
Fahamu kinachomsumbua
Unaweza kuhisi mtu anakupuuzia lakini kumbe moyoni mwake kuna simanzi na matatizo kibao. Ni muhimu kukaa chini na mtu huyo kuyazungumza mambo yanayowasumbua.
Tovuti ya kuandika masuala mtambuka ya trending us imeandika, “endapo kweli mtu anakupuuzia, ni muhimu pia kufahamu kama ni wewe una makosa au yupo kwenye hisia zake binafsi.”
Baada ya kumpa nafasi, unaweza kutafuta muda wa kuongea naye na kutatua tofauti kama zipo.
Mbali na hayo, unashauriwa kutokufikiria sana na kuchukua maamuzi magumu kisa tu haujajibiwa ujumbe.
Endapo utazingatia hayo, huenda itakuepusha kuandika meseji za “usinitafute tena au samahani kwa usumbufu, nimejua umuhimu wangu kwako” fahamu kuwa, siyo wewe tu ndiyo una matatizo. Hata wengine wanayo.
Latest
