Ahueni kidogo: Bei za petroli, dizeli zashuka Tanzania
- Bei ya petroli imeshuka kwa kati ya Sh4 hadi Sh 35 kwa lita
- Kushuka kwa bei kumechangiwa na Serikali kuondoa baadhi ya tozo.
Dar es Salaam. Angalau sasa watumiaji wa vyombo vya moto watapata ahueni kidogo baada ya bei za mafuta ya petroli na dizeli kushuka Januari mwaka huu.
Mwaka 2021 uliisha kwa maumivu kutokana na bei za bidhaa hizo kupanda zaidi mwishoni mwa mwaka kiasi cha kufikia hadi Sh2,510 kwa lita ya petroli jijini Dar es Salaam. Mikoa mingine ya pembezoni mwa Tanzania iliyo mbali na bandari bei zilikuwa juu zaidi.
Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Umeme (Ewura) leo Januari 4, 2022 imetangaza bei mpya elekezi zinazoonyesha kuwa bei ya petroli na dizeli zitashuka kidogo, kiwango ambacho angalau kitapunguza watumiaji kutoboa zaidi mifuko yao.
“Ikilinganishwa na bei za mwezi Desemba 2021, bei za Januari 2022 zitapungua kwa kati ya Shilingi 4 na 35 kwa lita ya petroli na kati ya Shilingi 43 na 67 kwa lita ya dizeli isipokuwa kwa bandari ya Mtwara ambapo bei zitaongezeka kwa Shilingi 2 kwa lita,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje.
Soma zaidi
- Ahueni: Rais Samia aagiza tozo za mafuta kupunguzwa Tanzania
- Ahueni, maumivu: Bei mpya za petroli, dizeli Tanzania
Kwa bei hizo mpya, wakazi wa Dar es Salaam sasa watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,501 kutoka Sh2,510 ya awali wakati wale wa Mtwara watanunua kwa Sh2,521 huku wa Mtwara wakinunua kwa Sh2,534.
Ewura inaeleza kuwa bei kikomo kwa Dizeli Januari 2022 itakuwa Sh2,425 kwa lita mkoani Mtwara, Tanga (Sh2,369) na kwa Dar es Salaam itauzwa kwa Sh2,325.
Bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia zimekuwa zikipanda tangu mwaka jana jambo ambalo limeendelea kupandisha pia bei za bidhaa hizo Tanzania.
Serikali yachangia kushuka kwa bei
Oktoba 2021 Serikali ilifuta baadhi ya tozo zilizokuwa zikitozwa kwenye mafuta kwa lengo la kupunguza maumivu kwenye bei ya mafuta kwa kati ya Sh23 na Sh31 kwa lita kulingana na aina ya mafuta na bandari yaliyopokelewa.
“Serikali iliahirisha ukusanyaji wa ada ya mafuta kuanzia Disemba 2021 na hivyo kufanya bei ya juu kufikiwa katika mwaka 2021 kuwa ni Sh2,510 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam, Sh2,525 Tanga na Sh 2,569 Mtwara,” amesema Chibulunje.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa Ewura, endapo maamuzi hayo yasingefanywa na Serikali, petroli ingeuzwa kwa Sh2,638 kwa lita moja jijini Dar es Salaam , Tanga (Sh2,648) na Sh2,693 mkoani Mtwara.
Latest
