Ahueni, maumivu: Bei mpya za petroli, dizeli Tanzania
Mabadiliko ya bei za mafuta yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji. Picha| NewsIndia24Live.
- Bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa asilimia 1.67.
- Bei za rejareja za dizeli zimeongezeka kwa Sh9 kwa lita na mafuta ya taa kwa Sh29 kwa lita.
- Ahueni na maumivu hayo yamejitokeza katika mikoa mingine.
Dar es Salaam. Wakati mwezi Januari ukitajwa kuwa mgumu kwa wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule mbalimbali Tanzania, baadhi ya watumiaji wa petroli kuendesha vyombo vya moto watapata ahueni baada ya bei ya nishati hiyo kushuka.
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Januari 2021 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa asilimia 1.67.
Kutokana na kushuka la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto wataokoa Sh31 kwa kila lita moja ikilinganishwa na bei ambayo walikuwa wananunulia Desemba 2020.
Wakazi wa jiji hilo, watanunua petroli kwa Sh1,834.
Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita wa Desemba 2020, bei ya jumla ya petroli imepungua kwa Sh31.1 kwa lita sawa na asilimia 1.79.
Hata wakati, bei ya petroli ikishuka, bei ya rejareja ya dizeli imeongezeka kwa Sh9 kwa lita na mafuta ya taa kwa Sh29 sawa na asilimia 1.8.
Hiyo ni sawa kusema, bei kikomo ya dizeli jijini humo ni Sh1,695 kwa lita na mafuta ya taa ni Sh1,650.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Kapwete John katika taarifa yake iliyotolewa Januari 5, 2020 amesema mabadiliko haya yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji.
Soma zaidi:
Ahueni, maumivu yafika mikoa mingine Tanzania
Kwa Januari 2021, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) inayotumia Bandari ya Tanga zimebadilika ikilinganishwa na bei zilizotolewa Desemba 2, 2020.
Bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh31 kwa lita na Sh61 mtawalia.
“Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe Desemba 2, 2020. Hii ni kwa sababu, kwa Desemba 2020 hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia Bandari ya Tanga,” amesema John.
Kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia Bandari ya Mtwara (mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma), bei ya rejareja ya petroli imepungua kwa Sh2 kwa lita, wakati bei ya dizeli imeongezeka kwa Sh20 kwa lita sawa na asilimia 1.15.
EWURA inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo.