Mercedes yaja na mpango wa gari la umeme lenye betri la kilometa 1,000

January 5, 2022 2:32 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Umbali wa kusafiri gari hiyo ni sawa na safari ya kwenda Lindi kutoka Dar es Salaam na kurudi.
  • Itaambatana na teknolojia ya umeme jua.
  • Licha ya majaribio kufanyika, bado gari hii ni dhana isiyo na muundo wa kufaa kuingia sokoni.

Dar es Salaam. Riadha ya kampuni za kutengeneza magari ya umeme yanayolenga kupunguza au kuachana kabisa na matumizi ya mafuta imezidi kupamba moto duniani.

Mwaka 2021 Subaru na Toyota walitangaza kuwa wanatarajia kuingiza magari ya umeme mwaka huu jambo litakaloongeza ushindani na kampuni nyingine mashuhuri ulimwenguni yanayozalisha magari ya aina hiyo ikiwemo Tesla. 

Baada ya kampuni hizo kutangaza hayo, wiki ya kwanza tu ya mwaka 2022, kampuni ya magari ya Ujerumani ya Mercedes Benz nayo imeweka wazi mipango yake ya kuingia kwenye riadha hiyo ya kutengeneza magari ya umeme.

Kampuni hiyo imetangaza dhana (concept) ya gari lake la kutumia umeme ambalo linatazamiwa kusafiri umbali wa hadi kilomita 1,000 kabla ya betri kuisha chaji. 

Hiyo ni sawa na kusema endapo betri ya gari hilo litachajiwa vema na kujaa, mtumiaji anaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Lindi (kilometa 459) na kurudi Dar es Salaam na bado akabakiwa na kiwango kidogo cha chaji ya kuzungukia mjini. 

Iwapo dhana hiyo itawekwa katika vitendo, gari hilo litakuwa ni zaidi ya baadhi ya magari ya umeme yaliyopo sokoni kwa sasa ikiwemo Lucid Air (maili 520) na Tesla S Long Range Plus inayotembea umbali wa maili 402 sawa na kilomita 647.  

Hata hivyo, tofauti na magari hayo, gari la Mercedes Benz lilopewa jina la Vision EQXX bado ni dhana tu huku mengine yakiwa barabarani tayari.

Paa la gari hiyo limenakshiwa kwa teknolojia ya “Solar panel” kwa ajili ya kufua umeme. Picha| Mercedes Benz.

Nini kipya kwa Vision EQXX

Kampuni ya Mercedes imeshafanya majaribio kwa wiki kadhaa hadi sasa. Hivi karibuni, gari hilo lilitambulishwa kwa wadau wa Mercedes kwa njia ya mtandao na muonekano wake ni “sporty” yaani kama zilivyo gari za Porsche na Tesla.

Matumizi ya umeme kwa Vision EQXX yameainishwa na Mercedes kuwa yanayozingatia hali ya nishati na foleni.

Gari hilo linatarajiwa kutumia umeme hadi “kilowatt (kWh)” 10 kwa kilometa 100 ambayo watalaamu wanaeleza kuwa ikiletwa kwa uhalisia wa matumizi ya mafuta ni sawa na kusema lita moja itoshe kuliwezesha gari kusafiri kilometa 100.

Mercedes imesema itafikia malengo hayo kwa kuzingatia ubunifu na sayansi kuja na gari lenye muundo mzuri.

Vision EQXX haitochajiwa tu na umeme bali Mercedes imeshirikiana na taasisi ya utafiti wa umeme jua ya Ulaya kunakshi paa la gari hiyo kwa teknolojia ya kufua umeme jua kwa ajili ya kuzalisha chaji. 

Kwa mujibu wa Mercedes, ‘solar panel’ ya gari hilo iinaweza kufua umeme unaotosha kutumika kwa kilomita 25 kwa siku.

Mercedes sio wa kwanza kutumia teknolojia hiyo kwa kuwa zipo kampuni zinazotengeneza magari ya kutumia umeme jua tu ikiwemo startup ya Kijerumani, Sono Motors.

Hata hivyo, wataalamu wa teknolojia kutoka Shirika la habari la The Verge wamesema, huenda Mercedes hawajazingatia baadhi ya changamoto za usafiri wa gari katika makadirio yao ikiwemo kupanda mlima na baridi ambavyo hupunguza uwezo wa betri. 


Soma zaidi


Sukari kwenye chai

Pamoja na mbwembwe hizo, muundo mzuri haupatikani kwenye Vision EQXX pekee, tumeuona pia kwa Toyota na Subaru. 

Hata hivyo, kujitofautisha Vision itaambatana na skrini ya inchi 47.5 ndani ya gari yenye uwezo wa kuonyesha picha kwa ubora wa juu zaidi ya kiwango cha 4K.

Swali linabaki kuwa Mercedes watatoboa katika kuibadili dhana hii kuwa uhalisia kama Tesla, Toyota na Subaru walivyoweza? Mimi na wewe hatujui lakini maadamu siyo gari la kwanza la umeme, huenda kukawepo asilimia kubwa ya kufanikiwa.

Endelea kusoma Nukta Habari na kusubscribe kwenye chaneli ya YouTube  ya Nukta TV. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW