Mwaka 2021 watajwa miongoni mwa miaka 7 yenye joto zaidi duniani
Kuongezeka kwa joto duniani kuna athari mbalimbali ikiwemo kusababisha mafuriko na ukame. Picha| Shutterstock.
- Wastani wa halijoto duniani mwaka 2021 ilikuwa takriban nyuzi joto 1.11 °C.
- Ongezeko la joto limetokana na ongezeko la gesi chafuzi.
Dar es Salaam. Shirika la Hali ya Hewa duniani (WMO) limetoa ripoti ya hali ya hewa ya mwaka 2021 na kueleza kuwa mwaka huo ulikuwa moja kati ya miaka saba yenye joto zaidi duniani katika rekodi zake.
Ripoti hiyo ya WMO imetolewa baada ya shirika hilo kupitia kwa kina takwimu za mamlaka sita za kimataifa zinazofanya tathmini ya hali ya joto na kuonyesha kuwa wastani wa halijoto duniani mwaka 2021 ilikuwa takriban nyuzi joto 1.11 °C katika kipimo cha Selsiasi.
Mwaka 2021 ni wa saba mfululizo (2015-2021) ambapo halijoto duniani imekuwa zaidi ya nyuzi joto 1°C katika kipimo cha Selsiasi kulingana na takwimu zote za mamlaka hizo za kimataifa zilizokusanywa na WMO.
“Matukio yanayofuatana ya La Niña yanamaanisha kuwa ongezeko la joto la 2021 lilikuwa kidogo sana ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni,” amesema Katibu Mkuu wa WMO Profesa Petteri Taalas.
Ongezeko la joto kwa ujumla limetokana na ongezeko la gesi chafuzi ambayo sasa ni kubwa ikilinganishwa na vichochezi vya hali ya hewa vinavyotokea kiasili.
“Mwaka 2021 utakumbukwa kwa halijoto iliyovunja rekodi ya karibu nyuzi joto 50°C nchini Canada, mvua ya kipekee, mafuriko mabaya huko Asia na Ulaya na vile vile ukame katika baadhi ya maeneo barani Afrika na Amerika Kusini.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazohusiana na hali ya hewa zimeleta athari mbaya kwa jamii katika kila bara moja,” amesema Prof Taalas
Katika miaka saba iliyopita, miaka ambayo imekuwa na joto zaidi ni mwaka 2016, 2019 na 2020.
Soma Zaidi:
Ongezeko la joto duniani ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu kama vile viwanda na ukataji miti hovyo, hivyo kuongezeka kwa gesi chafuzi zinazokusanyika katika angahewa na kuruhusu miale ya jua kupiga moja kwa moja katika uso wa nchi.
Ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti ongezeko la joto, huenda kukakawa na uwezekano wa visa vya matukio mabaya ya hali ya hewa ikiwemo kuyeyuka na kupungua kwa barafu.
Pia kuwepo kwa vipindi vya mvua zisizotabirika ambazo zinaweza kuleta ukame wa muda mrefu ama mafuriko na kugharimu maisha ya watu na mimea.
Umoja wa Mataifa (UN) umekuwa ukiitisha mkutano ni takribani miongo miwili sasa kwa nchi zote washirika kwa lengo la kuleta pamoja na kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2021 mkutano huo ulifanyika Oktoba 31, 2021 Glasgow nchini Scottland ukiwakusanya zaidi ya viongozi na wakuu wa nchi 200, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kujadili suluhu za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuhimiza upandaji wa miti.