Walichopoteza watoto wakati wa Uviko-19 ni vigumu kurekebishika: UNICEF
- Hatua zisipochukuliwa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika itaongezeka.
- Suluhu ni kurekebisha mifumo ya elimu.
Dar Es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) limesema kiwango cha hasara wanayopata watoto kielimu kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa elimu kulikosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona ni vigumu kurekebishika.
UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa Januari 23, 2022 jijini New York, Marekani imesema kuvurugika kwa mfumo wa utoaji elimu iwe kwa shule kufungwa kabisa au mchanganyiko wa kusomea nyumbani na mtandaoni kumeathiri zaidi ya watoto milioni 635 duniani kote.
Ikiwa ni takribani miaka miwili tangu kuanza kwa janga la Uviki-19, UNICEF inatoa takwimu hizo hii leo siku ya elimu duniani ambapo mkuu wa masuala ya elimu UNICEF, Robert Jenkins anasema
“Wakati tunataka kukoma kwa kuvurugwa kwa mfumo wa elimu, kufunguliwa shule pekee hakutoshi. Wanafunzi wanahitaji msaada wa kina ili kufidia kile walichopoteza. Shule lazima ziwe zaidi ya eneo la kujifunza ili kujenga tena afya ya mwili na akili ya mtoto sambamba na maendeleo yake kijamii na kilishe,” amesema Jenkins
Duniani kote, watoto wamepoteza stadi zao za kuhesabu na kusoma ikimaanisha kuwa mamilioni ya watoto wamekosa mihula yao ya shule ambayo wangetimiza iwapo wangekuwa darasani, huku watoto wadogo na walio pembezeni wakipata hasara kubwa zaidi.
Watoto wakipata mlo wa asubuhi shuleni huko nchini Msumbiji. Picha|UNICEF
Takwimu zinasemaje?
Katika Nchi zenye kipato cha chini na kati, kufungwa kwa shule kumesababisha asilimia 70 ya watoto wenye umri wa miaka 10 washindwe kusoma au kuelewa aya rahisi na kiwango hicho ni ongezeko kutoka asilimia 53 kabla ya Uviko-19.
Nchini Ethiopia, wanafunzi wa shule za msingi wanakadiriwa kuwa wangekuwa wamejifunza kati ya asilimia 30 hadi 40 ya hesabu ambazo wangeijifunza iwapo muhula wa shule ungekuwa wa kawaida.
Huko Afrika Kusini, wanafunzi wako nyuma ya muhula wa shule kwa asilimia 75 au muhula mzima ambao walitakiwa kuwa wamesoma.
UNICEF imesema kati ya mwezi Machi mwaka 2020 na Julai mwaka 2021 watoto wapatao 400,000 hadi 500,000 waliacha shule.
UNICEF imesema pamoja na kupoteza muhula wa masomo, kufungwa kwa shule pia kumeathiri afya ya akili ya watoto, na kupunguza fursa ya kupata lishe bora sambamba na kukumbwa na ukatili.
“Watoto wamekumbwa na viwewe na tafiti zinaonesha wasichana na barubaru walioko vijijini wako hatarini zaidi kupata shida hizo. Zaidi ya watoto milioni 370 walikosa mlo shuleni, ikimaanisha walipoteza chanzo cha mlo bora na wa uhakika,” imesema UNICEF.
Soma Zaidi:
- Unavyoweza kuzungumza na watoto kuhusu Corona
- Madhara ya corona: UNICEF yaangazia namna ya kuwarudisha wanafunzi shuleni
Nini kifanyike?
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema janga la Uviko-19 na changamoto nyingine zinaizokabili Dunia hivi sasa zimedhihirisha umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa.
“Dunia yetu inabadilika kwa kasi ya haraka mno, ubunifu katika teknolojia, mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye dunia ya ajira, dharura ya mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa ukosefu wa imani baina ya watu na taasisi,” amesema Guterres.
Ameonya kuwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa basi huenda idadi ya wasiojua kusoma na kuandika ikaongezeka kwa asilimia 53 hadi asilimia 70 na kutoa mapendekezo kuwa elimu ni zaidi ya hoja ya usawa.
“Elimu ni bidhaa ya umma na ni jambo muhimu linalohitajika kufanikisha ajenda nzima ya 2030 kwa maendeleo endelevu. Jamii ya kimataifa haiwezi kukubali kutokuwa na uhakika katika utoaji wa elimu, tena bora na inayoendana na wakati,” amesema Guterres na kubainisha kuwa,
“Muda umefika kuchochea upya azma yetu ya pamoja kwa elimu. Hii ina maana kuwekeza katika mipango thabiti ya kusaidia wanafunzi kupata mafunzo ambayo walipoteza.”
Latest
