Fedha za Uviko-19: Rais Samia atumbua wakurugenzi wanne
- Ni Wakurugenzi wanne wa halmashauri za Buchosa, Jiji la Mbeya, Manispaa ya Iringa na Singida.
- Mkurugenzi wa Geita Vijijini awekwa kiporo.
- Wanatuhumiwa kwa kuchezea fedha za Uviko-19.
Dar es Salaam. Huenda siku ya leo ikawa mbaya kwa Wakurugenzi wanne wa halmashauri za Buchosa, Jiji la Mbeya, Manispaa ya Iringa na Singida baada ya teuzi zao kutenguliwa kutokana matumizi mabaya ya fedha za Corona (Uviko-19) zilizotolewa na Serikali kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo shule.
Utenguzi huo umetangazwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa wilayani Magu mkoani Mwanza wakati akiwa safarini kuelekea Mkoa wa Mara katika maadhimisho ya miaka 45 ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Samia amesema kwa taarifa zilizopo katika halmashauri hizo nne, wakurugenzi wake wametumia fedha kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
“Siku ile tunazitangaza fedha nilisema kama mkurugenzi anataka kuona rangi yangu halisi achezee hizo fedha, sasa kwa taarifa zilizopo, Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini, wakurugenzi wamechezea fedha. Mheshimiwa waziri (Waziri wa Tamisemi) wakurugenzi hao nimewatengua sasa hivi,” amesema Rais Samia.
Wakurugenzi waliotenguliwa ni Paul Malaga wa Buchosa, Amede Ng’wanidako (Jiji la Mbeya), Bernard Limbe (Manispaa ya Iringa) na Zefrin Lubuva wa Manispaa ya Singida huku aliyekalia kuti kavu ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita Vijijini, John Wanga.
Aidha, amemuagiza Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa kuwasilisha ripoti za wakurugenzi hao huku akiahidi kuendelea kumchunguza Wanga anayelalamikiwa na Mbunge wa jimbo hilo Joseph Msukuma kukiuka utaratibu wa manunuzi kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa fedha hizo.
“Yule wa Geita endeleeni na uchunguzi na mimi timu yangu iko pale inafanya uchunguzi naye wakiniletea na makosa kama haya na yeye atatenguliwa,” amesema Rais.
Soma zaidi:
- Rais Samia ateua mawaziri wapya wanne, atengua watatu
- Ni panga, pangua: Rais Samia afumua baraza la mawaziri Tanzania
Septemba 2021, Shirika la Fedha Duniani (IMF) liliidhinisha kuipatia Tanzania mkopo wa dharura wa Dola za Marekani milioni 567.25 (Sh1.3 trilioni) kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa Corona (Uviko-19).
Baada ya Tanzania kupokea pesa hizo ambazo zinatakiwa kutumiwa kwa muda wa miezi tisa, ilizisambaza katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, afya na maji ili kuwapunguzia wananchi maumivu ya Uviko-19.
Wakati Rais Samia akizindua Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Corona kwa kutumia fedha hizo jijini Dodoma Oktoba 10, 2021 aliwaonya watendaji wa Serikali kutochezea fedha hizo na wazitumie vizuri kwa matokeo yaliyokusudiwa.
Awali akitoa taarifa kwa Rais, Waziri Bashungwa amesema wakurugenzi hao wamehusika na ubadhilifu wa fedha ambapo kwa jiji la Mbeya walibaini kushuka kwa mapato na baada ya uchunguzi walibaini kuzimwa kwa mashine za mapato kwa zaidi ya siku 100 ili kuficha upotevu wa fedha.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amesema, walipokea fedha za kujenga vyumba vya madarasa pamoja na vyumba 32 vya shule shikizi ambapo kazi ilifanyika lakini kuna watu waliiba fedha.
Amesema hawakupiga kelele baada ya jambo hilo hivyo kuna watu walikamatwa na wengine wapo ndani katika Halmashauri ya Buchosa lakini katika ujenzi wa vyumba vya madarasa fedha iliyobaki ni zaidi ya millioni 600.
Habari hii imeandikwa na Mariam John.
Latest