Mbowe na wenzake watatu wakutwa na kesi ya kujibu
- Uamuzi huo umetolewa leo Februari 18, 2022 jijini Dar es Salaam na Jaji Joachim Tiganga.
- Wana kesi ya kujibu katika mashtaka matano kati ya sita.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Division ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemkuta na kesi ya kujibu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu katika tuha za ugaidi zinazowakabili.
Mbowe na wenzake watatu ambao ni Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire, Adam Kasekwa wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi.
Mashtaka mengine ni kushiriki kikao cha kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria.
Katika kesi hiyo, Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa la ugaidi kati ya Mei na Agosti mwaka 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.
Leo Ijumaa Februari 18, 2022 Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo namba 217 Â ya mwaka 202o, amesema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 13 wa Jamhuri na vielelezo, mahakama imeona washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu.
Akitoa uamuzi huo mdogo, Jaji Tiganga amesema baada ya mahakama kupitia vielelezo hivyo na mashahidi vilivyotolewa kuthibitisha makosa yanayowakabili na baada ya kujiridhisha imeona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu katika shtaka la kwanza hadi la tano.
Katika shtaka la sita, mahakama imesema hawana kesi ya kujibu kwa sababu hakukuwa na vielelezo vya kutosha kuthibitisha tuhuma hizo.
Uamuzi huo wa uliokuja siku 202 tangu kesi hiyo ianze, umefungua milango kwa watuhumiwa hao kuanza kujitetea kwa nyakati tofauti kama itakavyoamriwa na mahakama.
Soma zaidi:
-
Jaji Siyani ajitoa kesi ya Mbowe na wenzake, atoa maelekezo
-
Polisi wasema Mbowe anahojiwa Dar es Salaam kwa makosa ya jinai
Baada ya uamuzi huo mdogo, Wakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya akasimama na kueleza kuwa mshtakiwa wa kwanza, Bwire, kwa shtaka pili na la nne atakuwa na mashahidi watano pamoja na yeye ni wa sita na atatoa vielelezo vitano katika ushahidi wake.
Pia akasimama Wakili mwingine wa utetezi John Mallya kwa niaba ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa anayekabiliwa na kosa la kwanza, pili, nne na la tano ambalo anashtakiwa pekee yake, amesema anakusudia kujitetea mwenyewe, ataleta mashahidi wawili na kuleta vielelezo vinne katika utetezi wake.
Wakili Fredrick Kihwelo anayemtetea mshtakiwa wa tatu (Ligw’enya) amesimama na kusema mteja wake atajitetea mwenyewe chini ya kiapo huku akiwa na mashahidi watano na vielelezo vitano.
Mbowe ambaye anayetetewa Wakili Peter Kibatala ataleta mashahidi 10 pamoja na yeye watakuwa 11 na anategemea kutumia vielelezo 20.
Hakimu Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 4, 2022 ambapo watuhumiwa hao wataanza kujitetea.
Uamuzi uliofanywa leo na Jaji Tiganga umekuja baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha kuwasilisha ushahidi wake wiki hii kupitia mashahidi wake 13 kati ya 24 waliotarajiwa kutoa ushahidi mahakamani.Â
Upande wa Mashtaka umeongozwa na mawakili Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Ignasi Mwinuka, na Wakili wa Serikali Tulimanywa Majige.
Mwenyekiti huyo wa Chadema na wenzake wanatetewa na mawakili 19 wakiongozwa Wakili Peter Kibatala.Â
Tangu kesi hiyo ianze, imesikilizwa na majaji watatu: Elinaza Luvanda, Mustapher Siyani na Joachim Tiganga.
Mbowe alikamatwa pamoja na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 siku akijiandaa kufanya kongamano la kudai katiba mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam.Â
Latest