Simulizi ya mwanamke aliyejifungua katikati ya mashambulizi Ukraine

March 9, 2022 12:56 pm · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchungu ulimshika siku ya kwanza ya mashambulizi.
  • Ajifungua wakati akisikia king’ora cha mashambulizi.
  • Ashuhudia kombora lililopigwa karibu na jengo alilokuwepo.

Dar es Salaam. Maria Shostak (25), anayeishi katika Mji Mkuu wa Ukraine, Kyiv anasimulia magumu na machungu aliyopitia wakati akileta maisha mapya katika kipindi ambacho nchi yao ipo katika sintofahamu.

Maria anasema kuwa alianza kusikia uchungu Februari 24 mwaka huu, siku ambayo Urusi ilianza mashambulizi ya kijeshi nchini Ukraine.

‘’Nilipoamka tarehe 24 Februari, skrini ya simu yangu ilikuwa imejaa ujumbe kutoka kwa ndugu na jamaa. Hata kabla ya kusoma, niligundua kuwa kuna kitu kilikuwa kimetokea,” anasema Maria

Kwa mujibu wa Kituo cha mawasiliano cha Umoja wa Mataifa (UN), alipelekwa hospitali n asubuhi ya siku hiyo hiyo alipata uchungu ulioanza kidogo kidogo na alasiri, walihamishwa kutoka Wodi ya  juu hadi kwenye mahandaki chini ya ardhi ikiwa ni mara ya kwanza kwake hali iliyomtisha na kumfanya asilale usiku.

Uchungu uliongezeka kwa kasi na taarifa za machafuko zilizidisha adha. Mapema asubuhi ya Februari 25, daktari alimchunguza na kumwambia kuwa angejifungua siku hiyo, hivyo alimpigia simu mume wake ili aende hospitalini hapo.

Safari ambayo kwa kawaida huchukua dakika 20, siku hiyo ilichukua karibu saa nne hadi mume wake kufika kwa sababu ya foleni kwenye kituo cha mafuta, maduka ya chakula na maduka ya dawa.

Yuril ambaye ni mume wa Shostak akiwa amembeba mtoto wao mchanga hospitalini. Mpango wao ni kuendelea kuishi kwenye handaki nyumbani mwao. Picha| Mariia Shostak/UNFPA.

Maria anasema kuwa alikuwa na bahati wakati wa kujifungua, kwani hakujifungulia kwenye handaki kama baadhi ya wanawake wengine. 

‘’Nilianza katika chumba cha kujifungulia lakini ilibidi nihamishiwe hadi kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili ya kupasuliwa. Baadaye, ving’ora vya mashambulizi ya anga vilipolia, wafanyakazi wa hospital na wauguzi walitaka kunitoa na kunipeleka kwenye handaki lakini nilikataa,” anasema.

‘’Kwa sababu ya maumivu, sikuweza hata kuongea, achilia mbali kutembea popote. Wakati wote niliokuwa hapo nilitengwa na ulimwengu wa nje, ambapo labda ndiyo wakati pekee nilisahau kuhusu vita,” anasimulia Maria wakati akizungumza na kituo cha mawasiliano cha UN.

Hofu, uchovu na maumivu

Baada ya upasuaji, Maria anasema kuwa aliwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa saa kadhaa, na hakuwa tena na ganzi.

Wasiwasi ulimshika kwani hakujua mtoto na mume wake wako wapi.

“Wakati huo huo, king’ora kingine cha mashambulizi ya anga kilisikika, na niliamua kushuka kwenye handaki. Nilikuwa nimevaa gauni la hospitali, bila viatu, kwenye kiti mwendo, nikiwa na katheta ya mkojo,” anasema.


Soma zaidi:


Maria anasimulia kuwa alifunikwa na blanketi na kupelekwa kwenye makazi ya dharura, ambapo kwa mara ya kwanza alimuona mwanae ambaye walimuita Arthur.

“Niliweza kulala kwa saa moja au mbili kwa siku. Muda mwingi tulikuwa kwenye handaki tukiwa tumekaa kwenye viti. Mgongo wangu uliuma kwa kukaa, na miguu yangu bado ilikuwa imevimba kama wakati wa shida ya ujauzito,” anasema Maria.

Mama Arthur anaongeza kuwa uchovu aliokuwa nao ulipunguza woga hadi pale kombora lilipogonga jengo la ghorofa karibu yao waliloweza kuliona kwenye dirisha.

Maria anasema anahisi yuko salama katika mji mkuu wa Kyiv, kwani kuna makazi ya kutosha na wanapata habari kwa wakati kutoka kwa mamlaka na kuwa mume wake aliwapangia kona maalum katika ghorofa ya chini ya nyumba yao ili wakae.

“Nilizaliwa na kukulia hapa Kyiv, sina sehemu nyingine ninayoweza kuiita nyumbani. Hatutaondoka,” anasisitiza Maria.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW