Umaskini unavyowatesa watoto duniani

March 15, 2022 8:30 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

                   


  • Takriban watoto bilioni 1 duniani wanaishi katika umaskini wa kukosa mahitaji yao muhimu.
  • Watoto  milioni 150 waongezeka katika kundi hilo kutokana na Uviko-19.
  • Watoto hao wapo hatarini kupoteza maisha na kuwa na maisha duni ukubwani.

Dar es salaam. Umaskini wa mtoto  bado ni changamoto kubwa duniani licha ya uwepo wa harakati za kutokomeza umaskini katika mataifa mbalimbali.

Hali hiyo inayomfanya mtoto kuishi katika mazingira duni, husababisha mtoto kukosa mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, malazi, huduma za afya na elimu.

Shirika la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) limesema kuwa takriban watoto bilioni 1 duniani wanaishi katika umaskini wa kukosa mahitaji yao muhimu, huku watoto milioni 150 wakiongezeka katika kundi hilo kutokana na Uviko-19.

Japo kuna watoto ambao wanapata mahitaji hayo, bado wanawekwa katika kundi hili kutokana na kiwango cha mahitaji wanayopata kuwa duni, ikiwemo kula chakula kisicho na lishe bora, na kutumia maji yasiyo safi na salama.

Takriban  asilimia 88 ya watoto wanakosa zaidi ya mahitaji matatu muhimu, huku zaidi ya nusu  wakikosa mahitaji hayo zaidi ya matano. Picha| Nukta Habari.

Watoto wengine wanaishi katika umaskini uliokithiri katika nyanja zote kwa kukosa mahitaji matatu au zaidi ya lishe, ulinzi, elimu, kupata na kutoa taarifa, maji, makazi, afya, na mazingira safi.

Kwa Tanzania, takriban  asilimia 88 ya watoto wanakosa zaidi ya mahitaji matatu muhimu, huku zaidi ya nusu  wakikosa mahitaji hayo zaidi ya matano, kwa mujibu wa Ripoti ya umaskini wa mtoto Tanzania  ya mwaka 2019 iliyotolewa na UNICEF pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). 

Hali hiyo inaweweka watoto hawa hatarini mara mbili zaidi kupoteza maisha wakiwa watoto ikilinganishwa na watoto ambao si maskini.


Zinazohusiana:


UNICEF inaeleza kuwa licha ya watoto kuwa theluthi moja ya idadi yote ya watu duniani, kundi hilo linachukua nusu ya watu wanaotumia chini ya dola 1.9 kwa siku  sawa na shilingi za Kitanzania 4,300, huku  watoto milioni 365 wakiishi katika umaskini uliopindukia.

Shirika hilo linaongeza kuwa watoto wanaokuwa katika umaskini huteseka ukubwani  kwa kuwa na maisha duni, ujuzi kidogo wa kazi, na kufanya kazi za mishahara ya chini.

Jambo linalohuzunisha zaidi ni kuwa, licha ya hali hiyo, ni mataifa machache ndiyo yameweka mkazo kutokomeza umaskini kwa watoto kama kipaumbele cha Taifa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW