Ajira kwa watoto bado tishio Afrika
- Mtoto mmoja kati ya wanne anatumikishwa katika ajira za utotoni katika nchi zinazoendelea.
- Ajira kwa watoto huwatoa kwenye elimu na afya bora.
Dar es Salaam, Janga la ajira za watoto huenda likaendelea kuathiri nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania kutokana na kuongezeka kwa ajira hizo kila mwaka na kuathiri maisha ya kundi hilo muhimu kwenye jamii.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, (ILO) katika ripoti ya kupinga ajira za watoto iliyotolewa Mei, 2022 inasema ajira kwa watoto Afrika zimefikia milioni 72.
Ripoti hiyo inasema janga hili la ajira kwa watoto, huzikumba nchi zinazoendelea zaidi kuliko na nchi zilizoendelea.
Katika nchi zinazoendelea, zaidi ya mtoto mmoja kati ya wanne wenye umri wa kati ya miaka mitano na 17 ni waathirika wa utumikishwaji wa watoto, ambao unachukuliwa kuwa hatari kwa afya na maendeleo yao.
Sababu za kuongezeka ajira za watoto
ILO imesema jitihada zilizofanyika kwa miaka 10 iliyopita zimefanikiwa kupunguza ajira kwa watoto kwa asilimia 6.4 duniani kote, lakini janga la Uviko-19, limeibua ongezeko jipya na kufikia watoto milioni 160 wanaofanya ajira kwenye umri mdogo.
Mbali na Uviko-19, sababu nyingine ya ajira kwa watoto ni kukosekana kwa ulinzi wa kutosha ambapo ILO inaeleza kuwa karibu robo tatu ya watoto, au watoto bilioni 1.5 duniani, hawana usaidizi wowote wa kijamii.
Umaskini pia ni sababu inayowaingiza watoto wengi kwenye ajira hizi, zinazowanyima haki yao ya kusoma na wakati mwingine kuhatarisha afya zao.
Zinazohusiana:
ILO imesema mwaka 2020, jumla ya watu bilioni 4.1, hawakuwa na usaidizi au ufadhili wa kifedha kutoka katika Serikali zao, hali iliyo watoto wengi kujiingiza katika ajira ili wajipatie fedha za kujikimu.
Ripoti ya ILO imesema kukosekana kwa elimu kwa watoto kunachangia pia kuongezeka kwa ajira za utotoni, pale mzazi anaposhindwa kumpeleka mtoto shule mara nyingi mtoto hujikuta akijiingiza katika ajira hizi.
Kadri idadi ya watoto duniani inavyoongezeka ndivyo kunakuwa na uwezekano wa kuongezeka kwa ajira za watoto.
ILO imesema katika nchi za kusini mwa Afrika, idadi ya ajira kwa watoto kutoka mwaka 2018 mpaka 2020 iliongezeka kufikia milioni 21 sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watoto milioni 104.
Hatua za kuchukua kupambana na ajira za utotoni
Katika Siku ya Kimataifa dhidi ya Ajira kwa Watoto iliyoyoadhimishwa Juni 12, Umoja wa Mataifa (UN) na wadau wake wanawekeza zaidi katika ulinzi wa kijamii na mifumo inayowalinda watoto dhidi ya vitendo hivyo.
Kuzingatia ulinzi wa kijamii kwani ni haki ya binadamu na sera yenye nguvu ya kuzuia familia kutoajiri watoto wakati wa shida.
Kwa mujibu wa UN, mifumo ya ulinzi wa kijamii inayotolewa na serikali za ulimwengu ni muhimu katika kupambana na umaskini kwa kutokomeza na kuzuia utumikishwaji wa watoto.
Latest