Umaskini unavyohatarisha maisha ya watoto Tanzania

May 10, 2022 8:08 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

                       


  • Asilimia 88 ya watoto Tanzania wanakosa zaidi ya mahitaji muhimu matatu.
  • Asilimia 19  ya watoto bado wanaishi katika familia ambazo zipo chini ya mstari wa kitaifa wa umaskini.

Dar es Salaam. Ripoti ya umaskini wa mtoto Tanzania iliyotolewa na Shirika la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2019 inaonesha kuwa watoto wengi Tanzania wanaishi katika umaskini wa kukosa mahitaji muhimu, jambo linaloathiri ustawi wao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 88 ya watoto Tanzania wanakosa zaidi ya mahitaji muhimu matatu, huku nusu wakikosa zaidi ya mahitaji matano.

Hali mbaya ikiwa ni kwenye makazi na usafi wa mazingira, ambapo takriban asilimia 90 ya watoto wanakosa mahitaji hayo muhimu.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa watoto tisa kati ya 10  wanaishi katika mazingira machafu ikiwemo sehemu za dampo na kutumia vyoo ambavyo ni duni na vinavyotumiwa na watu wengi. 

Kwa upande wa makazi asilimia 88 ya watoto wanaishi katika makazi duni ikiwa ni  pamoja na kuishi katika nyumba zilizoezekwa kwa nyasi, makazi yenye mlundikano wa watu pamoja na nyumba zinazotumia nishati isiyo safi kama kuni na mkaa.


Soma zaidi:


Vilevile  asilimia 86.4  ya watoto wanakosa hitaji muhimu la kulindwa kutokana na kuolewa katika umri mdogo, kuishi katika familia zenye kesi za wizi na ukabaji na kufanya ngumu ambazo ziko nje ya uwezo wao.

Mahitaji mengine ambayo watoto wanakosa ni  maji kwa asilimia 72.3, afya (asilimia 54.7), kupata taarifa (asilimia 39.4), elimu (asilimia 36.1) na Lishe kwa asilimia 30.1.

Licha ya umaskini wa mahitaji kwa watoto kupungua katika kipindi cha mwaka 2012/13 na 2014/2015 kwa asilimia 9.3, hasa katika kundi la watoto wenye umri wa miezi 0-23, ripoti hiyo inaonesha kuwa asilimia 19  ya watoto bado wanaishi katika familia ambazo zipo chini ya mstari wa kitaifa wa umaskini.

Ripoti hiyo inachanganua kuwa asilimia 0.5 ya watoto wanaishi kwenye umaskini wa kifedha pekee. Hii inamaanisha kuwa watoto hao wanapata mahitaji muhimu licha ya kuwa wanatoka katika familia zinazohaha kujipatia kipato.

 Watoto wanaokumbana na umaskini wa kimahitaji pekee ni  asilimia 69, wakati  watoto 19 kati ya 100 wakiwa katika hali mbaya kwa sababu wanakabiliwa na umaskini wa nyanja zote yaani kifedha na kimahitaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo watoto wengi wanaoishi katika umaskini uliopindukia ni wale ambao wazazi wao wana elimu chini ya elimu ya sekondari pamoja na wale ambao mama zao wapo chini ya umri wa miaka 18.

Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kuwa juhudi kubwa zinahitajika kufanyika ili  kupunguza makali ya umaskini kwa watoto, kwani ni asilimia 12 pekee ya watoto nchini ndiyo hawapo katika hali ya umaskini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW