Kupanda bei za vyakula, CPB waja na suluhu
- Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) yajikiza kuzalisha chakula.
- Kukiuza kwa bei rahisi wakati wa mfungo wa Ramadhan.
Mwanza. Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) Kanda ya Ziwa imejitosa kuzalisha kwa wingi vyakula mbalimbali ili kukabiliana na ongezeko la bei katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika kipindi cha mfungo, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei za bidhaa hasa zinazotumiwa na waumini wa dini ya Kiislamu ili kujipatia faida maradufu.
Meneja wa bodi hiyo, Kanda ya Ziwa, Steven Kubona amesema, wameanza kuzalisha mchele, unga wa sembe katika kiwanda chao ambacho kimeanza kufanya kazi hivi karibuni jijini Mwanza.
Kubona aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Aprili 5, 2022 amesema wanauza maharage, korosho, dengu, ufuta pamoja na mazao mengine wanayoyanunua kutoka kwa wakulima vijijini kwa bei nafuu.
“Mwezi kama huu wafanyabiashara wengi wanapandisha bei za vyakula, lakini sisi tumeamua kuja kitofauti kwa kuwa tunanunua mpunga kutoka kwa wakulima na kuukoboa wenyewe ukiwa na viwango vya hali ya juu na kisha kuwauzia wananchi kwa bei nafuu,” amesema Kubona.
Amesema mazao wanayokoboa wanayauza kwa wananchi mmoja mmoja na jumla na kwamba hatua hiyo inalenga kuwapunguzia mzigo wa bei kubwa Watanzania waliopo Kanda ya Ziwa na maeneo mengi ya nchi.
Kuhusu kumuinua mkulima, Kubona amesema wamefungua milango kwa wakulima wote wa mpunga kuuza mazao yao kwao na kwamba hawahitaji kuwa na dalali.
“Lengo ni kuhakikisha mkulima anainuka kiuchumi na kwamba kiwanda chao bado kina uhitaji mkubwa wa malighafi ikiwamo mahidi na mpunga”amesema
CPB kwa sasa inatoa kipaumbele kwa wakulima wadogo wa mpunga na mahindi na kila mtu atakayefikisha mzigo wake kwao atalipwa fedha siku hiyo hiyo na kuondoka.
Baadhi ya wakazi wa jijini Mwanza wamepongeza jitihada hizo na kueleza kuwa zitasaidia katika kupunguza changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hasa msimu huu wa mfungo wa mwezi mtukufu.
Jamali Jabil amesema bei za vyakula hazishikiki, vimepanda tofauti na mwaka jana kuanzia mchele, viazi mihongo na hata maharagwe
“Hivi sasa mchele tunapima kilo Sh2000, viazi vitamu fungu moja Sh1000 hadi Sh2000, Maharagwe Sh2000, vitu vitu vimepanda sana,” amesema Jabil huku akiiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia waweze kumaliza mwezi wao vizuri.
Latest