CAG: Wahitimu 600,000 wanaingia soko la ajira bila ujuzi Tanzania
- Zaidi ya wahitimu milioni moja wa shule za msingi na sekondari hukatisha elimu kila mwaka na kuingia katika soko la ajira.
- CAG asema ni asilimia 33 kati yao ndiyo huwa na ujuzi wa kazi.
- Sababu kubwa ni kukosa elimu ya ufundi stadi.
Dar es Salaam. Zaidi ya wahitimu 600,000 wa shule za msingi na sekondari wanaokatisha elimu kila mwaka huingia katika soko la ajira Tanzania bila ya ujuzi wa kazi unaohitajika.
Taarifa ya mwelekeo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Julai 2021 inakadiria kuwa zaidi ya wahitimu milioni moja wa shule za msingi na sekondari hukatisha elimu kila mwaka na kuingia katika soko la ajira.
Kati ya idadi hiyo, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma ya mwaka 2020/21 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wanafunzi 333,878 ndiyo walipata elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika vituo 190 vya Serikali na taasisi zinazomilikiwa na watu binafsi.
Hiyo ni sawa na kusema asilimia 33 au wahitimu watatu kati ya 10 ndiyo walipata elimu ya ufundi stadi.
“Hivyo, zaidi ya wahitimu 666,122 wa shule za msingi na sekondari waliokatisha safari yao ya elimu waliingia kwenye soko la ajira bila ujuzi wa kazi unaohitajika,” amesema CAG Charles Kichere katika ripoti hiyo.
Wahitimu wanaokatisha safari yao ya elimu wanaotajwa na ripoti hiyo ni wale ambao wanashindwa kuendelea na elimu ya juu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufeli.
Ili kuhakikisha nguvukazi hii ina ujuzi na stadi zinazohitajika, Serikali inatoa fursa mbadala za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha mafundi, mafundi stadi na wataalamu wengine ambao wanaendana na soko la sasa la ajira na kuongeza uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi.
Soma zaidi:
Nini kinasababisha hali hiyo?
CAG katika ripoti hiyo amesema sababu kubwa inayochangia hali hiyo ni ukosefu wa vyuo vya kutosha vya ufundi stadi vinavyoweza kukidhi ongezeko la wahitimu hao kila mwaka.
Elimu ya ufundi stadi hutolewa na vituo vya ufundi stadi (VETA), vyuo vilivyosajiliwa na NACTE (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi), vyuo vilivyo chini ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na vyuo vya binafsi.
Ingawa Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilidahili wanafunzi wengi zaidi ya uwezo wake mwaka 2020/21, CAG Kichere amesema bado kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawakusajiliwa kutokana na uwezo mdogo wa vituo vya VETA.
“Kwa miaka mitano mfululizo, Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi imeweza kupokea wastani wa asilimia 43 tu ya maombi yote,” ameeleza Kichere katika ripoti hiyo.
Hali hii ina maana kuwa VETA haijafikia hata asilimia 50 ya kudahili maombi yote yaliyopokelewa.

Aidha, ripoti hiyo imebaini kuwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa na VETA ilivuka idadi inayohitajika na vituo, wakati vituo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vinavyosimamiwa na Serikali Kuu na serikali za mitaa havikudahili kulingana na uwezo wake kwa takribani asilimia 31.
“Hali hii inaonesha kuwa vituo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vinavyosimamiwa na Serikali Kuu na serikali ya Mitaa vina uwezo usiotumika huku idadi kubwa ya wahitimu wa shule za msingi na sekondari wakimaliza safari yao ya elimu kila mwaka na kuingia kwenye soko la ajira bila stadi za kazi,” amesema CAG.
Katika mapendekezo yake, ameshauri Serikali ipanue miundombinu iliyopo ya vyuo vya ufundi; ianzishe vyuo vipya vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, na kuimarisha mafunzo pamoja na zana za kufundishia; na ihakikishe uwezo wote uliopo katika vituo vya Serikali kuu na Serikali za mitaa unatumika kudahili na kusomesha wanafunzi wengi zaidi.