Tozo miamala ya simu kupunguzwa Tanzania

June 14, 2022 3:51 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema lengo ni kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania.
  • Punguzo hilo ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa.
  • Yasisitiza tozo zinaendelea kuboresha huduma za jamii. 

Dar es Salaam. Serikali inakusudia kupunguza tozo za miamala ya kifedha inayofanyika kwa njia simu za mkononi katika mwaka ujao wa fedha ili kuwapunguzia Watanzania makali ya maisha.

Punguzo hilo la tozo litafanyika, Serikali itakaporekebisha sheria ya mifumo ya malipo ya Taifa katika mwaka wa fedha wa 2022/23 unaoanza Julai mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Serikali inapendekeza kupunguza tozo ya miamala kutoka kiwango kisichozidi Sh7,000 hadi kiwango kisichozidi Sh4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.

“Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa,” amesema Dk Nchemba aliyekuwa akiwasilisha hotuba ya mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 leo Juni 14 Bungeni jijini Dodoma.

Lengo la hatua hiyo ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wananchi ni kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki cha changamoto kubwa ya kiuchumi na kuweka usawa katika utozaji wa tozo hiyo.

Hata hivyo, Waziri huyo amependekeza kuongeza wigo wa tozo hiyo ili kuhusisha miamala yote ya kielektroniki.

Ukali wa maisha umechangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa duniani kuliko sababishwa na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi. Urusi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani huku Ukraine ikiwa mzalishaji wa ngano. 

Baada ya malalamiko ya muda mrefu juu ya tozo kubwa kwenye miamala ya simu, Serikali inapendekeza kupunguza tozo katika huduma hizo za kifedha. Picha|Nuzulack Dausen. 

“Tozo yaleta neema”

Wakati wananchi hasa wa kawaida wakilalamikia tozo za miamala ya simu, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa tozo hizo zimekuwa na manufaa makubwa katika uboreshaji wa huduma za kijamii nchini ikiwemo elimu. 

Dk Nchemba katika hotuba yake amesema katika mwaka huu wa fedha, Serikali imekamilisha maboma 560 ya  vyumba vya madarasa katika shule za sekondari nchini kutokana na tozo za miamala ya simu ambapo  Sh7 bilioni zilitolewa kukamilisha ujenzi huo. 

“Vilevile,  Serikali imewezesha ujenzi wa vituo vya afya 234  kwa kutumia tozo ya miamala ya simu yenye  thamani ya Sh86 bilioni,” amesema Waziri Nchemba.

Enable Notifications OK No thanks