Mfumuko bei za bidhaa wapaa Tanzania

July 11, 2022 1:06 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.4 katika mwaka ulioshia Juni  2022  kutoka asilimia 4 iliyorekodiwa Mei mwaka huu.
  • Umechangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeongezeka hadi kufikia asilimia 4.4 katika mwaka ulioshia Juni  2022  kutoka asilimia 4 iliyorekodiwa Mei mwaka huu ikichangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Taarifa ya mfumuko wa bei iliyotolewa leo Julai 11, 2022 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ni pamoja na ngano kwa asilimia 3.8, na mchele kwa  asilimia 14. 

Bei ya bidhaa zingine ni mahindi, bei yake imeongezeka kwa asilimia 30.9, viazi vitamu ( asilimia 20.3) na mihogo mibichi (asilimia 14.4).

“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni  2022 kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Juni 2022 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Mei, 2022,” imeeleza taarifa ya NBS.

Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizo changia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, ni pamoja na mabati, mavazi, usafirishaji, gesi ya kupikia majumbani, mafuta ya taa na nauli za mabasi.


Zinazohusiana: 


Miezi ya hivi karibu kumekuwa na malalamiko juu ya kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini ikiwemo unga wa mahindi uliokuwa ukiuzwa Sh1200 mwanzoni mwa mwaka 2022, kwasasa unga huo unauzwa kati ya Sh1600 hadi Sh1800 kwa kilo.

Ngano iliyokuwa ikiuzwa Sh1400 kwa kilo kwa sasa inauzwa kati ya Sh2000 hadi Sh2400.

Kupanda kwa bei bidhaa ikiwemo mafuta ya vyombo vya moto kumesababisha gharama za maisha kupanda kwa sababu watu wanalazimika kutoboa zaidi mifuko yao kuzipata bidhaa hizo. 

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23 Juni mwaka huu alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupunguza mfumuko huu wa bei ikiwemo kupunguza kodi kwenye bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Pia itaimarisha usimamiaji wa Sheria ya Ushindani namba 8 ya mwaka 2003 ikayozuia kupanda kwa bei za  bidhaa kiholela na kutafuta vyanzo mbadala vya  upatikanaji wa bidhaa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW