Majaliwa atoa maagizo mazito kwa TCU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (wa kwanza kulia) akipata maelezo kuhusu ubunifu wa ndege leo Julai 19, 2022 katika Maonesho ya 17 ya Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Mkoani Dar es Salaam. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Aitaka kuongeza udhibiti wa ubora wa vyuo vikuu.
- Aitaka kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iongeze jitihada katika udhibiti wa ubora wa vyuo vikuu nchini ili kuhakikisha kuwa azma ya kuwa na mitaala inayojibu mahitaji ya soko la ajira inatimia.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Julai 19, 2022) wakati akifungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam ambapo umesema taasisi zote za elimu ya juu ziendelea kufanya mapitio ya mitaala iliyopo kwa kuzingatia miongozo iliyopo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Pamoja na kusimamia taaluma, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, pia iongeze jitihada katika kusimamia masuala ya utafiti na ushauri katika vyuo vikuu ili kuvifanya viwe chachu ya maendeleo na suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo ya jamii yetu na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Kiongozi huyo mkuu wa shughuli za Serikali amesema taasisi za elimu ya juu ambazo ni wazalishaji wa maarifa na ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, hazinabudi kuwa mbele siku zote ili kuhakikisha kuwa zinabuni na kuanzisha programu mpya zinazokwenda na wakati.
“Taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti na maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hususan viwanda, na kuweka utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema.
Sekta ya elimu ya juu imeendelea kukua kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali, amesema Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tanzania ina vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 47 ambapo 28 kati yake vinamilikiwa na sekta binafsi.
“Serikali inatambua na kuthamini sana mchango wenu katika kuwahudumia Watanzania wote kwa kutoa elimu bora bila ubaguzi wa aina yoyote. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Serikali ishirikiane kwa karibu na sekta binafsi na kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuharakisha azma yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi wote,” amesisitiza Majaliwa.
Aidha, ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kusimamia na kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu mwenendo wa baadhi ya asasi zilizosajiliwa kuratibu wanafunzi wanaokwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Profesa Penina Muhando amesema maonesho hayo yana lengo la kukuza ushirikiano baina ya wao kama wasimamizi wa elimu ya juu na taasisi zinazotoa huduma pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa pamoja huduma zinazotolewa na taasisi hizo.
Latest