Kilimo mashamba makubwa kupata msukumo mpya Tanzania
- Zimetengwa na Serikali kuendeleza mashamba hayo
- Lengo ni kuongeza uzalishaji na kupunguza uagizaji wa mazao nje ya nchi.
- Alizeti na chikichiki kujumuishwa katika mashamba hayo.
Dar es Salaam. Huenda Tanzania akaanza kujitoshereza kwa chakula na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula na sukari baada ya Serikali kuweka mikakati ya kufufua na kuendeleza mashamba makubwa kwa ajili ya mazao muhimu.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya kuendeleza mashamba makubwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Kagera ambalo una eneo kubwa ambalo bado halijatumika kwa shughuli za kilimo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa ziara yake kwenye kiwanda cha sukari Kagera, kilichopo mkoani Kagera, leo Juni 9 amesema Tanzania bado ina uhaba wa sukari na mafuta ya kula.
“Nataka nitumie jukwaa hili la sukari kuzungumzia mafuta ya kula….Ili tuweze kujitosheleze kwa mafuta ya kula lazima tuwe na mashamba ya kutosha,” amesema Rais.
Kwa mujibu wa wizara ya Kilimo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ni wastani wa tani 300,000 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 650,000 kwa mwaka.
Kutokana na upungufu huo, Tanzania huagiza tani zipatazo 350,000 za mafuta ya kula ambapo hugharimu zaidi ya Sh470 bilioni kwa mwaka.
Ili kutatua uhaba wa mafuta, Rais samia amewataka viongozi wa mikoa kuainisha maeneo ambayo hayana kazi ili zoezi la kuanzisha mashamba makubwa lianze, hususani mkoa wa Kagera ambapo heka 70,000 mpaka 100,000 zinahitajika.
“Kagera mna ardhi nzuri mna ardhi kubwa lakini maeneno mengi hayatumiki…moja kati ya mashamba tuliyoyatarget ni hapa Kagera,” amesema Rais.
Mazao yatakayo pewa kipaumbele kwenye miradi hiyo ya mashamba makubwa ni michikichi na alizeti ili kuzalisha mafuta ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi hata nje ya nchi.
“Tutapanda sunflower (alizeti) kwa mbegu za kisasa, michikichi kwa mbegu za kisasa ili tuweze kujitosheleza mafuta ndani ya nchi na ikiwezekana twende nje ya nchi…tunaweza kuzalisha wenyewe,” amesema Rais.
Soma zaidi:
- Gharama ya uhai: Ukosefu wa zanahati unavyohatarisha maisha Maswa
- Wakulima wa mahindi walivyovuna zaidi ya Sh10,000 kwa gunia Tanzania
- Kupanda bei za vyakula, CPB waja na suluhu
“Wawekezaji njooni”
Kiongozi huyo mkuu wa nchini amesema Serikali inawahakikishia usalama wa vitega uchumi vinavyowekwa nchini wawekezaji wote watakaowekeza Tanzania, na itahakisha uwepo wa mazingira yanayovutia uwekezaji endelevu katika sekta zote za uchumi ikiwemo kilimo.
Rais Samia yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi iliyoanza tangu jana Juni 8, ambapo akiwa njiani amezungumza na wananchi, wabunge na madiwani na kutatua kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili.
Latest