Rais Samia azindua kiwanda kupunguza uhaba wa sukari Tanzania
- Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka na kuchakata zaidi ya tani 500,000 kwa mwaka.
- Rais Samia ameelezea umuhimu wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kiuchumi na kijamii.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua kiwanda kipya cha sukari cha Mkulazi mkoani Morogoro kitakachozalisha tani 50,000 kwa mwaka, hatua itakayoisaidia kupunguza uhaba wa sukari nchini na kuongeza ajira.
Uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo wilayani Kilosa utafanya Tanzania kuwa na viwanda sita vya sukari ambayo hutumika zaidi kwa matumizi ya chakula nyumbani na viwandani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mkulazi, Dk Hildelitha Msita amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukar kwa mwaka na kuchakata tani 500,000 za miwa kwa mwaka.
“Kiwanda hiki kimejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu…lakini pia ikiongezwa gharama kidogo tunaweza kufikia uzalishaji wa tani 75,000 kwa mwaka,” amesema Dk Msita.
Mbali na kuzalisha sukari, kiwanda hicho kwa mujibu wa tovuti yake, kinatarajiwa kuzalisha umeme kiasi cha megawati 15 ambazo kati ya hizo megawati nane ni kwa ajili ya mahitaji ya ndani na megawati saba zilizosalia zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mkulazi kinakuwa kiwanda cha tatu ndani ya mkoa wa Morogoro baada ya Kilombero Sugar na Mtibwa Sugar ambavyo vimekuwa vikichangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa sukari nchini.
Mahitaji ya sukari yamezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka Tanzania kutokana na ongezeko la watu jambo linaloendelea kuleta nakisi ya sukari nchini na kuifanya Serikali kuingiza kutoka nje kiwango kilichosalia.
Sukari yazidi kuhitajika
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo mahitaji ya sukari Tanzania ni tani 650,000 kwa mwaka wakati uzalishaji wake mwaka 2024 ukikadiriwa kuwa kati ya tani 520,000 hadi 550,000, chini ya mahitaji yote kwa takriban tani 100,000.
Kwa mujibu wa bajeti ya kilimo ya mwaka 2024/2025, kiwango cha ujumla cha uzalishaji wa sukari kinatarajiwa kuwa takriban tani milioni 1.1 huku uzalishaji huo ukichagizwa zaidi na jitihada za kuimarisha teknolojia, kuboresha miundombinu na kuhamasisha wakulima.
Rais Samia amesema kiwanda hicho cha Mkulazi kina umuhimu wa kipekee kwa Taifa na kwamba kitasaidia sana katika kupunguza upungufu wa sukari nchini na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Mkulazi itapunguza uhaba wa sukari
“Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kiwanda hiki kinafanikiwa na kuongeza uzalishaji wa sukari kwa mahitaji ya ndani na nje ya nchi,” amesema Rais Samia wakati akizindua kiwanda hicho leo mkoani Morogoro.
Kiwanda hicho, kinachomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kitachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo kwa kutoa ajira zaidi ya 5,000 na kusaidia kuinua kipato cha wakulima wa miwa.
Rais Samia ameikaribisha sekta binafsi kushirikiana na Serikali kuwekeza katika jitihada za upanuzi wa kiwanda hicho ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kupunguza uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.