Hapana: Chanjo ya Uviko-19 haibadilishi hedhi kwa wanawake

October 6, 2022 7:46 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa afya wasema ni uzushi unaolenga kuzuia watu kupata chanjo.
  • Wafafanua hakuna chanjo ya Uviko-19 inayoweza kutoka nje ya mwili.

Dar es salaam. Juhudi  za kukabiliana na janga la Uviko-19 zinaendelea ambapo pamoja na njia nyingine kama kuvaa barakoa na kunawa mikono kupata chanjo ya Uviko-19 inatajwa kama ndiyo njia salama zaidi ya kujikinga na ugonjwa huo.

Pamoja na wataalamu wa afya kuthibitisha kuwa chanjo za Uviko-19 ni salama na hazina madhara kwa afya ya binadamu bado kumekuwepo na habari potofu ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye jamii kuhusu chanjo.

Uzushi wa hivi karibuni ni ule unaodai kuwa mwanamke ambaye hajapata chanjo anapokuwa karibu na wanawake waliopata chanjo basi mzunguko wake wa hedhi unaweza kuathirika.

Wataalamu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) wamekanusha uzushi huo kwa kufafanua kuwa kitaalamu jambo hilo huitwa ‘Vaccine shedding’ ambapo sehemu ya chanjo hutolewa ndani au nje ya mwili ikiwa tu ilikuwa na sehemu dhaifu ya virusi.

“Hakuna chanjo ya Uviko-19 iliyoidhinishwa ambayo ina sehemu ya virusi kwa hiyo watu waliochanja hawawezi kutoa virusi vya Corona kupitia chanjo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa Septemba 27 mwaka huu.


Soma Zaidi


WHO imesisitiza kuwa kwa namna yoyote ile kuwa karibu na mtu aliyepata chanjo hakuwezi kuathiri mzunguko wa hedhi wa mwanamke hivyo wamewataka watu kupuuza madai hayo yenye lengo la kukwamisha juhudi za utoaji wa chanjo.

Itakumbukwa kuwa ni miaka mitatu sasa imepita tangu ugonjwa wa Uviko-19 uibuke huku tiba kamili ikiwa haijapatikana na chanjo imetajwa kama njia pekee iliyothibitishwa  kuwa na uwezo wa kukinga watu na ugonjwa huo unaoathiri mapafu.

Kwa mujibu wa WHO mpaka kufikia Septemba 27 mwaka huu jumla ya dozi bilioni 12.6 za chanjo zilikuwa zimetolewa duniani kote ambapo Tanzania mpaka sasa watu milioni 18.8 wamepata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW