Unachoweza kufanya kujikinga na maambukizi mapya ya corona
- Waliowahi kupata corona na wakapona wapo kwenye hatari ya kupata tena virusi hivyo.
- Watu ambao hawajapata chanjo wapo kwenye hatari zaidi ya maambukizi mapya.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea na mapambano dhidi ya janga la uviko-19, kumeibuka hofu miongoni mwa watu juu ya uwezekano wa kupata tena virusi hivi na kurudi kwenye maradhi na vifo vinavyoendelea kumaliza maisha ya watu duniani.
Kama wewe ni mmoja wa watu wenye hofu ya kuukwaa kwa mara ya pili ugonjwa huu, nikutoe shaka kwamba kuna njia ambazo unaweza kuzitumia kujiepusha na maambukizi hayo kwa mara nyingine.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa (CDC), mtu aliyewahi kupata ugonjwa wa Corona na akapona yupo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa tena virusi hivyo kwa mara nginine.
“Virusi vinabadilika kila wakati, ikiwemo virusi vinavyosababisha Uviko-19. Mabadiliko haya yanaweza kusababisha aina mpya za virusi ambazo zinaweza kuongeza hatari ya maambukizi mapya,” inasema taarifa ya CDC iliyotolewa 9 Septemba, 2022
Ripoti ya utafiti wa kituo hicho uliotolewa 21 Agosti, 2021 iliyopewa jina la ‘kupunguza hatari ya maambukizi ya uviko 19 kwenye mji wa Kentucky nchini Marekani kwa mwezi Mei na Juni 2021” umeonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mtu kuambukizwa tena uviko-19 muda mfupi baada ya kupon ugonjwa huo.
Hata hivyo, hatari hiyo inaweza kuwakabili zaidi watu ambao bado hawapata chanjo ya Uviko-19.
Soma zaidi:
Unawezaje kujikinga na Uviko-19 usikupate tena?
Zipo njia nyingi za kujikinga na maambukizi ya uvikiko-19 kwa mara ya pili, japo njia hizi zinafanana na zile za kujikinga na maambukizi mapya kama zinavyoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hatua ya kwanza unayoweza kuchukua kukabiliana na maambukizi ya mara ya pili ni kupata chanjo kwa wakati sahihi.
Hakikisha unanawa mikono kila mara kwa kutumia sabuni na maji tiririka kwa angalau sekunde 20, ama tumia kitakasa mikono. Kwa kufanya hivyo utakuwa una jikinga na Uviko-19.
Vaa barakoa unapokua sehemu zenye watu wengi kama vile sokoni ama kwenye usafiri wa umma. Hii ni muhimu hasa katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huo.
Funika mdomo wako na pua kwa kutumia kiwiko ama tishu unapokohoa ama kupiga chafya. Tupa tishu sehemu salama baada ya kuitumia.
Kumbuka kukaa umbali kati yako na watu wengine kadiri inavyowezekana. Hii inamaanisha kukaa umbali wa mita 1 kati yako na watu wengine, epuka mikusanyiko na maeneo yenye watu wengi