Microsoft, Apple zawarahisishia maisha watumiaji wake
- Zaunganisha huduma ya kuhifadhi picha, video mtandaoni.
- Programu ya iCloud ya Apple kuwezesha watumiaji wa microsoft kupata picha kwa urahisi.
Dar es Salaam. Watumiaji wa Microsoft wanaotumia mfumo endeshi wa Windows 11 hawatakua na hofu tena ya kuzipata picha zao kwenye simu za iPhone na tableti za iPad kwa sababu suluhu imepatikana.
Wataweza kuzipata kwa sababu kampuni ya Microsoft ya Marekani imeunganisha programu yake na huduma ya iCloud ya kampuni ya Apple inayotumika kuhifadhi vitu mtandaoni.
Maboresho haya yanayolenga uunganishaji wa huduma za kampuni hizi mbili yametangazwa kwenye blogu ya Microsoft katika tukio maalum la Microsoft’s Surface la Oktoba 12, 2022 wakati kampuni ya Redmond ilipokuwa ikitambulisha vifaa vyake vipya.
Uunganishi huu wa huduma utawawezesha watumiaji wa vifaa vya Apple kufungua video na picha zao kwa kutumia kompyuta za Microsoft kwa kutumia huduma ya uhifadhi wa mtandaoni ya iCloud.
iCloud ni huduma kutoka Apple ambayo inawezesha uhifadhi na ushiriki wa picha, mafaili, madokezo, nenosiri na data nyingine kwa usalama kupitia mtandao na kuzisasisha kiotomatiki kwenye vifaa vyote kwa watumiaji wake.
“Programu ya Picha za Microsoft hukuruhusu kuona, kupanga, na kushiriki picha kutoka OneDrive kwenye Kompyuta yako, na ukiwa na sasisho hili, utaweza kuongeza na kufikia picha zako za iCloud moja kwa moja kutoka ndani ya programu pia,” Dave Grochocki, Meneja Mkuu wa Bidhaa kutoka Microsoft amesema.
Soma zaidi
Ili kufanikisha uunganishaji huu, mtumiaji anapaswa kupakua programu ya iCloud kupitia duka la Microsoft store kisha kuingia kwa kutumia utambulisho wake wa Apple (Apple ID).
Kumbuka kuchagua kipengele cha Picha cha ndani ya program ili kuiruhusu Microsoft 11 kufuingua maktaba ya iCloud.
Kwa sasa, programu hii mpya ya picha (iCloud Photos) inapatikana kwenye Dev Channel kwa baadhi ya watumiaji wa Microsoft Windows Insider, lakini itapatikana kwa watumiaji wote kufikia Novemba mwaka huu.
Uunganishaji wa programu za kampuni za Microsoft na Apple unawapa watumiaji wao uwezo wa kuzifikia na kufungua picha, muziki na vipindi vya televisheni kati ya majukwaa hayo kupitia mtandao kwa urahisi.
Huo ni mwanzo wa makampuni hayo kuongeza ushirikiano. Microsoft pia imethibisha itaachia programu za utazamaji wa vipindi vya video na muziki za watumiaji wa Apple Tv na Apple Music mapema mwaka ujao kupitia duka lake kama ilivyo kawaida.
Latest