Waziri Bashe: Hamtakufa njaa
- Asema Serikali inapeleka mahindi maeneo yenye upungufu wa chakula.
- Wananchi kuuziwa mahindi iliyo chini ya bei ya soko.
- Kuanzisha kilimo cha umwagiliaji Kanda ya Ziwa.
Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeanza kupeleka mahindi katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa na kuyauza kwa bei ya chini ili kuwanusuru wananchi na baa la njaa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya bei ya mahindi kuendelea kupanda nchini huku baadhi ya watu wakishindwa kumudu bei ya soko, jambo linalotishia uhai wa maisha yao.
Sababu nyingine iliyochangia bei ya mahindi kupanda ni kufunguliwa kwa mipaka na kusuasua kwa mvua katika msimu wa mwaka huu na hivyo wakulima kupata mavuno kidogo.
Hata hivyo, Waziri Bashe ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wananchi wa Kanda ya Ziwa wasiwe na hofu ya kufa njaa kwa sababu Serikali itawauzia mahindi kwa bei ya chini.
Maeneo hayo ambayo yameanza kupokea mahindi ni pamoja na Wilaya za Ukerewe na Sengerema mkoani Mwanza , Bunda (Mara) na Mkoa wa Geita ambapo mahindi hayo yatauzwa kwa bei ya chini ya soko.
“Serikali ina akiba ya chakula cha kutosha hivyo wananchi hawatokufa njaa na kinachofanyika tunaangalia maeneo ambayo mahindi yamepanda sana na kupelekewa mahindi hayo yatakayouzwa kwa bei ya chini ya sokoni,” amesema Bashe.
Soma zaidi:
Mipango ya muda mrefu kuwawezesha wakulima kuwa na akiba ya kutosha, amesema hivi sasa wataanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria ili kuwe na chakula kingi nchini.
Amesema kilimo hicho kitafanyika kwenye maeneo yote yaliyo karibu na Ziwa Victoria ikiwemo Mwanza kwa wilaya zote zilizopo kando kando ya ziwa, Mara na Kagera.
“Mungu katupa maji na tutaanza kuyatumia maji hayo na sasa tutaanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kuanzia Tarime mkoani Mara hadi Kagera lengo ni kutumia neema ya maji ambayo Mungu amatupatia,” amesema Bashe.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya Septemba 2022 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki ya Tanzania (BoT), gunia la kilo 100 la mahindi lilikuwa linauzwa kwa Sh89,039 Agosti mwaka huu.
Bei hiyo imepanda kutoka Sh44,811 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.
BoT katika ripoti hiyo imeeleza kuwa akiba ya chakula katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa tani 144,410 hadi kufikia Agosti 2022 ikiongezeka kutoka tani 140,695 zilizokuwepo mwezi uliotangulia.
Pia Agosti, NFRA iliza tani 2,009.2 za mahindi kwa wafanyabiashara na wakoboaji nafaka huku ikinunua tani 5,966.3 za mahindi na tani 211.5 za mtama.
Latest
