Chanjo ya Uviko-19 ni salama kwa wajawazito?

November 2, 2022 11:59 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Tafiti zaonesha hakuna mjamzito aliyeathirika kwa kupata chanjo.  
  • Chanjo ya Uviko-19 huimarisha afya ya mama na kinga ya mtoto aliyepo tumboni.

Dar es salaam. Wakati maelfu ya watu kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiendelea kupata chanjo ya Uviko-19 umeibuka uzushi unaodai kwamba chanjo hiyo huathiri uzazi wa mwanamke pamoja na kuharibu mimba jambo ambalo limewaweka baadhi ya watu njia panda.

Hata hivyo, timu ya wataalamu wa afya kutoka tovuti ya Viral Fact inayojishughulisha na uelimishaji wa watu juu ya Uviko-19 ambayo hutumiwa pia na Shirika la Afya duniani Ukanda wa Afrika wamekakusha madai hayo na kuwataka watu kupuuza.

“Mwanamke mjamzito anaweza kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata changamoto za ujauzito wake ikiwa ataambukizwa Uviko-19, chanjo hazina viambata vyovyote vinavyoweza kusababisha madhara kwa mama mjamzito au mtoto aliyepo tumboni,” imeeleza tovuti hiyo.

Wataalamu hao wamefafanua kuwa tafiti za kitabibu zimeonesha mwanamke mjamzito anapopata chanjo husafirisha kinga za mwili mpaka kwa mtoto aliyepo tumboni na hivyo kinga zake huimarika zaidi.

Kwa mujibu wa Viral Fact wajawazito zaidi ya 140,000 waliopata chanjo ya Uviko-19 nchini Uingereza hawakukumbana na changamoto yoyote ya kiafya ambapo msisitizo umetolewa kuwa chanjo ni salama na zinasaidia kumlinda mama na mtoto.

“Kama wewe ni mjamzito na unatamani kupata chanjo zungumza na mtaalamu wa afya akueleze madhara ya Uviko-19 na faida za kupata chanjo, hilo litakusaidia kufanya maamuzi sahihi ukiwa na taarifa sahihi,” wanasisitiza Viral Fact.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW