Tanzania itakavyofaidika ziara ya Rais Samia nchini China

November 4, 2022 1:11 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping wakati akikagua gwaride la heshima katika ukumbi wa The People Great Hall, Beijing nchini China, Novemba 3, 2022. Picha | Ikulu. 


  • Ni pamoja na kukua kiuchumi na kutanua sekta ya uwekezaji.
  • Hiyo ni ziara ya kwanza baada ya miaka nane kupita.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini China hii leo Novemba 4, 2022 mara baada ya kuwepo nchini humo kwa siku tatu kufuatia mualiko aliopewa na Rais wa China Xi Jinping.

Huenda ukawa miongoni mwa watu wanaotaka kufahamu ni kwa namna gani Tanzania itanufaika na ziara hiyo ya kwanza kabisa kufanywa na kiongozi kutoka Afrika tangu Rais Xi Jinping alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China kwa mara ya tatu.

Kukua kiuchumi

Rais Samia akiwa nchini China ameshuhudia utiaji saini wa mikataba na hati za makubaliano ya kimkakati 15 ambayo imelenga kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana Novemba 3, 2022 imeeleza kuwa kupitia makubaliano hayo Tanzania imesamehewa sehemu ya deni lake yenye thamani ya Sh31.4 bilioni fedha ambazo zitatumika katika masuala mengine ya maendeleo.

“Miongoni mwa mikataba na makubaliano yaliyotiwa saini ni kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la usafirishaji wa maparachichi kutoka Tanzania kwenda China.

“Pia wametia saini mkataba unaohusu msaada wa Yuan milioni100  sawa na Sh32 bilioni za Tanzania  kwa ajili ya  ushirikiano wa kiuchumi na kitaalam baina ya nchi hizo mbili,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kupanuka kwa soko la kuuza zao la parachich nchini China  kunaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa zao hilo katika ukanda wa Afrika Mashariki  na kuinua uchumi wa wananchi wake kwani kwa sasa zao hilo linauzwa pia katika nchi za Afrika Kusini pamoja na India.


Soma zaidi:


Ziara hiyo pia itatoa fursa ya kukua kwa sekta ya uvuvi kwani kumetiwa saini makubaliano ya uwepo wa soko la mabondo ya samaki pamoja na bidhaa nyingine za uvuvi kutoka Tanzania kwenda China.

Pamoja na China  kutoa msaada wa Yuan milioni 100 ambazo ni sawa na Sh32.1 bilioni, Tanzania imepewa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani Dola za Marekani milioni 56.72 ambazo ni sawa na Sh132.2 bilioni za Tanzania.

“China imetoa mkopo wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 56.72 wenye masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar, Terminal II,” inaeleza taarifa hiyo.

Kupanua uwekezaji

Huenda ziara hiyo ikaongeza kasi ya uwekezaji wa kampuni za China nchini Tanzania na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania. Kampuni za nchi hiyo zina miradi 1,098 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 9.6 (Sh22.3 trilioni) ambayo ilikuwa imesajiliwa hadi Octoba 2022.

Taifa la China ndilo linaongoza kwa kuwa na miradi mingi nchini katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano, madini na uvuvi na kuzalisha ajira 131,718.

Ushirikiano wa hizo mbili uliodumu kwa muda mrefu unaweza kuimarika katika nyanja mbalimbali za utamduni, undugu na kuwafaidisha zaidi wananchi wake. 

Pamoja na kufanya mazungumzo na Rais wa China, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na  Waziri Mkuu wa China pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo.

Ziara hiyo inafanyika katika kipindi ambacho Tanzania na China zinasheherekea miaka 58 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali na  ikiwa imepita miaka nane tangu Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete alipozuru nchi hiyo Oktoba mwaka 2014.

Enable Notifications OK No thanks