Mikoa mitano yenye watu wachache zaidi Tanzania
- Ni kwa mujibu wa matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
- Mkoa wa Njombe ndiyo una watu wachache zaidi kwa Tanzania Bara.
Dar es salaam. Idadi ya Watanzania imeongezeka kwa asilimia 3.2 ndani ya kipindi cha miaka 10 hadi kufikia milioni 61.7 mwaka huu, huku Njombe, ukitajwa kuwa mkoa wenye watu wachache zaidi Tanzania Bara.
Idadi hiyo imeongezeka kutoka watu milioni 44.9 waliohesababiwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizindua matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 jana Oktoba 31 jijini Dodoma alisema ongezeko la idadi ya watu linaweza kuwa mzigo kwa Taifa.
Kutokana na ongezeko hilo, ametaka kuwepo mikakati madhubuti ya kuwahudumia watu ili kufikia malengo ya maendeleo.
Licha ya ongezeko hilo, Mkoa wa Dar es salaam umeongoza kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu nchini Tanzania wapatao milioni 5.4 sawa na asilimia 8.7 ya watu waliopo nchini. Hata hivyo, ipo mikoa yenye watu wachache zaidi ambayo baadhi idadi ya watu wake hawazidi milioni 1.
5. Songwe
Songwe ni mkoa uliopo Nyanda za Juu kusini mwa Tanzania, awali ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Mbeya kabla ya kutangazwa rasmi Januari 29, 2016 kuwa Mkoa mpya.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu, Songwe ina jumla ya watu milioni 1.3 ambapo kati yao wanawake ni 701,008.
Songwe ina jumla ya shule 626 zikiwemo 130 za sekondari. Ina vituo vya kutolea huduma za afya 247, zikiwemo zahanati 200.
Viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakiwa kwenye uwanja wa Michezo wa Lake Tanganyika kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara Oktoba 18, 2022. Picha | Ikulu.
4. Lindi
Licha ya kuwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 67,000 za mraba ambalo ni sawa na asilimia 7.1 ya eneo la Tanzania Bara bado mkoa wa Lindi hauna idadi kubwa ya watu.
Matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi yanaonesha Lindi ina wakazi milioni 1.1 ikiwa juu kidogo ya Songwe.
Matokeo hayo pia yamebainisha kuwa Lindi ina jumla ya vituo 303 vya kutolea huduma za afya na shule 633 za msingi 530 na za sekondari 133.
3. Iringa
Mkoa wa Iringa umezidiwa watu 1,300 tu na Lindi kwani wenyewe una jumla ya watu milioni 1.1 wakiwemo wanawake 618,415.
Mkoa huu mkongwe uliopo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania una jumla ya shule 735 huku vituo vinavyotoa huduma za afya vikiwa 349 zikiwemo zahanati 283. Mkoa huo uligawanywa mara mbili na kuunda Mkoa mpya wa Njombe.
Zinazohusiana:
2. Katavi
Katavi ni mkoa ulioanzishwa rasmi mwaka 2012 baada ya kuugawa Mkoa wa Rukwa. Licha ya idadi ya watu kuongezeka mara mbili zaidi ya ilivyokuwa mwaka 2012 bado mkoa huu ni miongoni mwa mikoa yenye idadi ndogo ya watu Tanzania.
Kwa sasa una idadi ya watu milioni 1.1 isipokuwa umezidiwa takribani watu 39,770 na Iringa ambao ni sawa na asilimia 3.4 ya wakazi wa Katavi.
Mkoa wa Katavi una vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 134 na kwa upande wa elimu, Katavi ina shule 328.
1.Njombe
Njombe ndiyo mkoa pekee kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ambayo haijafikisha idadi ya watu milioni 1 kwa mujibu wa matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Mkoa huo una watu 889,946 ambapo kati yao 420,533 ni wanaume. Idadi hiyo ni pungufu mara sita zaidi ya ile ya mkoa wa Dar es salaam.
Watu wa Njombe wanapata huduma za kiafya kutoka kwenye zahanati 271, vituo vya afya (44) pamoja na hospitali 22. Upande wa elimu Njombe kuna jumla ya shule 683 zikiwemo shule za msingi 544.
Kwa upande wa Zanzibar, Mkoa wa Kusini Unguja ndiyo wenye idadi ndogo zaidi ya watu wapatao 257,290.