Simulizi ya vijana wanaochangamkia biashara ya mabondo Ziwa Victoria

April 6, 2022 5:40 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mahitaji yake nje ya nchi yawavuta vijana kufanya biashara hiyo.
  • Yachangia uvuvi haramu na kuyumba bei ya samaki.
  • Wadau washauri Serikali iweke utaratibu mzuri wa biashara hiyo.

Dar es Salaam. Kwa sasa, unaweza kusema mabondo yana thamani zaidi kuliko samaki kwa sababu wafanyabiashara wanayasaka kila kukicha ili kujipatia kiasi kikubwa cha pesa ambacho hawawezi kukipata wakiuza samaki wa kawaida.

Mfanyabiashara wa samaki soko kuu la Mwanza, Keflen Juma anasema bondo ndiyo faida yake. 

“Unakuta samaki niliowanunua wamenisababishia hasara na wakati mwingine hawauziki wote ndiyo maana tunatoa mabondo na kuyauza ili kupunguza hasara iliyopatikana na sisi tupate faida,” anasema Juma.

Amesema samaki mkubwa mwenye kilo 80 anatoa bondo lenye gram 200 ambazo linalompatia kati ya Sh90,000 hadi Sh100,000 na inategemea na bei ya soko ya siku hiyo.

“Unakuta samaki wa kilo 80 tunamununua Sh80,000 na kuja kumuuza kati ya Sh85,000 hadi 90,000 bado haujatoa gharama zingine, hivyo ili kupata faida tunatoa bondo na kuliuza ili kufidishia gharama na sisi kupata faida,” anasema Kefleni.

Nini siri ya mabondo?

Wafanyabiashara na wanunuzi wa mabondo waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wamesema mabondo yanahitajika sana kwa wakati huu kwa sababu yanatumika katika shughuli za utabibu. 

Mmoja wa wafanyakazi katika kampuni zinazojishughulisha na ununuzi wa mabondo,  Zuberi Ndibalema anasema mabondo ni utumbo wa samaki aina ya sangara ambapo hutumika kama chakula na matumizi mengine ya matibabu hasa nje za nje.

“Ni mboga hasa akina mama inafaa sana kwa sababu wenzetu wanasema akitumia hii inamtengeza mtoto kuwa mzuri tumboni. Pili kwenye nyuzi za binadamu wanaposhona haitaji tena kuzitoa.

“Ni chakula hata kwa afya ya mwanaume ni supu nzuri inatengeneza kuwa lijali,” anasema Ndibalema.

Mabondo hayo huuzwa yakiwa mabichi na baadaye hukaushwa kabla hajasafirishwa kwenda nje ya nchi hasa China.

Wavuvi katika kisiwa cha mchangani wilaya ya Sengerema wakiendelea na shughuli zao ndani ya Ziwa Victoria. Picha|Mariam John.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, biashara ya mabondo ilianza miaka ya 1990 ambapo viwanda vingi vilisafirisha mabondo yakiwa yamegandishwa kwenye barafu kwenda nchi za bara la Asia.

Mahitaji ya bidhaa hiyo yaliongezeka na mwaka 2000 wafanyabiashara walianza kuja nchini na kujishughulisha na ukusanyaji wa mabondo, kuyakausha na kuyapeleka katika masoko ya China na Hong Kong.

Katika mikoa inayozungukwa na Ziwa Victoria, wizara hiyo inabainisha kuwa kuna viwanda 22 vya kuchakata mabondo kati ya hivyo sita vilipewa kibali na hadi kufikia mwaka 2018 kulikuwa na viwanda 9 vya kuchakata mabaondo na 13 vilivyofungiwa.


Biashara ya samaki hatarini

Wakizungumza na Nukta habari baadhi ya wavuvi katika visiwa mbalimbali vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria wamesema kushamiri kwa biashara ya mabondo pia kumechangia kuyumba shughuli nyingine za uvuvi wa samaki, jambo linalowakatisha tamaa kuendelea na uvuvi.

“Biashara ya mabondo imechangia kwa sehemu kubwa biashara ya samaki kutouzika, mfanyabiashara wa samaki aina ya sangara hawezi kuuza samaki huyo bila kutoa bondo na bondo hilo lina gharama kubwa,” anasema mvuvi katika mwalo wa Muswahili jijini Mwanza, Martine John. 


Zinazohusiana:


Mbali na biashara hiyo pia ipo changamoto ya baadhi ya wavuvi kushirikiana na vibarua wasio waaminifu kuwapora samaki ili kupata mabondo, jambo ambalo pia linachochea uvuvi haramu unaochangia kuharibu rasilimali za majini.

“Vitendo vya unyang’anyi wa samaki na zana za uvuvi vimeibuka kwa kasi na hii ni kutokana na wanunuzi wa mabondo ya samaki aina ya sangara,” anasema Joseph Charles, mvuvi katika mwalo wa Nafuba wilayani Ukerewe.

Charles anakiri kuwa biashara ya mabondo sasa inafanywa na wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao wengine huenda hadi ndani ya Ziwa Victoria hali inayosababisha kuongeza kwa uhalifu huo unaolenga kupata mabondo.

“Baada ya samaki kutumbuliwa na kutolewa mabondo hutupwa ndani ya maji hivyo kuwakosesha mapato wamiliki wa mitumbwi,” anasema Charles.

Mvuvi mwingine katika kisiwa cha Ilugwa kilichopo katika ziwa hilo, Marco Mgaziba anasema yeye anamiliki mitumbwi ya uvuvi 10 na kwamba biashara ya samaki aina ya sangara  imekuwa ngumu baada ya kuingiliwa na wafanyabiashara wa mabondo.

“Vibarua wa uvuvi  wanashirikiana wahalifu hao kutimiza malengo yao ovu wakiwa huko ndani ya ziwa, samaki hutumbuliwa na kutolewa mabondo na wavuvi kuwauzia hao huko huko wakifika ufukweni wanakuwa na samaki wachache,” anasema Mgaziba.

Mikakati ya kuboresha biashara ya mabondo

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mabondo mkoani Mwanza, Salimu Kachimbo anasema kuna haja biashara hiyo ifanywe kwa uratibu mzuri ili kuwanufaisha wavuvi na wafanyabiashara na kuondoa sintofahamu iliyopo sasa kwa baadhi samaki kukosa thamani.

“Sisi ni wauzaji tu ila wanunuzi wakubwa ni wachina na ndiyo wanapanga bei huenda mabondo yakawa na bei kubwa kuzidi hiyo tunayouzia, hivyo ni vyema Serikali ikaliangalia suala hili kwa kina,” anasema Kachimbo.

Kwa mujibu wa kanuni za uwekezaji katika sekta ya uvuvi, wavuvi na wachuuzi ndiyo wamepewa haki kisheria ya kukusanya mazao hayo yakiwemo mabondo na kuyapeleka kiwandani na siyo wawekezaji.

Mwenyekiti wa soko kuu la Mwanza, Ahmad Nchora aansema biashara ya mabondo imeongeza ajira kwa vijana hivyo Serikali haina budi kuirasimisha ili isiwe inawanufaisha wafanyabiashara wa nje pekee ambako yanapelekwa kuliko wazawa wenyewe.

Mwenyekiti huyo anashauri pia kuwepo kwa njia nzuri za kununua mabondo hayo tofauti na ilivyo sasa ambapo wapo wengine wanayafuata ziwani na kusababisha samaki kupungua viwandani.

“Wapo wavuvi wasio waaminifu wanauza mabondo ziwani kisha samaki kuwatupa ziwani kitendo hicho ni haramu na kinasababisha kupunguza upatikanaji wa samaki viwandani lakini pia pato la Taifa kupungua kwa kuwa yanauzwa kinyemela,’ anasema Nchora.

Afisa uvuvi Wilaya ya Nyamagana, Kennedy Kitunusa anasema wawekezaji wa nje kwa mujibu wa sheria hawaruhusiwi kujihusisha moja kwa moja kwenye suala la ukusanyaji wa mazao ya samaki badala yake fursa hiyo imeachwa kwa wazawa ambao huyakusanya na kuyapeleka viwandani.

Anasema wameweka mikakati mbalimbali kuhakiisha biashara ya mabondo inafanyika kwa utaratibu mzuri ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yake. 

Enable Notifications OK No thanks