Benki Kuu yatahadharisha udanganyifu wa fedha mtandaoni
- Ni ule unaofanyika kwa kutumia barua pepe na mitandao ya kijamii.
- Unaoelekeza kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha nyingi.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watanzania kuwa makini na utapeli mpya unaofanyika kwa njia ya barua pepe unaoelekeza kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha nyingi.
BOT katika taarifa yake iliyotolewa leo Januari 6, 2022 imebaini kuongezeka kwa udanganyifu wa fedha nchini unaohusisha mwananchi kupokea taarifa (hati au barua pepe) inayodai kuwa ni uthibitisho wa malipo kupitia SWIFT na/au mifumo mingine ya uhamishaji fedha.
“Mpokeaji anafahamishwa kuwa fedha zimeingizwa kwenye benki au akaunti katika taasisi ya fedha nchini Tanzania; wakati mwingine, mpokeaji fedha anaelekezwa kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha hizo nyingi,” imeeleza taarifa ya BoT
Matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.
Benki Kuu imesema taarifa hizo ni za kughushi na za kubuni na kusema “wananchi mnashauriwa kuwa waangalifu na kuacha kujihusisha na miamala hiyo ambayo kwa kawaida inalenga kuwatapeli fedha.”
Nini kifanyike?
Pia, wananchi wanakumbushwa kuzingatia kanuni bora za kufanya miamala ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha ambazo ni kutokutoa taarifa za fedha wakati wa kutoa taarifa binafsi mtandaoni (tovuti, mitandao ya kijamii), kupitia barua pepe au kwenye simu kwa watu wasio na uhakika nao.
“Kutojihusisha kujibu barua pepe, barua au simu zinazoahidi kupokea fedha kutoka kwa watu au kampuni wasizozifahamu vizuri,” imesisitiza BoT.
Wananchi wametakiwa kuwa waangalifu wanapofanya malipo ya mtandaoni kwa kufanya uhakiki wa mshirika wa kibiashara (mtu au kampuni) kabla ya kutoa maelezo au kufanya malipo.
Aidha, wananchi waliokumbwa na matatizo hayo wanashauriwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama kwa hatua stahiki.
Tangazo:
