Mambo yatakayosaidia kuboresha mfumo wa kodi Tanzania

January 12, 2023 2:33 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wadau washauri kuboreshwa kwa sera ya kodi iendane na mazingira sasa ya biashara. 
  • Serikali yapokea mapendekezo na kwenda kuyafanyia kazi.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikisema Watanzania hawana uelewa wa kutosha kuhusu uhusiano wa kodi na maendeleo ya nchi, wadau wa kodi nchini wametoa maoni yao juu ya njia zinazoweza kumaliza tatizo hilo ikiwemo uboreshaji wa sera za kodi.

Maoni hayo yametolewa kwenye kongamano lililohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa sekta binafsi za uzalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na viongozi wa dini lililofanyika  jana(Januari 11, 2023)kwenye ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC)  jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa maoni yaliyopaziwa sauti kwenye kongamano hilo ni pamoja maboresho kwenye sera mbalimbali ikiwemo sera ya kodi ambayo imeruhusu viwango vikubwa vya kodi kwenye malighafi kutoka nje.

“Tulifanya utafiti mdogo kubaini changamoto katika sekta ya uzalishaji hasa viwanda, tukabaini kubwa ni ukosefu wa malighafi ambazo wanalazimika kuagiza nje kuna kiwanda kiliagiza malighafi zake zikatozwa kodi kwa asilima 35,”amesema Dk Donald Mmari ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti (Repoa).

Mmari ameongeza kuwa sera hizo zimeangazia zaidi ukusanyaji wa mapato na sio ukuaji wa uchumi na sekta kwa ujumla.


   Baadhi ya wadau wa kodi waliohudhuria Kongamano la Kikodi Taifa lililofanyika jijini Dar es Salaam. Picha l Wizara ya Fedha na Mipango.

Uhimilivu wa deni la taifa, mfumuko wa bei kutupiwa macho 

Serikali imeshauriwa kutupia macho mfumuko wa bei ambao unaendelea kutokea sehemu mbalimbali duniani kutokana na changamoto za kiuchumi ikiwemo vita ya Ukraine ambazo zinaweza kuathiri uhimilivu wa deni la taifa kwani kiwango cha riba kinaendelea kuongezeka.

Charles Kimei ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo ametoa Ushauri huo katika Kongamano la Kikodi ambapo amesema kiwango cha riba kimeongezeka kutoka kutoka asilimia 0.6 mwezi Septemba mwaka 2022 mpaka 5.5 Januari 2023.

“Uhimilivu wa deni utaathiriwa pia na mfumuko wa bei ambao unaendelea kuongezeka, kwa hiyo bajeti ya mwakani iangazie namna gani tutaweza kukabiliana na hayo bila kusahau viwango vya kubadilishia fedha za kigeni,” amesema Kimei.


Zinazohusiana 


Kulinda wawekezaji wa ndani na kupunguza utitiri wa kodi

Wadau hao wameishauri Serikali kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji waliopo nchini ili wapanue uwekezaji wao na hata kuwashawishi watu wengine kuwekeza jambo ambalo litachochea kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bakhresa Food Products Salim Aziz amesema bado Tanzania haijaweka mazingira rafiki kuwekeza ndio maana wawekezaji wengi wanawekeza kutokea nje ya Tanzania.

“Mbinu za ukusanyaji wa kodi, sera za kodi, na mazingira ya uwekezaji yanapaswa kutupiwa macho, sisi tumewekeza katika kiwanda cha sukari kwa fedha nyingi lakini imechukua miaka minne kupata baadhi ya vibali wakati tayari tulisharuhusiwa, “ amesema Aziz

Kwa upande wao Taasisi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa Anga Tanzania (Taoa) wameishauri Serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa waedeshaji wa shughuli za usafiri wa anga nchini kodi iliyoanza mwezi Julai 2022.

Latifa Zax ambaye aliwakilisha Taoa kwenye kongamano hilo amesema kodi ya VAT imepunguza shughuli za usafiri wa anga nchini  kwani wasafiri wengi wamekuwa wakitumia ndege za mataifa ya nje kutokana na gharama zao kuwa chini.

“Tangu mwezi Julai mwaka 2022 kutokana na kodi ya Vat, orodha ya watu wanaohitaji usafiri wa anga imepungua na hii inamaanisha hata idadi ya watalii ambao inawategemea kuwapata kwa mwaka huu haitafika,” amesema Zax.

Viongozi wa dini wanena

Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama Eliona Kimaro  ambaye naye alikuwa miongoni mwa waalikwa katika kongamano hilo amesema Serikali inapaswa kuwalinda, na kuwaheshimu wawekezaji wa sekta binafsi  kwani wamebeba hatima ya watanzania wengi.

“Naomba watendaji wa Serikali wafahamu wawekezaji wa sekta binafsi wanatakiwa kutiwa moyo na kusaidiwa na sio kuwakatisha tamaa, hawa watu wanapata misukosuko wakati mwingine, tutafute namna ya kuwafanya hawa watu wawe walipa kodi wakubwa,” amesema Kimaro kwenye kongamano hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha, na Uchumi Zanzibar Dk Saada Mkuya (aliyevaa ushungi) ni miongoni mwa waliohudhuria Kongamano hilo. Pichal Wizara ya Fedha

Serikali yapokea maoni

Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu nchemba amewaambia washiriki wa kongamano hilo kuwa Serikali imeyapokea maoni yao na kuahidi kuyafanyia kazi ambapo matokeo watayaona katika bajeti ya mwaka 2023/24.

“Bado tutakuwa na mazungumzo kati yetu na taasisi binafsi, na msingi wa kongamano hili ni kusikia haya kutoka kwenu hivyo tumeyapokea na huu sio mwisho kongamano hili litakuwa endelevu,” amesema Nchemba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kongamano hilo.


Tangazo:

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW