Dk Mpango ataja mambo 10 yatayoongeza mapato ya ndani Tanzania
- Ni pamoja kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kukusanya kodi ili kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Isdor Mpango amebainisha hatua 10 za kuzingatia ili kuongeza mapato ya ndani jambo litalosaidia kupunguza na hatimaye kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Dk Mpango aliyekuwa akizungumza leo Aprili 15, 2025 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kodi na uwekezaji jijini Dar es Salaam, amebanisha kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Taifa kutekeleza sera maalum ambazo zitahakikisha ukuaji endelevu wa pato la Taifa.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa utekelezaji wa sera hizo ni muhimu kutokana na ongezeko la watu na mahitaji yanayokua hivyo Serikali inapaswa kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa mapato hayo.
“Idadi ya Watanzania sasa inaendelea kuongezeka kwa kasi na sasa tunakadiriwa kuwa watu milioni 65 wengi wakiwa vijana lakini maana yake ni kuwa mahitaji kitaifa yanaendelea kukuwa kwa kasi kubwa,” ameeleza Dk Mpango.

Hatua nyingine aliyotaja Makamu wa Rais ni kuongeza jitihada katika kuboresha mfumo wa kodi ambao utahakikisha usawa na kuondokana na misamaha ya kikodi.
Aidha, Dk Mpango amesema kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi ili kukabiliana na vitendo vya rushwa pamoja na kukuza matumizi ya Tehama katika ukusanyaji wa kodi vitarahisisha wananchi kushiriki katika shughuli hizo.
“Tunahitaji kukuza matumizi ya tehama katika ukusanyaji wa kodi na uwekaji wa akiba, lazima tuongeze msukumo katika matumizi ya EFD,” amesema Dk Mpango.
Dk Mpango ameongeza kuwa njia nyingine ni muhimu kuboresha mazingira ya biashara ili kukuza uwekezaji hasa wawekezaji wa ndani.
Sanjari na hizo pia, Dk Mpango ameongeza kuwa kujenga kanzi data mathubuti ya taarifa za walipa kodi wa sasa na walipa kodi tarajiwa kwa kuangalia mtu mmoja mmoja, mashirika na taasisi na kufanya jitihada za kuongeza idadi ya walipa kodi kama njia ya kupunguza mzigo wa kodi.
“Ni vyema Wizara zetu Wizara za fedha, pia Wizara ya mipango na uwekezaji kuzingatia sana ushauri uliotolewa kuhusu elimu kwa wajasiliamali wetu wadogo wadogo, lakini pia kupunguza gharama za kurasimisha biashara ili zitoke sekta isiyokuwa rasmi ili ziende sekta rasmi.

Hatua nyingine iliyopendekezwa na mchumi huyo mbobevu ni kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto za kilojistiki na kisiasa katika utozaji wa kodi katika sekta isiyo rasmi, pamoja na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi, ufuatiliaji na upimaji, kwa taasisi za kodi na zile za usimamizi.
Awali Makamu wa Rais alibanisha kuwa uwiano wa mapato kwa pato la Taifa umekuwa hafifu kutoka asilimia 12 mwaka 2001/2002 hadi asilimia 14.9 kwa mwaka 2024/2025, ikiwa ni chini ya wastani kwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Dk mipango licha ya jitihada za Serikali kuongeza mapato bado kuna changamoto ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu huku idadi ya walipa kodi ikiwa ni ndogo na kusababisha makusanyo ya kodi kuwa madogo.
Kwa upande wake, Waziri Ofisi ya Rais Fedha na Mipango kutoka Zanzibar, Dk Saada Mkuya amefafanua kuwa kupitia makongamano mbalimbali ya kodi wamekuwa wakitatua changamoto zinazotajwa ikiwa lengo ni kuwarahisishia wawekezaji wa ndani na kuweka mazingira mazuri ya biashara.
Miongoni mwa mambo yaliofanyika kupitia makongamano hayo ni pamoja kupunguza ushuru wa maji sindika na kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa za nje.
Latest



