Vifahamu vijiwe 10 maarufu vya kitimoto Dar
- Vijiwe hivyo ni pamoja na Kazimoto Pork, City Pork na Meat Pork.
- Hivi ni baadhi tu maeneo unayoweza kujipatia kitimoto safi ukiwa Dar es Salaam.
- Ladha, mapishi na huduma za kipekee ndiyo zimevipa umaarufu vijiwe hivi.
Dar es Salaam. ‘Kitimoto’ sio jina lake mahususi lakini ndio jina maarufu zaidi nchini Tanzania na ukitaka kuipata kwa haraka mahali popote basi ulizia kwa jina hilo.
Nini kimekujia kichwani? Ndiyo! Ni nyama ya nguruwe, Waswahili wakaamua kuibatiza majina mbalimbali, likiwemo hilo la kitimoto kumaanisha huwa tamu zaidi ikiliwa ikiwa ya moto.
Walaji wa nyama hiyo wamesheheni pia jijini Dar es Salaam kama zilivyo sehemu nyingine. Siyo ajabu kuona mabango yakitangaza uwepo wa vijiwe vinavyouza kitoweo hicho.
Je! Wewe ni miongoni mwa watu ambao hupata changamoto ya kujua ni wapi utapata kitoweo hicho, ukala na kufurahia? Makala haya yameainisha baadhi ya vijiwe unavyoweza kupata kitimoto katika mitaa mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.
1#. Kazimoto Pork
Kijiwe cha kwanza unachoweza kupata nyama hiyo ni Kazimoto Pork kilichopo Tabata Segerea jijini hapa.
Kijiwe hiki kinasifika kwa kuwa na kitimoto kitamu unachoweza kushushia na ndizi au ugali wa moto uliopikwa umaridadi kumpa mlaji ladha ya kipekee.
Unaweza kupata kitimoto iliyochomwa, rosti, au makange aina zote. Pia kunogesha mapishi yao unaweza kupata kitimoto baga, pizza, soseji, na mishikaki ambayo yote imetengenezwa kwa nyama hiyo.
Kijiwe hicho ambacho kinapatikana Mita 400 kutoka kituo cha mabasi cha Tabata Segerea, kina huduma ya ziada ya vinywaji na kuosha magari wakati ukiwa unafurahia msosi wako.
Utamu wa kitimoto unaenda sambamba na kachumbari, pili pili na chakula cha ziada cha kusindikiza kitoweo hichoo ikiwemo ndizi. Picha| MeatPoint/Instagram.
2#. City Pork
City Pork ni kijiwe kingine maridadi cha kitimoto kilichopo Tabata na Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kijiwe hiki kina aina nyingi za upishi wa kitimoto ikiwemo mbavu, mishkaki, soseji, steki na makange. Vyote hivi ni kwa ajili ya kuhakikisha ukitoka kwenye kijiwe hicho utaibeba historia nzuri ya utamu wa nyama hiyo.
Ukiwa hapo pia unaweza kujipatia aina mbalimbali za juisi zitakazosindikiza mlo wako. Juisi za matunda, za tende, milkshakes, smoothies hata kwa wale wapenda vilevi City Pork ndiyo mahali pake.
Kilo moja ya kitimoto katika kijiwe hiki utajipatia kwa Sh14,000 mpaka Sh18,000 kutegemena na aina ya nyama utakayochagua.
Ufikaji wa kijiwe hiki ni rahisi sana, kwa tawi la Tabata ni kilomita moja tu kutoka kituo cha mabasi Tabata Bima na kwa tawi la Ubungo ni mita 290 kutoka kituo cha mabasi cha Riverside.
3#. Meat Point
linapofika suala la kuandaa kitimoto kitamu kijiwe hiki huwa hawakosei kabisa. Wana ofa nyingi na punguzo la bei litakalokuwezesha kufurahia msosi huku mfuko wako ukisalia na vichenchi vya nauli.
Kila jumanne City Point wana ofa maalum wenyewe wanaiita “Tuesday Vuruga” ambapo unajipatia kitimoto nusu kwa Sh7,000 na ndizi mzuzu za kukaanga bure.
Unaweza kusema kama vijiwe hivi vimepangana, kwa sababu mita chache tu kutoka tawi la Ubungo ilipo City Pork unakutana na kijiwe hiki kilichopo Ubungo External jijini Dar es Salaam.
Kazi inabaki kwako kuchagua wapi uende kulingana na mfuko wako na aina ya pishi la kitimoto unalotamani kula wakati huo.
Soma zaidi
-
Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD
-
Fukwe tano zisizo na kiingilio unazoweza kutembelea Dar
4#. Kitimoto Masterz
Raha ya kutembelea kijiwe hiki ipo kwenye aina nyingi ya vyakula walivyo navyo ikiwemo biriani, ugali, au wali unaosindikizwa na mboga mbalimbali kama samaki.
Ikiwa una rafiki asiyependelea kitimoto na unatamani kuongozana naye basi kijiwe hiki kitawafaa sana.
Cha kufanya ni kutembelea tu maeneo ya Kinondoni, umbali wa mita 800 sawa na mwendo wa dakika 3 kutoka Kinondoni Biafra kwa usafiri wa gari.
Kwa msimu huu wa sikukuu kuanzia Disemba 8, 2022 mpaka Januari 3, 2023, Kitimoto Masters hawatoi huduma hivyo unaweza kuchagua kijiwe kingine kati ya hivi vilivyoainishwa kwenye makala haya.
5#. Mibs Tavern
Kijiwe hiki cha kitimoto kinapatikana Sinza, mita 300 kutoka kituo cha mabasi cha Sinza kwa Remmy na ikiwa utatembea kwa miguu kutoka kituoni basi ni dakika 4 kufika kwenye kijiwe hicho.
Kinatoa huduma ya kitimoto siku zote za wiki. Ukijisikia tu kula kitimoto unaweza ukapitia na ukafurahia utamu wa nyama hiyo.
Bei zao ni kawaida ambazo unaweza kuzimudu hata ukienda na marafiki, kwa kitimoto choma hapa utaipata kwa Sh16,000. Usiniulize kuhusu robo kwa sababu huwezi kuipata wenye kijiwe hiki.
Kama si mpenzi wa kitimoto unaweza kwenda kupata upepo na kufurahia muziki mzuri, bendi zinazotumbuiza eneo hilo pamoja na mandhari nzuri ya eneo hilo linalofaa hata kwa familia au vikao mbalimbali.
Licha ya burudani yote hiyo kijiwe hiki kina sehemu ndogo ya kuegesha magari. Ikiwa utatembelea hapo siku za mwisho wa wiki ni vyema ukatafuta mapema mahali ya kuegesha ili usipate usumbufu.
Soseji za kitimoto pia ni moja kati ya kiburudisho pendwa unachoweza kujipatia kwenye vijiwe hivi vya kitimoto. Picha | City Pork/Instagram.
6#. Tango Pork Park
Kwa wale walio nje ya mji kidogo hamjasahaulika. Unaweza kupita Tango Pork Park kwa ajili ya kujipatia kitimoto safi iliyoandaliwa kwa utaalamu wa hali ya juu.
Kijiwe hiki kipo Makongo, mita 400 tu kutoka kituo cha mabasi Makongo mwisho. Pia wanafanya huduma ya kuwasambazia wateja huduma hiyo majumbani (delivery).
Unachotakiwa kufanya ni kuwapigia simu na kuwapa oda yako. Unataka kitimoto mbichi ili upike mwenyewe, au unataka kitimoto choma, makange, au rosti? kazi ni kwako.
7#. Rud’s Farm, Bar & Grill
Kama unapenda maeneo tulivu yasiyo na vurugu wala makelele mengi basi Rud’s Farm ndiyo penyewe, hapa utapata kitimoto safi wakati huo huo ukiburudika kwa utulivu ulipo maeneo hayo.
Kijiwe hiki kipo Ununio jijini Dar es Salaam. Kimezungukwa na miti ya asili na bustani ambayo hukitofautisha na vijiwe viingine.
Ikiwa unatamani kutembelea kijiwe hiki kwa usafiri wa daladala, panda magari ya Ununio shuka kituo kinaitwa Kondo kisha uchukue bodaboda au bajaj na waambie wakupeleke Rud’s Farm, ndani ya dakika nne tu utakuwa umefika.
Tangazo
8#. Kinyaiya Pork Grill
Ukiwa katikati ya jiji na unatamani kupata kitimoto safi iliyoandaliwa vizuri, basi pitia Kinyaiya Pork Grill.
Mandhari mazuri na wahudumu walio tayari kukuhudumia kwa haraka kunaweza kukufanya umalize tu utamu huo wa kitimoto hapo hapo.
Najua unajiuliza utafikaje hapa. Kama unatumia usafiri binafsi ni kilomita moja kutoka kituo cha mabasi Posta na kama utatumia daladala basi wakushushe kituo cha mabasi Mnazi Mmoja kisha vuka barabara ndani ya dakika tano utakuwa umefika kwenye kituo hicho.
9#. Containers Pub
Ni eneo zuri la kupata kitimoto kwa watu wenye haraka, wasiopenda kukaa muda mrefu kusubiri.
Kijiwe hiki ni chimbo la aina zote za kitimoto kuanzia kitiimoto chhma, makange, rosti na kavu, kipo kilomita 1.3 kutoka kwenye kituo ca mabasi cha Morocco
Ukiwa kwenye chimbo hili jihakikishie kupata chakula kwa haraka na kupata huduma nzuri kutoka kwa wahudumu ambao wako tayari kukuhudumia muda wote. Bei zao ni za kawaida zinazomuwezesha yoyote kumudu nyama hiyo.
Hata kama wewe si mpenzi wa nyama unaweza kujipatia piza iliyotengenzwa kwa kitimoto. Picha | Kazimoto Pork.
10#. Melly’s Kitimoto
Mazingira mazuri ya kijiwe hiki kilichopo Bunju Mianzini yanaweza kukuaminisha kuwa hata ‘mbuzi katoliki’ (nyama ya nguruwe) anayeandaliwa hapa atakuwa na ladha ya aina yake.
Kijiwe hiki kilichopo mita kadhaa kutoka kituo cha mabasi cha Mianzini kinatengeneza aina mbalimbali za kitimoto ikiwemo kitimoto choma, rosti makange na aina nyingine za chakula .
Ukiwa hapo usijali kuhusu sehemu ya kuegesha gari yako wanao utaratibu mzuri wa kuhakikisha usafiri wako unakuwa salama wakati wote.