Zifahamu simu mpya nne za Samsung zilizoingia sokoni

- Ni toleo jipya la simu za Galaxy S23.
- Zina uwezo mkubwa hasa kupiga picha zenye ubora wa hali ya juu.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa simu za Samsung, basi mwaka 2023 utakuwa wa kicheko kwako. Kampuni hiyo ya vifaa vya kielektroniki imezindua toleo jipya la simu za Galaxy S23.
Toleo hilo limekuja na simu nne za Galaxy S23 Ultra 512 GB ambayo itauzwa kwa Sh3.8 milioni, Galaxy S23 Ultra 256 GB (Sh3.5 milioni), Galaxy S23+ (Sh2.7 milioni) na Galaxy S23 itauzwa kwa Sh2.44 milioni.
Kamera ya simu hizi za Galaxy zitawapa watumiaji uhuru wa kuonyesha ubunifu kama vile kupiga picha zenye hadhi ya sinema nyakati za usiku pamoja na video zenye uwezo wa akili bandia (AI), teknolojia ya kujiongoza ya kisasa.
Pia mtumiaji wa simu hizi atapata fursa ya kucheza michezo mingi ya mtandaoni kwa uhuru na kumpatia picha zenye hadhi ya juu na kasi nzuri.
“Simu ya Galaxy S23 Ultra inakuja na penseli yake ambayo watumiaji wengi wa simu hizi wanafahamu na kupenda matumizi yake na uwezo wa kufanya vitu vingi kwa pensili hiyo,” imeeleza Samsung.
Simu zote hizi za Samsung zina uwezo wa kisasa wa kiteknolojia na muonekano maridhawa ambao unaendelea kuonyesha kujali kwa matumizi mbadala ya vifaa ili kutunza mazingira ambayo Samsung huzingatia.
Mkuu wa kampuni hiyo kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Manish Jangra akizungumza mara baada ya uzinduzi wa simu hizo Februari 1, 2023 amesema Tanzania ni kati ya nchi ambazo zimekuwa na mchango mkubwa wa katika kukuza bidhaa za simu zao.
“Kwa sasa suala siyo kuangalia tu ubora wa simu zetu ambazo hakika ni bora na zimekuwa zinakubalika sehemu mbalimbali duniani lakini pia kinachoangaliwa kwa sasa ni namna ambavyo simu hizi zinachangia katika maendeleo ya shughuli za teknolojia na Taifa kwa ujumla,” amesema Jangra.
Zinazohusiana
- Samsung, Huawei zinavyochuana katika soko la simu duniani
- Upo tayari kununua simu ya mkononi ya zaidi ya Sh3 milioni?
Amesema kuwa huduma zinazopatikana kwenye simu hizo ni bora na zimekuwa zikichangia katika nyanja mbalimbali za kukuza uchumi ikiwemo kamera za kisasa katika simu hizo ambazo zimekuwa zikitumiwa kwenye shughuli mbalimbali nje ya mawasiliano ya kawaida.
“Simu hizo zina uwezo mkubwa wa aina mbalimbali katika ufanyaji wake wa kazi hasa kwa kutoa picha bora hata kwenye mazingira ya giza. Ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi data na ina gallery (sehemu) kubwa yenye uwezo wa kuhifadhi picha,” amesema Jangra.
Simu hizo zina uwezo wa kumbukumbu (memory) kuanzia jigabaiti 256 (GB). Uwezo ambao ni mkubwa kuliko simu shindani. Kwa simu nyingi zilizopo sasa, uwezo wa kumbukumbu wa chini zaidi ni GB 128.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Samsung Afrika, Sung Yong Hong amesema mwaka jana simu ya Samsung Galaxy S22 ilifanya vema sokoni na kwa sasa kampuni hiyo ina imani kuwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki simu zake hizo mpya za Galaxy S23 zitauzwa kwa wingi kutokana na ufanisi wake mkubwa.
The S Pen on the #GalaxyS23 Ultra has truly expressive potential – here’s what people were ‘saying’ with it today.
Learn more: https://t.co/SE5RxyMpbZ
pic.twitter.com/NH2f2Ef9s5— Samsung Mobile (@SamsungMobile) February 2, 2023
Latest
