Yaliyomo simu mpya za Samsung mwaka 2022
- Samsung S22 Ultra yachukua nafasi ya Note.
- Ili kupata simu hiyo unahitaji zaidi ya Sh2.5 milioni.
Dar es Salaam. Ni siku chache zimepita tangu kufanyika hafla ya uzinduzi wa matoleo mapya ya bidhaa za Samsung mwaka huu. Kwa baadhi huenda matarajio hayakufikiwa baada ya bidhaa zilizozoeleka kutangazwa katika hafla hiyo kutokusikika.
Kwa muda mrefu sasa, Samsung imekuwa ikizindua matoleo ya Samsung Galaxy S sambamba na toleo la Galaxy Note. Mwaka 2022, hakuna”Note” iliyosikika.
Badala yake, Samsung imetangaza toleo la Samsung S22 Ultra ambalo huenda ndiyo mrithi wa toleo la Note kutokana na sifa zinazoambatana na simu hiyo.
Kilichoitofautisha Note na matoleo ya Galaxy S ni simu kuambatana na kalamu yake hivyo kuwa siMu mujarab kwa wadau wa grafiki, uchoraji na kazi za uandishi na ubunifu.
Makamu wa Rais wa Samsung kitengo cha menejimenti ya bidhaa za simu nchini Marekani, Drew Blackard katika hafla ya uzinduzi ya Galaxy Unpacked 2022 amesema S22 Ultra inakuwa simu ya kwanza toleo la S kuwa na kalamu.
Awali katika matoleo ya simu, kalamu ya simu ilipatikana kwenye toleo la note pekee.
S22 Ultra Inakuja katika rangi nne ikiwemo kijani. Picha| Notebook Check.
Ikilinganishwa na S21 Ultra, nini kipya kwa S22 Ultra?
Mbali na kalamu, Ultra ya mwaka huu imeambatana na sifa zingine lukuki. Blackard amesema simu hyo inaambatana na betri lenye uwezo wa mAh 5000, uwezo ambao ni sawa na Ultra 21 ya mwaka jana.
Hata hivyo, S22 Ultra inakubali kuchajiwa haraka zaidi kwani inaruhusu chaja zenye uwezo wa wati 54 tofauti na S21 Ultra inayoruhusu chaja yenye uwezo wa wati 25 tu.
Kwa uelewa zaidi, mdau wa teknolojia kutoka chaneli ya Mobile Fun amesema kuwa, chaja ya wati 54 inahitaji muda chini ya saa moja kujaza simu kwa hadi asilimia 100 huku wati 25 ikihitaji muda zaidi ya saa moja.
Kwa mtu ambaye anategemea zaidi simu yake huenda akafurahia zaidi simu hiyo kwani hatoweza kuwa mbali na simu yake kwa muda mrefu.
Mbembwe za kamera
Kupata picha za usiku kwa S22 Ultra ni kitu kidogo kwani mbwembe mpya ya “Nightography” inayoambatana na simu hiyo inasaidia kupata picha za usiku bila bugdha ya giza.
Blackard amesema, S22 Ultra inaambatana na uwezo wa kuchukua picha usiku na mbwembe zingine za kamera ikiwemo “LightRoom, Auto Focus na Pro Mode” kwa anayetaka kuwa na udhibiti wa lensi za kamera.
Mbali na mbwembwe mpya za kamera, uwezo wa kamera kwa upande wa Mega Pixel (MP) ni ule ule kama wa S21 Ultra.
Kamera kuu ina uwezo wa MP108, kamera ya mapana ina uwezo wa MP12 na kamera ya picha za mbali (telephoto) ikiwa na uwezo wa MP10 na uwezo wa kuvuta picha (zooming) kwa mara tatu hadi mara 10.
Uwezo wa uhifadhi wa kumbukumbu za muda mfupi (RAM) kwa simu hiyo unaenda hadi Jigabaiti (GB) 12 huku uhifadhi wa mafaili ukiwa hadi Terabaiti (TB) 1 ambayo ni sawa na GB 1000.
Soma zaidi:
- OnePlus 10 Pro: Simu janja itakayokata utepe mwaka 2022
- Mapinduzi: Gari inayopaa angani kuanza safari mwaka 2023
- Mbinu za kuondoa harufu mbaya kwenye gari yako
Unene wa pochi yako
Simu hii inaingia kwenye daraja la “High End phones” ikiwa chumba kimoja na kina iPhone 13 Pro Max na One Plus 10 Pro, simu ambazo zinahitaji kipato kikubwa kumiliki.
S22 Ultra kwa mujibu wa Blackard iaanza kuuzwa kwa Dola za Marekani 1,199 sawa na zaidi ya Sh2.7 milioni.
Kwa gharama hiyo unaweza kuipata simu hii yenye uwezo wa kubailiana na vumbi na maji ikiwa katika rangi nne. Rangi zilizotajwa na Samsung ni pamoja na Burgundy (mfanano wa pinki), Kijani, nyeusi na nyeupe.
Zaidi ni malighafi yaliyotengeneza simu hii. Samsung imetaja kutumia madini ya aluminiumu nyuma na pembezoni mwa simu huku mbele ikiwa na kioo aina ya “Gorilla Glass Victus.”
Pamoja na S22 Ultra, Samsung imetangaza Samsung Galaxy Watch4, Sumsung Galaxy TabS8 pamoja na Samsung Galaxy S 22 na S 22 Plus.
Tukutane madukani tukinunua au tukutane nukta.co.tz tukizichambua.
Latest