Samsung, Huawei zinavyochuana katika soko la simu duniani

February 25, 2019 8:39 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Huawei imezindua simu mpya ya Mate X zikiwa zimepita siku tano tangu Samsung kutambulisha simu za Galaxy S10  and Galaxy Fold zenye uwezo mkubwa wa kutunza taarifa na kutumia mtandao wa 5G. 
  • Mate X ina uwezo wa kujikunja pande zote mbili, muonekano mzuri wa kioo na uwezo kupakua filamu yenye 1GB kwa sekunde tatu tu. 
  • Bei ya Mate X ni takribani Sh5.9 milioni ambayo inaipiku Galaxy Fold ambayo itauzwa kwa takribani Sh4.5 milioni. 

Vijana wanaoenda na wakati ambao kwao teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ni sehemu ya maisha yao hawawezi kupitwa na matoleo mapya ya simu janja zinazoingia sokoni kila siku. 

Sasa kampuni ya Huawei wamezindua simu mpya inayojikunja na yenye uwezo mkubwa ya Mate X  ikiwa zimepita siku tano tangu kampuni ya Samsung ilipotoa simu mpya za Galaxy S10 na toleo jijinge la simu ya kujikunja ya Galaxy Fold ambazo miongoni mwa sifa kubwa ni uwezo wa kuhifadhi taarifa nyingi hadi kiwango cha GB1,024.

Mate X imezinduliwa katika mkutano wa dunia wa wadau wa simu ‘Mobile World Congress’ jana (Februari 24, 2019) katika Jiji la Barcelona, Hispania ambapo itaanza kuuzwa robo ya pili ya mwaka huu kwa takribani Dola za Marekani 2,600 (Sh5.9 milioni).

Bei hiyo ya Mate X ni zaidi ya Galaxy Fold ambayo itauzwa kwa Dola za Marekani 1,980 sawa na Sh4.5 milioni ambayo ilizua mjadala miongoni mwa watumiaji wa simu duniani kwasababu ilionekana ni ya bei kubwa.   

Lakini sasa watumiaji wa simu za Huawei, watalazimika kuvunja vibubu vyao ili kuipata simu hiyo ambayo inaakisi ukuaji wa teknolojia duniani.

Simu ya Mate X yenye uwezo wa kujikunja na kujikunjua kukupa muonekano tofauti imezinduliwa na kampuni ya Huawei ya China. Picha| Pocketlint.

Kampuni ya Huawei yenye makao yake makuu yako China, imesema  Mate X ina uwezo wa kutumia intaneti yenye kasi kubwa ya 5G na kujikunja na kuwa njembamba katika muonekano tofauti na kuwezesha kioo kuonekana katika pande zote mbili (mbele na nyuma). 

Mate X ikikunjuliwa inakuwa nyembamba kwa upana wa milimita 5.4 ambapo Galaxy Fold ina upana wa milimita 17mm. Usanifu huo unaifanya simu ya Mate X kuwa nyembamba zaidi wakati imekunjwa na kukunjuliwa ukilinganisha na Galaxy Fold ambayo itazinduliwa rasmi Aprili 26 mwaka huu.


Soma zaidi: Upo tayari kununua simu ya mkononi ya  zaidi ya Sh3 milioni?


Sifa nyingine ya simu hiyo ni kuwa ina mfumo mpya wa kamera (New Leica Camera) ili kupata picha zenye ubora wa hali ya juu, uwezo wa kutumia laini mbili za simu na kioo angavu (Flexible OLED screens). 

Katika maelezo yake, Huawei imesema simu hiyo itakuwa na mfumo endeshi wenye kasi kubwa (Kirin 980 processor) ambao utasaidiwa na intaneti ya 5G kumuwezesha mtu kupakua filamu ya 1 gigabaiti (1 gigabyte) kwa sekunde tatu tu.

Teknolojia hiyo inaenda sambamba na tolea jipya la tabiti (Tablet) yenye ukubwa wa nchi 8 kama iliyozinduliwa na Samsung ambazo zote zina uwezo wa kujikunja pande zote mbili.

Huu ndiyo muonekano wa Galaxy Fold ambayo inachuana na Mate X ya Huawei. Picha|Mtandao.

Hata hivyo, Huawei hawajaweka wazi ni wapi simu ya Mate X itauzwa, hata Marekani ambako inatumia teknolojia za viwango vya juu haijafahamika kama itafika. 

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la CNBC limesema baadhi ya Maafisa wa Marekani wameonya juu ya matumizi ya vifaa vya Huawei ikiwemo simu kwa sababu zinaiwezesha China kufanya udukuzi wa taarifa muhimu, madai ambayo kampuni hiyo imeyakana kuhusika nayo. 

Hivi karibuni, Huawei imejikuta katikati ya mkanganyiko wa Marekani na China wa kugombania matumizi ya mtandao wa 5G ambao unatajwa utaleta mapinduzi makubwa ya teknolojia duniani. 

Enable Notifications OK No thanks