Boss Nukta Africa atoa suluhu vyombo vya habari kujiimarisha kiuchumi
- Asema habari zenye ubora zitaifanya tasnia kuwa endelevu.
- Awataka wanahabari kugeukia matumizi ya takwimu kufanya maamuzi.
- Matumizi ya teknolojia za kisasa kufungua fursa zaidi kwa vyombo vya habari.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa Nuzulack Dausen amewashauri waandishi wa habari kuandika habari zenye ubora ili kuiwezesha tasnia ya habari nchini kuwa endelevu.
Amesema hatua hiyo itachangia vyombo vya habari kuaminika na jamii na kuviwezesha kujiimarisha kiuchumi huku vikitoa mchango chanya katika maendeleo ya Tanzania.
Dausen ametoa wito huo leo Mei 2, 2023 wakati akichangia katika kongamano la miaka 30 ya uhuru wa vyombo vya habari linalofanyika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar ambapo amesema tasnia ya habari itaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao lakini itategemea na aina ya maudhui yanayozalishwa.
“Uandishi wa habari hautakufa leo au kesho, hata miaka 1000…chombo kinaweza kubadilika mara kwa mara lakini uandishi wa habari utabaki. Tunapaswa kuzingatia kutoa habari bora kwa sababu hii ndiyo itafanya uandishi wa habari kuwa endelevu,” amesema Dausen.
Tasnia ya habari kwa sasa inakumbana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hivyo kuibua changamoto kwa wamiliki na waandishi wa habari kuendana na mabadiliko hayo ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen akisisitiza jambo katika kongamano la miaka 30 ya uhuru wa vyombo vya habari uliofanyika Zanzibar. Picha | Nukta Africa/Twitter.
Dausen ambaye ni mmoja wa wadau muhimu wa habari Tanzania amegusia umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuthamini habari zenye ubora na kuepukana na habari za uzushi zinasambaa kwenye mitandao ya kujamii.
“Lakini kuwaambia pekee haitoshi inabidi tutengeneze vipindi vinavyovutia…namna unavyoandaa kipindi chako dakika 3 au 5 kutokana na watazamazaji wetu ikizingatia kwamba wengi ni vijana,” amesema
Pia ameshauri matumizi ya takwimu katika uendeshaji wa vyombo vya habari na uzalishaji wa maudhui ili kuhakikisha yanafanyika maamuzi sahihi yatayokuboresha maisha ya waandishi wa habari.
Kongamano hilo linalofanyika kwa siku tatu litafikia kilele siku ya kesho Mei 3, 2023 wakati wa kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari Duniani ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi.
Wakichangia mada katika kongamano hilo, wadau mbalimbali wamepaza sauti kuendelea kuimarisha tasnia ya habari kwa kuboreshwa kwa sheria, sera, kuongeza uhuru wa kutoa maoni na waandishi wa habari kuwa wabunifu katika uzalishaji wa maudhui bora.
Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda amesema pamoja na waandishi wa habari kudai uhuru wa kujieleza na maslai mazuri wanapaswa kutimiza wajibu wao katika kutoa habari za kweli na kuepuka “uzushi na upotoshaji.”
Soma zaidi
-
Rais Samia: Posho ya kufundishia kwa walimu ni mzigo kwa Serikali
-
Jinsi unavyoweza kutengeneza picha, video kwa programu za akili bandia
Naye Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), James Marenga amesema wanaofanya upotoshaji mitandaoni kwa asilimia kubwa hawazingatii maadili ya taaluma ya habari.
Marenga ametaka wadau kuungana kukabiliana na habari za uzushi ili kuhakikisha jamii inatumia habari sahihi kufanya maamuzi katika shughuli za maendeleo.
Nukta Africa kupitia jukwaa lake la Nukta Fakti limekuwa likitoa elimu n amafunzo ya uthibitishaji habari na kuwa mstari wa mbele kukabiliana na habari za uzushi hasa zinazpsambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa akizungumza katika kongamano hilo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari katika kuboresha maslahi yao na kupanua wigo wa uhuru wa kujieleza.
Pia amewataka wadau wa habari nchini kuwa mstari wa mbele katika kutoa maoni ya uboreshaji wa sheria na kanuni zinazosimamia tasnia ya habari nchini ikiwemo Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ili ziwe na manufaa katika kazi zao za kila siku.
“Kwa upande wa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, ninawaomba wadau kujadili, kuchunguza na kubaini maeneo yenye mapungufu ndani ya sheria hiyo,” amesema Msigwa.