Makonda: Vyombo vya habari haviwezi kuwa huru bila uchumi imara
- Avishauri kutanua misuli ya kiuchumi na kuzingatia weledi wa taaluma ya habari.
- Wadau wataka ushirikiano katika kutatua changamoto za tasnia ya habari.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema vyombo vya habari Tanzania haviwezi kuwa huru bila kuwa na uchumi imara, akisisitiza umuhimu wa taasisi za habari kujijengea misingi thabiti ya taaluma na fedha ili kulinda uhuru wake.
Makonda aliyekuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Kitaifa jijini Arusha leo Aprili 30, 2026 amesema vyombo vingi vinashindwa kuwa huru kutokana na udhaifu wa kiuchumi unaotoa mwanya kwa mafisadi na wala rushwa kuvitumia kuharibu rasilimali za Taifa.
“Uchumi wa habari unapokuwa mdogo unawapa nafasi wanasiasa uchwara na wala rushwa kuwatia mfukoni,” amesema Makonda.
Amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao licha ya changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo usalama na uchumi, akiwaonya dhidi ya kurubuniwa kwa maslahi binafsi.
“Uhuru wa habari ni ngumu kuupata kama wanahabari wenyewe ni masikini. Freedom (Uhuru) tunayoipigania lazima iendane sambamba na mapambano ya kujenga uchumi imara wa wanahabari,” amesisitiza Makonda.
Kwa muda mrefu, tasnia ya habari Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushuka kwa mapato, hali inayosababisha malimbikizo ya madeni ya muda mrefu pamoja na kucheleweshwa au kutolipwa kwa mishahara kwa baadhi ya wanahabari.
Miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo ni ushindani kutoka kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanayoongeza kasi ya upatikanaji taarifa, pamoja na kupungua kwa imani ya wananchi kwa baadhi ya vyombo vya habari.
‘Tutafute njia mbadala’
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema ni wakati sasa vyombo vya habari kurejea katika misingi ya kutoa habari zenye maslahi mapana kwa umma.
Kwa mujibu wa Dausen, kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha imani ya wananchi na kuongeza uungwaji mkono wa jamii kwa vyombo vya habari.
“Tunataka ufike wakati hata chombo cha habari kikitaka kufungiwa kwa sababu ya kukosa fedha au faini basi wananchi waseme hapana hizo fedha tutachanga,” amesema Dausen.
Nukta Africa, ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya maadhimisho hayo ambapo imeshiriki katika mijadala inayounda mustakabali wa vyombo vya habari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kukuza sauti muhimu, na kuendeleza mazungumzo kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari, na upatikanaji wa taarifa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deogratius balile amesema ni vyema kwa vyombo vya habari kutafuta vyanzo mbadala vya mapato badala ya kutegemea njia za jadi kama matangazo.
Balile aliyekuwa akizungumza kwenye mjadala jana April 29, 2026 amesema hatua hiyo itasaidia kuviwezesha vyombo hivyo kujitegemea kiuchumi na kuongeza uimara wa uendeshaji wake.
“Tatizo kubwa tunalipata kwenye vyombo vya habari ni kutegemea vyanzo vya jadi kupata mapato. Tutoke huko tuangalie ni jinsi gani tunaweza kutengeneza mapato nje ya hapo,” amesema Balile.
Balile amependekeza kuwa ni vyema kwa Serikali kutenga mfuko kwa ajili ya vyombo vya habari utakaowawezesha kukopa na kufanya miradi itakayowaimarisha kiuchumi.
“Serikali itenge fedha kwenye mfuko kwa ajili ya vyombo vya habari, kama wanavyopewa kina mama, wasanii na vijana,” ameshauri Balile.
Tuongeze ubunifu
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Egbert Mkoko amesema vyombo vya habari viache kufanya kazi kwa mazoea bali viongeze ubunifu utaokavisaidia kuendelea kuwepo katika soko la ushindani.
“Ni muhimu sana kwa vyombo vyetu vya habari kuwa na timu ya ubunifu ambayo inatusaidia kujua hali ya sasa hivi ikoje na mahitaji yake ni haya. Kwa hiyo, tubadilike na tuachane na “business as usual” ambayo tumekuwa tukiifanya miaka ya nyuma ili tuendelee kuwepo kwenye soko,” amesema Dk Mkoko katika maadhimisho hayo.
Wadau wengine waliotoa maoni katika maadhimisho hayo ambayo yanafikia kilele chake leo jijini humo, wamesisitiza ushirikiano utakaosaidia tasnia ya habari kukua kwa haraka na kuboresha maslahi ya wanahabari.
“Kama tunataka tasnia ya habari ambayo ni endelevu na inayoleta matokeo lazima wote tuungane. Hiyo ndio namna pekee ya kubaki katika soko na kupata maendeleo,” ameshauri Jacqueline Lawrence, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (MOAT).
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wadau wa habari kuendesha shughuli zao huku akisisitiza ushirikiano na mazungumzo katika kutatua changamoto za tasnia hiyo.
Latest