Upotevu wa vifaa tiba Buchosa wamuibua Makala
- Agiza uchunguzi ufanyike kubaini walioiba mashine yenye thamani ya Sh80 milioni.
- Amtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buchosa ajitathmini.
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amemwagiza Katibu tawala wa Mkoa huo, Elikana Baladya kuunda tume ya kuchunguza upotevu wa vifaa tiba katika hospitali ya Buchosa itakayosaidia kupata muafaka wa jambo hilo.
Amos Makalla aliyekuwa akizungumza wakati wa kujitambulisha kwa watendaji na watumishi wa Halmashauri ya Buchosa Juni 5, 2023 amewaambia amebaini uwepo wa wafanyakazi wasio waaminifu ambao huiba vifaa tiba vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya kutibu wananchi.
Miongoni mwa vifaa vilivyoibiwa ni pamoja na mashine ya kisasa ya vipimo (Portable-ultrasound) yenye thamani ya Sh80 milioni ambayo ilirejeshwa hospitalini hapo baada ya kuanza kufuatiliwa.
“leo hicho kifaa kimoja kimepatikana, hatuwezi kujua hivyo vifaa vingine viko salama kiasi gani, namwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa na vyombo vingine waunde kamati ya kuchunguza vifaa vyote vya hospitali na vituo vya afya, na waliohusika kuiba kifaa hicho wafuatiliwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Makalla
Timu hiyo ya wataalamu wa afya itakayoongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa imetakiwa kufanya kazi ya kuchunguza na kuhakiki vifaa vyote vya hospitali na vituo vya afya ndani ya siku saba kuanzia leo Juni 7, 2023.
Soma zaidi
-
Takukuru yanusa upigaji miradi 22 ya maendeleo Mwanza
-
Rais Samia aziagiza Takukuru, Zaeca kufuatilia na kuichukulia hatua miradi yenye kasoro
Pamoja na kuundwa kwa tume hiyo Makalla amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buchosa kutafakari utendaji kazi wake kutokana na mfululizo wa matukio ya kupotea na kurejeshwa kwa vifaa katika hospitali zilizopo wilayani humo.
Mwanza inaendelea kukabiliwa na changamoto ya rushwa na ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi kwa kuwa miezi miwili iiliyopita Takukuru mkoani walibainimiradi 22 yenye thamani ya Sh6.5 bilioni kuwa na kasoro za utekelezaji.
Sambamba na hilo, Makalla ambaye amehamihishiwa mkoani Mwanza akitokea Dar es Salaam amewataka viongozi wa dini kuchunga ndimi zao wanapotoa mafundisho yanayohamasisha waumini wao kupuuzia matibabu yanayotolewa hospitalini.
Kwa mujibu wa Makalla baadhi ya viongozi wa dini wanawaaminisha waumini wao kutoamini tiba za wataalamu wa afya badala yake wanapougua waende kwenye maombi ambako watapokea uponyaji.
“Ni wahubiri ambao hawaamini kwenye tiba za wataalamu wa afya na wengine kudiriki kuwaambia wazazi wasiwaandikishe watoto wao shule, mahubiri ya namna hii hayafai, nimwagize katibu tawala wa Mkoa kufuatilia suala hili kwa undani kisha hatua zianze kuchukuliwa,” amesema Makalla